Yaliyojificha utekelezaji wa bajeti Wizara ya Nishati 2019-2020
Huenda baadhi ya miradi ya maendeo iliyopangwa kutekelezwa na Wizara ya Nishati katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 isikamilike kwa wakati baada ya Serikali kuchelewa kutoa fedha zilizoidhinishwa mwaka huo.
- Hadi Aprili 30 mwaka huu wizara hiyo imepokea asilimia 28.5 ya fedha zote za 2019/2020.
- Waziri Kalemani asema kiasi hicho kilichopokelewa na wizara hadi Aprili kinaendana na mpango kazi uliopo sasa.
- Wizara hiyo kutumia Sh2.19 trilioni mwaka 2020/2021.
Dar es Salaam. Huenda baadhi ya miradi ya maendeo iliyopangwa kutekelezwa na Wizara ya Nishati katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 isikamilike kwa wakati baada ya Serikali kuchelewa kutoa fedha zilizoidhinishwa mwaka huo.
Katika mwaka 2019/2020 wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge bajeti ya Sh2.14 trilioni, kati ya fedha hizo, miradi ya maendeleo ilitengewa Sh2.11 trilioni sawa na asilimia 98.8 ya yote ya wizara na kiasi kilichobaki kilielekezwa katika matumizi ya kawaida.
Hata hivyo, hadi Aprili 30, 2020, wizara hiyo ilikuwa imepokea jumla ya Sh611.14 bilioni sawa asilimia 28.5 ya fedha zote ilizotengewa mwaka 2019/2020 ambao unaisha Juni 30.
Hiyo ni sawa kusema wizara hiyo imepokea zaidi ya robo ya bajeti yote ya mwaka huu. Huenda mipango ya wizara hiyo iliyopangwa kutekelezwa mwaka huu isikamilike kwa wakati kutokana na mwenendo huo wa utekelezaji bajeti.
Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani aliyekuwa akiwasilisha makadiri ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2020/2021 leo (Mei 8, 2020) bungeni jijini Dodoma amesema kiasi hicho kilichopokelewa na wizara hadi Aprili kinaendana na mpango kazi uliopo sasa.
“Serikali inaendelea kutoa fedha kulingana na mpango kazi na mahitaji yaliyopo,” amesema Dk Kalemani.
Soma zaidi:
- Bajeti ya Wizara ya Ulinzi yapaa kwa mara ya pili mfululizo.
- Bashungwa: Sijapewa fedha za maendeleo wizara ya viwanda, biashara 2019-2020
- Kamwelwe aomba matrilioni kugharamia ujenzi, uchukuzi Tanzania
Baadhi ya vipaumbele vya wizara hiyo muhimu kuwapatia wananchi nishati mwaka 2019/2020 ni pamoja kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo Julius Nyerere katika Mto Rufiji kwa megawati 2,115, Rusumo (megawati 80), Kinyerezi I – Extension (megawati 185), Malagarasi (megawati 45), Kakono (megawati 87) na Mtwara (megawati300).
Pia kujenga njia za kusafirisha umeme ikiwemo Singida – Arusha – Namanga wenye uwezo wa kilovoti 400, kuendelea na utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini.
Dk Kalemani amesema pia walipanga kuimarisha shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha kupitia utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja ili kuendesha shughuli za maendeleo.
Hata hivyo, amesema kwa mwaka 2020/21, wizara yake itaendelea kutekeleza maeneo ya vipaumbele mbalimbali yaliyoanishwa mwaka huu ikiwemo kushirikisha wawekezaji binafsi katika utekelezaji wa miradi ya umemejua wa megawati 150 na umeme wa upepo wa megawati 200.
Bajeti ya 2020/2021 yaongezeka kiduchu
Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Chato amesema katika mwaka 2020/21, Wizara ya Nishati inakadiria kutumia Sh2.19 trilioni ikilinganishwa na Sh2.14 trilioni iliyotengwa 2019/20, sawa na ongezeko la asilimia 2.5.
Kati ya fedha hizo za mwaka ujao, Sh2.16 trilioni sawa na asilimia 98.7 zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kiasi kilichobaki ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara ya watumishi na matumizi mengineyo.
Wizara hiyo ni miongoni mwa wizara ambazo zimetengenewa fedha nyingi zinazozidi trilioni moja zikiwemo za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.