October 6, 2024

WHO kutathmini upya marufuku ya kutoka nje kudhibiti Corona

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO), linakusudia kuchapisha mwongozo wenye taarifa za kuwezesha nchi kuchukua hatua za kupunguza kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19)

  • Imesema baadhi ya nchi zinazohatarisha haki za binadamu, na nyingine hata kusababisha watu kushindwa kujipatia kipato.
  • Itatoa mwongozo utakaotumiwa na nchi kulingana na hali ya maambukizi ya ugonjwa huo.
  • Hiyo itasaidia watu kufurahia uhuru wao.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO), linakusudia kuchapisha mwongozo wenye taarifa za kuwezesha nchi kuchukua hatua za kupunguza kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19)  na kuhakikisha haki za binadamu  zinazingatiwa ili kuwawezesha wananchi kupata kipato.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi.

Dk Tedros amesema hatua hiyo inazingatia ukweli kuwa mataifa mbalimbali katika kukabiliana na COVID-19, yamechukua hatua nyingine zinazohatarisha haki za binadamu, na nyingine hata kusababisha watu kushindwa kujipatia kipato.

“Unaishi vipi kwenye marufuku ya kutoka nje ilhali unategemea kibarua ili uweze kupata chakula? Ripoti mpya kutoka maeneo mbalimbali dunia zinaelezea jinsi gani watu wako hatarini kusalia bila chakula,” amesema Dk Tedros.

Amesema, shule nazo zimefungwa ambapo watoto bilioni 1.4 hawako shuleni hali ambayo amesema imesitisha mafunzo yao, huku ikifungua milango ya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto na wengine wakikosa mlo ambao walizoea kupata shuleni.

Dk Tedros amesema kwamba suala la kuzuia watu kuchangamana ni moja tu ya mikakati lakini kila serikali inapaswa kutathmini mazingira yake, huku ikilinda raia wake hususan wale walioko hatarini zaidi.

Ni kwa mantiki hiyo amesema mkakati huo mpya unaweka kwa muhtasari kile ambacho wamejifunza na kubainisha hatua za kuchukua ambapo kuna vipengele sita ambavyo nchi zinapaswa kuzingatia pindi zinapotaka kuondoa vikwazo au marufuku zilizowekwa katika kudhibiti COVID-19.


Zinazohusiana:


Mwongozo huo unapendekeza kuwa maambukizi yanadhibitiwa, mifumo ya afya iliyopo ina uwezo wa kutambua, kuchunguza, kutenga na kutibu kila mgonjwa na mwambata wake na tatu, Hatari za mlipuko zinapunguzwa hasa kwenye maeneo ya hospitali, vituo vya afya na makazi ya kuuguza.

Pia kinga iwepo maeneo ya makazini, shuleni na kwingineko ambako ni lazima watu waende. Kuwepo na hatua za kudhibiti maambukizi yanayoletwa na hatimaye jamii zielimishwe vya kutosha na ziwezeshwe kuendana na mazingira mapya yaliyojitokeza.

WHO imesisitiza kuwa kila nchi inapaswa kutekeleza mikakati ya kina ya kupunguza maambukizi na kuokoa maisha, kwa lengo la kuwa na kiwango cha chini cha maambukizi na hatimaye kutokomeza kabisa maambukizi.