October 6, 2024

Wenye ulemavu wapewa siri ya kujikwamua kiuchumi

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya ya watu wenye ulemavu, Stella Ikupa amesema namna ya pekee ya watu wenye ulemavu kuondokana unyanyasaji ni kujiimarisha kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na kuachana na utegemezi.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu), Stella Ikupa  akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu, Kayanda Ibrahim alipowasili wilaya ya Pangani kwa ajili ya ziara kukgua utekelezaji wa masuala ya Ukimwi na wenye ulemavu. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Watakiwa kuacha utegemezi, bali wachangamkie fursa za mikopo.
  • Pia watakiwa kuanzisha miradi ya kiuchumi kujikwamua kimaisha.
  • Serikali yasema itaendelea kuwashika mkono ili wapate haki zao zote. 

Dar es Salaam. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya ya watu wenye ulemavu, Stella Ikupa amesema namna ya pekee ya watu wenye ulemavu kuondokana unyanyasaji ni kujiimarisha kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na kuachana na utegemezi. 

Ikupa aliyekuwa akizungumza jana (Oktoba 3, 2019) mkoani Tanga, amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kuchangamkia fursa za mikopo zitolewazo na Serikali pamoja na wadau mbalimbali ili ziwasaidie kuboresha maisha yao.

“Kwa muda mrefu sasa watu wenye ulemavu nchini wamekuwa wakinyanyaswa na kunyimwa haki zao za ajira, elimu, afya na kufikia wakati jamii kuwaficha badala ya kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao na kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali ili waweze kujikwamua kiuchumi kuondokana na hali ya utegemezi.”amesema Ikupa.

Naibu Waziri huyo amesema Serikali inaendelea kutekeleza sheria namba 9 ya mwaka 2010 inayohusu haki na ulinzi kwa watu wenye ulemavu na kuhakikisha wanapatiwa haki zote ikiwemo ajira, elimu, afya na utengamao wa maisha yao ili kuondokana na dhana potofu ya utegemezi kwa kundi hilo.


Soma zaidi: 


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali imeendelea na jitihada za kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kuwatengea asilimia mbili katika kila Halmashauri nchini ambazo zinatumika katika kuwapatia mikopo kupitia uundwaji wa vikundi vinavyotambulika kisheria.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah amesema wanafanya jitihada kuhakikisha wanawafikia wenye ulemaviu katika kuwapatia mahitaji yao ikiwemo, elimu na kuwapa nafasi katika fursa mbalimbali zinazojitokeza katika Wilaya yake.

“Hadi sasa Wilaya yetu ina watu wenye ulemavu zaidi ya 700 hivyo ni wakati sahihi kuona namna kundi hili linaangaliwa na kupatiwa elimu ya ujasiriamali ili waweze kujikimu katika mahitaji yao na familia zao kwa ujumla,” amesema Abdallah.