November 24, 2024

WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania

Wanautumia mtandao huo kutangaza biashara zao na kuwafikia wateja popote walipo ili kuongeza mapato.

  • Wanautumia mtandao huo kutangaza biashara zao na kuwafikia wateja popote walipo ili kuongeza mapato.
  • Wataalam wa masoko washauri wafanyabiashara wadogo kutumia ‘WhatsApp Bussiness’ na mitandao mingine kuwafikia watu wengi zaidi.
  • Vijana wahimiza kutumia vizuri fursa za mitandao ya kijamii kujiajiri na kujikwamua kimaisha.

Dar es Salaam. Mtandao wa WhatsApp umekuwa jukwaa muhimu kwa watu wa rika tofauti kukutana na kubadilishana mawazo na kupeana mawasiliano yanayotumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo. 

Kutokana na ukweli kuwa jukwaa hilo la mtandaoni linawakutanisha pamoja watu waliopo maeneo tofauti, baadhi ya vijana wameanza kulitumia kupenyeza biashara zao ikiwa ni hatua ya kujitangaza na kupata wateja. 

Inawasaidia kuachana na mfumo wa zamani wa kusubiri wateja waje dukani na kuingia katika ulimwengu wa teknolojia inayorahisha kazi ya kufahamu tabia za wanunuzi wa bidhaa na mambo wanayopenda ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku. 

Upendo Mosses, mjasiriamali  kutoka Nanyori Food Products inayosambaza matunda ya ‘Strawberry’ (tunda nyanya) naye ameamua kutumia WhasApp kama soko ambapo huyatumia makundi ya mtandao huo na watu anaofahamiana nao kuwafikishia bidhaa popote walipo.

Matunda ya Strawberry yamejipatia umaarufu kwa miaka ya hivi karibuni kwa sababu ya faida zake ikiwemo kuchochea ukuaji wa kinga ya mwili pamoja kusaidia ulinzi dhidi ya kansa, upofu, na kuzeeka mapema.

Kupitia WhatsApp, Upendo ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam amekuwa akiwafikia wateja wengi ambao wako maeneo mbalimbali Tanzania lakini hawawezi kuyapata matunda hayo kirahisi. 

“Mimi biashara yangu sijaanza muda mrefu sana lakini niliona nianzie kwa kutumia WhatsApp hasa baada ya kuona fursa ya kuweza kupata wateja,” anasema Upendo.

Baadhi ya bidhaa ambazo Nanyori Food Products wanauza kwa kupitia WhatsApp. Picha| Upendo Mosses

Anaamini mafanikio ya biashara yake ambayo inamuingizia kipato cha kujikimu kimaisha imechangiwa zaidi na mtandao huo wa kijamii ambao kwa sehemu kubwa umechukua nafasi mawasiliano yanayofanywa na ujumbe mfupi wa simu (SMS) wa kampuni za simu.

“Nina mpango wa kuhamia na kujitangaza katika mitandao mingine, kama Twitter na Instagram ila kwa sasa najitanua zaidi kwenye soko la WhatsApp,” anasema Upendo. 

Pamoja na kupata wateja wengi kupitia WhatsApp bado anakumbana na changamoto ya baadhi ya watu kutothamini biashara yake wakati akiitangaza kwenye makundi mbalimbali.  

Bado hajakata tamaa kwasababu amegundua kuwa tabia za wateja zimetofautiana lakini anaendelea kuimarisha huduma kwa wateja ikiwemo kutumia lugha nzuri na kutoa elimu kumfikia na kukidhi mahitaji ya kila mteja anayekutana naye mtandaoni.  


Zinazohusiana: 


Ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya WhatsApp, wataalam wa mifumo ya manunuzi wanapendekeza wafanyabiashara kujiunga na App ya WhatsApp Business ambayo inamsaidia mjasiriamali kuwafikia wateja waliokusudiwa na kuepusha changamoto za kutumia muda mwingi kuwashawishi watu ambao hawako tayari kutumia bidhaa husika. 

“WhatApp Bussiness ni kwa ajili ya huduma ya kujitangaza kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo, hivyo watumie vizuri fursa hiyo,” anasema Mevin Paulose, Mtaalam wa masuala ya masoko kutoka mtandao wa Quora.

Wakati wajasiriamali wanawaza kutanua masoko mtandaoni, wana kila sababu ya kuboresha ubora wa bidhaa na vifungashio ili kuongeza mvuto kwa watumiaji.