WHO sasa yaingia Whatsapp kutoa taarifa za Corona
Shirika la Afya Duniani (WHO) limezindua huduma ya ujumbe mfupi wa maneno (meseji) kwa kushirikiana na mitandao ya kijamii ya WhatsApp na Facebook ili kuwalinda watu dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona.
Watu wenye uhitaji wa kuzipata ambapo watatakiwa kujiunga kwa kutumia kiunganishi hiki shorturl.at/nQY23 au kwa kutuma neno “hi” kwa namba hii +41 79 893 18 92 kwa WhatsApp. Picha|Wired.
- Shirika hilo limeshirikiana na Whatsapp na Facebook kutoa huduma ya meseji za WhatsApp.
- Taarifa hizo ni pamoja na zile za watu wanaoambukizwa, kufariki na jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo hatari.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limezindua huduma ya ujumbe mfupi wa maneno (meseji) kwa kushirikiana na mitandao ya kijamii ya WhatsApp na Facebook ili kuwalinda watu dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona.
Huduma hiyo iliyozinduliwa jana (Machi 20, 2020) inalenga kuwafikia watu bilioni 2 na kuwawezesha kupata taarifa sahihi za Corona moja kwa moja katika simu zao kupitia mtandao wa WhatsApp.
“Kutoka kwa viongozi wa Serikali hadi kwa wafanyakazi wa afya, familia na marafiki, huduma hii ya meseji itawapatia habari za papo kwa papo na taarifa muhimu za virusi vya Corona ikiwemo undani wa dalili na jinsi watu wanaweza kujikinga wao na wengine,” inaeleza taarifa ya WHO.
Pia huduma hiyo inatoa taarifa za hali halisi ya ugonjwa ikiwemo idadi ya watu wanaoambukizwa, kufariki kila siku na kuzisaidia Serikali na watoa maamuzi kuwakinga watu wao.
Zinazohusiana:
- WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania
- Wadau mtandaoni watoa neno WhatsApp kudhibiti habari za uongo
WHO imesema taarifa hizo zitawafikia tu watu wenye uhitaji wa kuzipata ambapo watatakiwa kujiunga kwa kutumia kiunganishi hiki shorturl.at/nQY23 au kwa kutuma neno “hi” kwa namba hii +41 79 893 18 92 kwa WhatsApp.
Baada ya hapo utaanza kupokea taarifa zote za Corona katika kiganja chako zitakazokusaidia kufanya maamuzi sahihi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Mfumo huo wa meseji umetengenezwa na WHO kwa kushirikiana na taasisi ya Praekelt.Org kwa kutumia teknolojia ya “Turn” (mashine inayotumia kompyuta kusoma tabia za watu).