July 8, 2024

Wingi wa vyuo vikuu unavyoshindwa kuhimili viwango vya ubora

Ndani ya miaka 10 iliyopita idadi ya vyuo vikuu imeongezeka kwa asilimia 51 lakini ubora umekuwa kikwazo kikubwa cha ukuaji.
Kozi 75 zafungiwa udahili mwaka wa masomo 2017/2018 kutokana na vyuo kutokidhi vigezo.

  • Ndani ya miaka 10 iliyopita idadi ya vyuo vikuu imeongezeka kwa asilimia 51 lakini ubora umekuwa kikwazo kikubwa cha ukuaji.
  • Kozi 75 zafungiwa udahili mwaka wa masomo 2017/2018 kutokana na vyuo kutokidhi vigezo.

Dar es Salaam. Kupata nafasi ya kusoma elimu ya juu miaka 15 iliyopita lilikuwa ni suala la kufa au kupona. Ni wachache tu waliweza kupata fursa ya kwenda chuo kikuu kutokana na uhaba wa nafasi za udahili licha ya kuwa baadhi walikuwa na fedha za kujisomesha na ufaulu mzuri.

Lakini kwa sasa mambo ni tofauti. Kufika chuo kikuu mwanafunzi anahitaji mambo mawili tu: kuwa na fedha za kumudu masomo ya elimu ya juu na angalau alama za kumpa sifa za kudahiliwa, shukran kwa kasi ya ongezeko la vyuo vikuu nchini.

Uchambuzi wa takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) uliofanywa na Nukta umebaini kuwa idadi ya taasisi za elimu ya juu nchini imepaa kwa kasi ya asilimia 51 ndani ya miaka 10 iliyopita.

Takwimu hizo zilizochapishwa katika kitabu cha takwimu muhimu za mwaka 2016 (Tanzania in Figures 2016) ambazo hutolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaonyesha kuwa idadi ya vyuo na vyuo vikuu imeongezeka kutoka 33 mwaka 2007 hadi 50 mwaka 2016 huku takriban robo tatu (asilimia 72) vikimilikiwa na taasisi binafsi.

Ongezeko la vyuo binafsi lilirekodiwa zaidi kati ya mwaka 2012 hadi mwaka 2016 baada ya idadi ya taasisi hizo kuwa takriban mara mbili ya vyuo vya umma hivyo kutoa wigo zaidi kwa Watanzania kupata fursa ya kupata elimu hiyo ya juu.

Katika mwaka wa masomo wa 2015/16 vyuo na vyuo vikuu nchini vilidahili wanafunzi 189,857 kwa mujibu wa TCU kutoka wanafunzi 135,367 katika mwaka wa masomo wa 2011/12.

Licha ya kuwepo taasisi nyingi za elimu ya juu zinazomilikiwa na watu binafsi na taasisi za dini, bado vyuo na vyuo vikuu vinadahili asilimia 61.4 ya wanafunzi wote wa mwaka 2015/16. Hii ina maana kuwa licha ya kuwa katika kila vyuo vinne nchini vitatu ni binafsi bado wanafunzi sita kwa kila 10 waliodahiliwa mwaka huo walitoka taasisi za elimu ya juu za umma.

Pamoja na kasi ya kuongezeka kwa taasisi hizo, bado kumekuwa na maswali juu ya ubora wa elimu inayotolewa na vyuo hivyo vinavyochipukia kama uyoga.

Katika mwaka wa masomo wa 2017/2018 vyuo 19 vilifungiwa udahili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Pia katika mwaka huo kozi 75 zilizuiwa kufundishwa katika baadhi ya vyuo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kukidhi viwango vinavyotakiwa katika ufundishaji.

Dar es Salaam iliongoza kwa kuwa na vyuo vingi vilivyofungiwa kudahili baadhi ya kozi mwaka jana kwa kuwa na vyuo vitano ambavyo ni United African University of Tanzania, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) na, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) kampasi ya Dar es Salaam.

Vingine ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Johns cha Tanzania (SJUIT) kituo cha Marks na Chuo Kikuu cha Uhandisi na Teknolojia cha Mtakatifu Joseph.

Moja ya chuo kilichofungiwa udahili |Picha ya mtandao

          Moja ya chuo kilichofungiwa katika udahili wa masomo kwa mwaka wa kwanza mwaka wa masomo 2017/2018.Picha| Mtandao.

Wadau wa elimu ya juu wanaelea kuwa kasi ya kuongezeka kwa vyuo nchini inabidi iendane na ubora wa elimu wanayotoa ili kuzalisha wasomi watakaoweza kutatua matatizo yanayolikumba taifa.

“Chuo lazima kiwe vizuri kimazingira, kiwe na walimu wa kutosha wenye ujuzi, na sehemu za kufanyia mazoezi kwa vitendo. Mfano, chuo cha udaktari lazima kiwe na hospitali ya kufanyia majaribio,” anasema Egidius Kamanyi, Mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kamanyi anasema kuwa hata vyuo ambavyo havijafungiwa lazima vijitathimini kama vinatoa elimu inayostahili na kama kuna maktaba za kutosha zenye vitabu zitakazo mfanya mwanafunzi asome zaidi.

Ili kufikia lengo hilo la kuboresha viwango vya elimu, vyuo vinashauriwa kuimarisha mifumo yao ya ndani ya udhibiti kuhakikisha wanafunzi wametoka na ujuzi unaotakiwa.

Mhitimu wa UDSM, Dadley Bahemu anasema unahitajika utashi wa kweli kwa wadau wakuu wa elimu ya juu kwa kuthibiti mifumo ya ndani hususani katika ufundishaji.

“Mfano hata vikifungiwa vyuo vingi vikabaki vitano kama hakutakuwa na uwiano kati ya alama za darasani na maarifa kichwani, bado kama Taifa tutakuwa na tatizo la kuwa na wasomi ambao hawawezi kutusaidia nchi yetu kusonga mbele,” anasema Dadley.

Hata hivyo, baadhi ya wadau bado wanatupia lawama kwa mfumo wa elimu ambao hauwajengi wanafunzi kuwa mahiri katika fani zao.

“Tunaamini watu wanafika chuo kikuu hawapati kazi, hawawezi hata kufanya assignment (mazoezi), kuna tatizo ndani ya elimu yetu kwa kweli tunahitaji mjadala wa kitaifa kuhusu elimu yetu,” anasema Mwanaharakati wa masuala ya elimu na mwalimu, Richard Mabala.

Wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu mkoani Iringa, Shirikisho la Wafanyakazi nchini (Tucta) liliitaka Serikali ifanye utafiti kubaini kozi zenye tija sokoni ikiwemo za ujasiriamali.

Katibu Mkuu wa Tucta Yahya Msigwa alisema kitendo cha vyuo vya kati kugeuzwa vyuo vikuu ni “janga la Taifa” kwa kuwa nchi haiwezi kujengwa na wenye shahada pekee bila kuwa na kada za elimu ya kati.

Wadau wanaeleza kuwa ubora wa elimu inayotolewa vyuoni ukiongezeka utasaidia wahitimu kuweza kukabiliana na mazingira ya sasa kwa ama kuajiriwa au kujiajiri.