November 24, 2024

WHO yataka tafiti zaidi kuhusu madhara plastiki kwa binadamu

Imesema maji ya chupa yana chembechembe nyingi za plastiki ikilinganishwa na maji ya bomba lakini kitisho kibwa kwa sasa kwa afya za binadamu siyo plastiki bali ni maji yasiyo safi na salama

  • Imesema maji ya chupa yana chembechembe nyingi za plastiki ikilinganishwa na maji ya bomba.
  • Imesema kitisho kikubwa kwa afya za binadamu kwa sasa siyo plastiki bali ni maji yasiyo safi na salama. 
  • Imetaka tafiti zaidi kuondoa utata wa plastiki zinazopatikana kwenye maji ya kunywa. 

Dar es Salaam. Shirika la afya ulimwenguni (WHO) limesema tafiti zaidi zinahitajika kubaini madhara ya taka za plastiki zinazopatikana kwenye mazingira, huku likibainisha kuwa kwa sasa kitisho kikubwa kwa afya za binadamu ni maji yasiyo safi na salama. 

WHO kupitia tafiti yake ya athari za uchafu wa chembechembe za  plastiki kwa binadamu limeeleza kuwa plastiki zinapatikana katika mazingira ya viumbe vya baharini, katika maji taka na maji safi, chakula na hewa na maji ya kunywa iwe ya chupa au bombani.

“Kwa kawaida chembechembe hizo za plastiki ni zile ambazo ni chini ya milimita tano kwa urefu na idadi kubwa hupatikana katika maji ya kunywa vikitokana na vipande vidogo vya chupa za plastiki za maji,” inaeleza WHO katika utafiti huo.

WHO imesema kwa kuzingatia taarifa za sasa,  uwepo wa chembechembe hizo hauhatarishi afya kwa viwango vya sasa lakini utafiti zaidi unahitajika.


Zinazohusiana:


Katika taarifa iliyotolewa na Bruce Gordon kutoka kitengo cha afya ya umma, cha WHO, amesema kwa sasa hatari kubwa kuliko chembechembe hizo za plastiki ni maji yasiyo safi na salama alama huku yakiathiri watu bilioni 2 duniani kote na kusababisha vifo vya watu milioni moja kila mwaka. 

Ameongeza kuwa muorobaini ni kuweka mifumo bora ya kuchuja maji na hivyo kupunguza uchafuzi wa plastiki ndogo ndogo kwa asilimia 90.

Kwa sasa WHO imejikita katika utafiti wa  maji ya kunywa huku ikibainisha kuwa maji ya chupa yana chembechembe nyingi za plastiki ikilinganishwa na maji ya bomba.

Hata hivyo,  imetoa angalizo dhidi ya kufikia uamuzi kwani chembechembe zinazopatikana kwenye maji ya chupa za plastiki ni aina ya plastiki inayotumika kutengeneza chupa za plastiki na aina nyingine inatumika kutengeneza vikombe kwa hiyo utafiti zaidi unahitajika kuelewa plastiki hizo zinatoka wapi.