Waziri Makamba ziarani kukagua uharibifu wa mazingira
Ziara hiyo kuanisha maeneo yatakawekwa kwenye uangalizi wa mazingira nyeti
- Ziara hiyo kuanisha maeneo nyeti yatakayosimamiwa na Serikali
- Ni hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba anatarajia kuanza ziara katika mikoa 19 kukagua na kutathmini maeneo yatakayowekwa kwenye usimamizi maeneo nyeti ya mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi..
Katika ziara hiyo ambayo inaanza leo (Agosti 20, 2018), Waziri Makamba atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Halmashauri husika kuhusu maeneo yanayopendekezwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.
“Sheria ya Mazingira, hasa vifungu vya 47, 51, 54, 56, na 58 (3), inatoa mamlaka kwa Waziri mwenye dhamana ya mazingira kutangaza, kutamka au kuamuru, kupitia kwenye Gazeti la Serikali, baadhi ya maeneo nchini kuwa ni Environmental Protected Areas au Environmental Sensitive Areas (Maeneo yenye usimamizi nyeti wa mazingira),” ameandika Waziri Makamba kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inampa mamlaka Waziri kutangaza eneo lolote ambalo liko katika hatari ya kuharibika au kutoweka, kuwa chini ya usimamizi wa serikali ili kuepuka uharibifu wa mazingira unaoweza kutokea na kuhatarisha mfumo wa maisha ya binadamu na viumbe wengine.
Maeneo ambayo yanawekwa kwenye uangalizi ni pamoja na vyanzo vya maji, mito, maziwa, mabwawa, milima na vilima, chemichemi, ardhi oevu, mazalia ya samaki na misitu ambayo haina ulinzi wa Sheria nyingine.
Maeneo mengine ni ardhi kame au nusu kame, ardhi yoyote ambayo imeidhinishwa na Baraza la Ardhi kuwa haipaswi kuendelezwa kutokana na hali yake ya kuharibika kwa urahisi, eneo lenye mteremko wenye mwinamo unaozidi pembe yoyote ambayo Waziri atabainisha. Pia maeneo ambayo Waziri amezuia ufugaji, makazi, kilimo na shughuli zingine zinazohatarisha utunzaji wa mazingira.
Ukataji miti ni sababu kubwa ya uharibifu wa mazingira. Picha| Yourcommonwealth
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, baada ya Waziri kutangaza maeneo ambayo ataona yanafaa kuwa chini ya usimamizi wa mazingira nyeti, mtu yeyote atakayekataa au kupuuza taratibu zilizowekwa kusimamia maeneo hayo atakuwa anatenda kosa.
“Baada ya ziara hizi, natarajia kuyaona maeneo hayo, kutathmini hoja na haja ya kuyahifadhi na kuzungumza na viongozi wa mikoa, halmashauri na wananchi katika maeneo hayo ili kubaini utashi, uwezo na utayari wao wa kushiriki uhifadhi pale tutakapoyatangaza” ameandika Waziri Makamba kwenye ukurasa wa Twitter. .
Awamu ya kwanza ya ziara hiyo ambayo inaanza leo (tarehe 20 Agosti hadi tarehe 6 Septemba 2018) inajumuisha mikoa ya Singida, Tabora, Simiyu, Geita, Mwanza, Mara, Arusha, na Manyara. Mikoa hiyo inatajwa kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu hasa uchimbaji wa madini, kilimo na ufugaji usiozingatia taratibu za kisheria, jambo linaloathiri uhai wa viumbe na maisha ya kila siku ya binadamu.
- Megawati 300 za umeme wa upepo kuchagiza ukuaji wa viwanda Tanzania
- Teknolojia ya utengenezaji mkaa mbadala inavyoweza kupunguza ukataji miti
Maeneo ambayo yamewekwa chini ya usimamizi wa mazingira nyeti mpaka sasa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mbuga ya wanyama ya Selous na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro. Eneo lingine ni Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Mafia ambayo ilitangazwa rasmi mwaka 1995 kama eneo lililo chini ya uangalizi maalum ambapo maeneo yote hayo yanatambulika kuwa miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia (World Heritage Sites) ambayo yako hatarini kutoweka.
Changamoto ya uhifadhi wa maeneo hayo nyeti ni shughuli za binadamu. Mathalani, serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la kuzalisha umeme wa megawati 2,100 kwenye maporomoko ya maji ya Stiegler Gorge yaliyopo ndani ya mbuga ya wanyama ya Selous.
Taasisi za kimataifa na wanaharakati wa mazingira kwa nyakati tofauti wameukataa mradi huo wakidai siyo rafiki kwa mazingira na endapo utatekelezwa utaliondoa eneo hilo kwenye maeneo machache ya urithi wa dunia.