Wizara sita zitakazotumia fedha nyingi bajeti 2020-21
Wizara hizo ni pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
- Wizara hizo ni pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
- Wizara hizo zimetengewa zaidi ya Sh1 trilioni kila moja.
- Wizara ya fedha ndiyo imepata fedha nyingi zaidi asilimia 35.5 ya bajeti yote.
Dar es Salaam. Wakati macho na masikio ya Watanzania yakisubiri bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2020/21 itakayowasilishwa Alhamis wiki hii, wizara sita ikiwemo ya fedha na mipango ndiyo zitakazotumia kiwango kikubwa cha fedha katika bajeti hiyo.
Bajeti hiyo ambayo ni ya mwisho kwa kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya Rais John Magufuli inatarajiwa kuwa Sh34.88 trilioni ikiwa imepanda kutoka Sh33.1 trilioni ya mwaka huu wa 2019/20 unaoisha Juni 30.
Uchambuzi wa bajeti uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) umebaini wizara sita; Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Nyingine ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Nishati ndiyo zimeidhinishiwa kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti ya mwaka 2020/21 kuliko nyingine zote.
Fedha zilizoidhinishwa kwa wizara hizo ni zaidi ya Sh1 trilioni kwa kila moja. Jumla ya fedha zitakazotumika katika wizara hizo ni zaidi ya nusu ya bajeti yote.
- Wizara ya Fedha na Mipango
Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo imepangiwa kiasi kikubwa kuliko wizara zote ambapo itatumia Sh12.4 trilioni sawa na asilimia 35.5 ya bajeti yote.
Licha ya wizara hiyo kupangiwa kiwango kikubwa cha fedha, Sh10.48 trilioni ya fedha zote ni kwa ajili ya kulipa deni la Serikali na kiasi kilichobaki kitaelekezwa katika matumizi mengineyo, mishahara na maendeleo.
Hiyo ni sawa na kusema asilimia 84.5 ya bajeti yote ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa 2020/21 itaelekezwa kulipa deni la Serikali.
Waziri wa fedha na mipango, Dk Philip Mpango amesema kwa mwaka 2020/21 wizara itaandaa na kutekeleza mikakati itakayowezesha Serikali kukopa katika soko la fedha la ndani na nje bila kuathiri uhimilivu wa deni la Serikali, Sheria ya mikopo, dhamana na misaada Sura 134 na vigezo vya viashiria hatarishi vya madeni yaliyotokana na dhamana za Serikali.
2. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
Wizara ya pili itakayotumia kiasi kikubwa cha fedha ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo itatumia Sh7.1 trilioni. Kati ya fedha zinazoombwa, Sh4.7 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara na matumizi mengineyo.
Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo aliliambia Bunge hivi karibuni kuwa baadhi ya mipango itakayotekeleza na wizara yake mwaka 2020/21 ni pamoja na kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa huduma za afya ya msingi, lishe na ustawi wa jamii katika mamlaka za serikali za mitaa.
“Tutaratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa elimu ya msingi na sekondari katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ikijumuisha utekelezaji wa mpango wa utoaji wa elimumsingi bila ada,” amesema Jafo wakati akiwasilisha bungeni bajeti hiyo.
3. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nayo imebahatika kuingia katika orodha ya wizara zilizopata fedha nyingi baada ya kuidhinishiwa na Bunge Sh4.7 trilioni.
Kati ya fedha hizo, Sh1.6 trilioni ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi, mawasiliano (Sh15.6 bilioni) huku uchukuzi ikipata Sh3.15 trilioni sawa na theluthi mbili au asilimia 66 ya bajeti yote ya wizara hiyo.
Fedha hizo za uchukuzi zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya usafiri wa majini na nchi kavu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa meli zinazotumiwa katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa ili kuwarahishia wananchi usafiri.
Waziri wa wizara hiyo Mhandisi Isack Kamwelwe amesema pia mwaka 2020/21 wanakusudia kulipa malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mbili mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na kulipa malipo ya awali ya ununuzi wa ndege moja ya mizigo (freighter) aina ya Boeing 767-300.
Ndege hiyo ya mizigo itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani katika bidhaa za Tanzania ikiwemo maua, samaki na bidhaa zitokanazo na samaki, nyama, korosho, matunda na mboga mboga.
Zinazohusiana:
- Dk Mpango: Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 4 mwaka 2020
- Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019-20
- Matarajio ya wadau bajeti kuu ya Serikali Tanzania 2020-21
4. Wizara ya Nishati
Namba nne imeenda kwa Wizara ya Nishati ambayo ina jukumu kubwa la kuwaangazia wananchi kwa nishati ya umeme unaotumika nyumbani na maeneo ya uzalishaji.
Waziri wa wizara hiyo Dk Medard Kalemani aliyewasilisha bajeti katika mwaka 2020/21 Mei 8, amesema Wizara ya Nishati inakadiria kutumia Sh2.19 trilioni ikilinganishwa na Sh2.14 trilioni iliyotengwa 2019/20, sawa na ongezeko la asilimia 2.5.
Kati ya fedha hizo za mwaka ujao, Sh2.16 trilioni sawa na asilimia 98.7ya bajeti yote ya wizara zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kiasi kilichobaki ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara ya watumishi na matumizi mengineyo.
5. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeshika nafasi ya tano kwa kupata kitita kikubwa baada ya kuidhinishiwa bajeti ya Sh2.14 trilioni katika mwaka wa fedha 2020/21 ikiongezeka kutoka Sh1.85 trilioni iliyopitishwa mwaka 2019/20 huku Serikali ikitakiwa kutoa fedha kwa wakati ili kufanikisha mipango ya wizara hiyo.
Kati ya fedha hizo, Sh1.9 trilioni sawa na asilimia 92.4 ya bajeti yote zitaelekezwa katika matumizi ya kawaida huku kiasi kilichobaki kitatumika kutekeleza shughuli za maendeleo za wizara hiyo nyeti nchini Tanzania.
Bajeti hiyo ya mwaka ujao ndiyo bajeti ya kiwango cha juu kabisa kwa wizara hiyo ndani ya miaka minne iliyopita.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika mapendekezo yake kuhusu bajeti hiyo imeishauri Serikali kutoa fedha zilizoidhinishwa kwa wakati kwa wizara hiyo ili shughuli zilizopangwa zifanyike kwa wakati.
Rais John Magufuli akiongoza moja ya kikao cha Baraza la Mawaziri. Picha|Mtandao.
6. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
Orodha ya wizara sita zilizoidhinishiwa fedha nyingi zinazozidi Sh1 trilioni imefungwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo imepanga kutumia Sh1.4 trilioni katika mwaka ujao.
Kati ya fedha hizo, Sh857.5 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo Sh606.7 bilioni ni fedha za ndani na Sh250.7 bilioni ni fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Wakati wizara hizo sita zikipangiwa kiasi kikubwa cha fedha, Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ndiyo itatumia kiasi kidogo cha pesa baada ya kuidhinishiwa Sh27.9 bilioni.