November 24, 2024

Waziri Mpina aagiza kuvunjwa Bodi ya soko kuu la samaki Feri

Uamuzi huo unatokana na kamati ndogo aliyounda kuchunguza mwenendo na utendaji wa soko hilo na kubaini changamoto kuu za sheria, muundo ya uendeshaji wa soko, mfumo wa mapato ya uvuvi na mazao ya uvuvi.

  • Amegiza ukarabati wa miundombinu ya soko hilo hadi kufikia mwisho wa mwaka wa bajeti 2018/19 uwe umekamilika.
  • Uchimbaji wa matundu 24 ya vyoo utaanza mara moja katika soko la Feri ili kukidhi mahitaji ya huduma hiyo sokoni hapo.
  • Bodi hiyo ilijipanga kupeana milioni 20 kwa kila mtu mwisho wa mwaka wa bajeti 2018/2019 sawa na milioni 180 kwa watu 9.
  • Wavuvi wamelalamika kukosa uwakilishi katika bodi hiyo, jambo linalowanyima fursa ya watu wa kuwatetea katika shida zao.

Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameiagiza Manispaa ya Ilala kuvunja Bodi ya Soko Kuu la Samaki la Feri na menejimenti mpya itatengenezwa ili soko hilo liendeshwe katika misingi ya sheria na kukuza mapato ya Serikali.

Hatua hiyo inatokana na Kamati iliyoundwa wiki chache zilizopita kuchunguza mwenendo na utendaji wa soko ambapo imebaini kuwa kuna changamoto kuu za sheria, muundo ya uendeshaji wa soko, mfumo wa mapato ya uvuvi na mazao ya uvuvi.

“Tumeona changamoto katika muundo wa bodi ya soko,” amesema John Komakoma, mwenyekiti kamati ndogo ya uchunguzi iliyoundwa na bodi.

Bodi hiyo ambayo imeundwa na sheria ndogo za Manispaa ya Ilala kwa lengo la kusimamia soko hilo mara baada ya kuanzishwa kwake kipindi cha Rais Benjamin Mkapa, na Serikali ikaamua kuwakabidhi Manispaa ya Ilala kuliendesha soko hilo.

Hata hivyo imeonekana kuwa Manispaa ya Ilala imeshindwa kuliendeleza mpaka kupelekea soko kutokuendelea na kukumbwa na changamoto nyingi za miundombinu.

“Tulilikabidhi soko kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, hatujaridhika na usimamiaji wa soko,” amesema Emmanuel Buyai, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi ambaye aliambatana na waziri katika ziara hiyo.

Hata hivyo Buyai amemshukuru waziri kwa hatua ya kuunda kamati iliyoibua madudu yaliyokuwepo katika menejimenti na bodi katika soko kuu la samaki Feri.

  Wavuvi wakifuatilia kwa makini maagizo ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (hayupo pichani) wakati akitoa mrejesho wa kamati ndogo iliyochunguza changamoto za soko la Feri jana Jinini Dar es Salaam. Picha| Zahara Tunda.

“Bodi hiyo ilijipanga kupeana milioni 20 kwa kila mtu mwisho wa mwaka wa bajeti 2018/2019 sawa na milioni 180 kwa watu 9,” amesema Mpina.

Kutokana na hali hiyo ya pesa wanazopata wanabodi imebainika  haziendani na utendaji wao wa kazi katika kusimamia miundombinu mbalimbali iliyopo sokoni hapo, ikiwemo vyoo ambavyo vilijengwa kuwahudumia watu 2,000 lakini kwa sasa vinatumiwa na watu hadi 15,000.

Aidha, Waziri amemuagiza Katibu Mkuu katika wizara yake pamoja na Mkurugenzi wa Uvuvi wasimamie ujenzi wa vyoo vyenye matundu 24 ili kusaidia watumiaji wa soko hilo.

Pamoja na hayo ameitaka Manispaa ya Ilala kuhakikisha wanaboresha na kufanya ukarabati wa  miundombinu ya soko hilo kabla ya kuisha mwaka wa fedha wa 2018/2019.

“Mpaka Juni 30, 2019, miundombinu ya vyoo na marekebisho mengine yawe yamekamilika,” ametoa maelezo Mpina ambayo yanayotakiwa kufanyiwa kazi mara moja.


Zinazohusiana:


Upande wa wadau wa Soko la Feri na wavuvi wametoa kilio chao cha kutaka kukaa meza moja na Waziri Mpina ili waweze kufanya kazi vizuri na kumpelekea changamoto wanazokupambana nazo katika soko hilo.

Vilevile wavuvi wamelalamika kukosa uwakilishi katika bodi hiyo, jambo linalowanyima fursa ya watu wakuwasemea au kuwatetea katika shida zao.

“Kero yetu ni kwa uongozi wa soko kuanzia Meneja na Bodi ya soko wote ondoa, nimeomba eneo la kujenga ofisi ya wavuvi wameninyima,” amesema Amiri Amani, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wavuvi Wadogo Wadogo (UWAWAKI).

Malalamiko hayo yanakuja mara baada ya Rais John Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli kuwapatia wavuvi wadogo kiasi cha milioni 25 kwa ajili ya kujenga ofisi ya UWAWAKI na wakina mama wajasiriamali wanaofanya kazi ndogondogo hasa ya mamalishe kwenye eneo hilo.