July 8, 2024

Waziri Dk Mwakyembe aingilia kati sakata la TCRA na kampuni na visimbuzi

Akanusha uvumi wa kufungiwa kwa visimbuzi vya Azam, Zuku na DSTV.

  • Asisitiza ni haki ya mtanzania kupata habari bila kulipia habari hiyo.
  • Akanusha uvumi wa kufungiwa kwa visimbuzi vya Azam, Zuku na DSTV.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amezitaka kampuni za visimbuzi vya kampuni za Multichoice Tanzania (DStv), Simbanet Tanzania (Zuku) na Azam zilizozuiwa kuonyesha chaneli za ndani kuomba muongozo kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iwapo zinapenda kuendelea kubeba na kuonyesha maudhui ya chaneli hizo.

Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe imekuja baada ya kuendelea kuwepo sintofahamu katika sekta ya habari kutokana na uamuzi wa TCRA kukusudia kuzifuata leseni za kampuni hizo zilizokuwa zimekiuka sheria kwa kubeba na kuonyesha chaneli zinazotazikiwa kutazamwa bure (Free-to-Air (FTA) katika huduma za kulipia.

Dk Mwakyembe amewaambia wanahabari leo (Agosti 14, 2018) haikuwa vyema kwa kampuni hizo kuonyesha na kulipisha chaneli “kichinichini” kwa kuwa isingewasaidia na zaidi walipashwa kufuata utaratibu wa leseni zao zinazowataka kutoonyesha chaneli za ndani zaidi ya televisheni ya Taifa pekee ya TBC1.

“Kama wanahamu sana na soko wasifanye kichinichini hazisaidii waombe mwongozo toka TCRA, wapewe kanuni na sheria zilizowekwa na bunge ili wazifuate,” ameeleza Dk Mwakyembe.

Tayari DStv, Azam na Zuku wameshatoa chaneli zote za ndani katika visimbuzi hivyo kutii agizo hilo la TCRA.

Waziri huyo amesema wananchi wana haki ya kupata taarifa bila vikwazo na Serikali inatafuta njia nzuri ya kutatua changamoto zilizojitokeza ili kuhakikisha wanaohusika wanatoa huduma za mawasiliano na kutimiza wajibu wao. 

Katika mkutano huo uliolenga kuendelea kutoa ufafanuzi juu ya sakata la kuondolewa chaneli za ndani katika visimbuzi vya DStv, Zuku na Azam, Dk Mwakyembe ameitaka TCRA na kampuni za Zuku, Azam na Multichoice kukaa meza moja ili kumaliza tofauti zao na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata haki ya kuhabarika.  

Amesema kuwa kampuni hizo zinarusha matangazo yao kutoka nje ya nchi na kwamba iwapo wanataka kupata sifa ya kubeba chaneli za ndani walete mitambo yao nchini na kuomba leseni ya kurusha chaneli za ndani kama ilivyo kwa kampuni za Basic Transmission Ltd (Continental na Digitek), Star Media (Startimes) na Agape Associates (Ting).

“Kama wangekuwa wanaonyesha chaneli za ndani bure baada ya kifurushi cha kisimbuzi kuisha wangetupa ugumu kwenye maamuzi ya kuchukua hatua dhidi yao,” amesema.

         Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dk Harisson Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari picha| fullshangweblog.com.

Alipoulizwa Serikali itachukua hatua gani kwa kampuni zilizowatoza wananchi kutazama runinga zinazotakiwa kutazamwa bure, Dk Mwakyembe amesema jukumu  la kumlipa mteja ni la mwenye visimbuzi lakini watajaribu kuongea na Mwanasheria wa Serikali kupata ushauri wa kisheria wa hatua ya kufanya kwa wale ambao walishalipia na sasa hazionyeshwi tena.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe alizitaka kampuni hizo kuwarudishia wateja wao fedha za vifurushi vya visimbuzi walivyokuwa wamelipia baada ya kuondoa chaneli hizo za ndani kutokana na kukiuka masharti ya leseni zao. 

Hata hivyo, Dk Mwakyembe amesema hakuna kampuni iliyofungiwa mpaka sasa kinyume na uvumi unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii wa kufungia kwa baadhi ya kampuni zinazotoa huduma ya visimbuzi kwa wateja wao. 

“Visimbuzi havijazuiliwa, tumekataza ambavyo leseni zao hazijaruhusu na wameshaondoa hizo chaneli za bure zinazozalisha maudhui ambazo ni za bure katika visimbuzi vyao na kubakia na TBC ambayo ni lazima kutokana na masharti waliopewa katika leseni,” amesema Dk Mwakyembe