October 6, 2024

Yatakayosaidia kuongeza ubunifu kwenye vyombo vya habari Tanzania

Wakati vyombo vya habari Tanzania vikichangamkia fursa ya teknolojia katika shughuli zao, vimetakiwa kuongeza ubunifu katika uzalishaji na usambazaji wa habari zenye kutatua changamoto za wananchi na Taifa.

  • Wadau wasema vyombo vya habari viweke katika kutengeneza habari zenye ubora wa hali ya juu.
  • Wanahabari watakiwa kubobea katika uandishi wa masuala.
  • Ubunifu unatakiwa kuanza na wanafunzi wanaosoma uandishi wa habari waliopo vyuoni. 

Dar es Salaam. Wakati vyombo vya habari Tanzania vikichangamkia fursa ya teknolojia katika shughuli zao, vimetakiwa kuongeza  ubunifu katika uzalishaji na usambazaji wa habari zenye kutatua changamoto za wananchi na Taifa. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa vyombo vya habari Tanzania (TMF), Fausta Musokwa aliyekuwa akizungumza leo (Machi 11, 2020) jijini Dar es Salaam katika mdahalo kuhusu kubuni suluhisho za kidijitali kukuza tasnia ya habari Tanzania, amesema vyombo habari vinatumia teknolojia lakini vinahitaji kwenda mbali zaidi.

“Tukibadilika kimtazamo tunaweza kutumia vizuri ubunifu kwenye vyombo vya habari,” amesema Musokwa ambaye alikuwa mzungumzaji mkuu katika mdahalo huo.

Amesema changamoto iliyopo sasa kwa wanahabari wengi ni jinsi ya kutengeneza maudhui yanayogusa moja kwa moja changamoto za jami (solution journalism) ili mchango wao uonekane kwa urahisi katika sekta mbalimbali za maendeleo.

“Wanapaswa kuongeza uwezo wa kutengeneza habari zenye ubora wa hali ya juu hasa kufanya habari za uchunguzi lakini hili linawezekana kama kuna mazingira rafiki ya kufanya hivyo,” amesema bosi huyo wa TMF. 

Ili ubunifu uongezeke kwenye vyombo vya habari, Musokwa amesema wadau wa habari wanatakiwa kuwa na mtazamo chanya wa kufikiri kwa kina kuhusu masuala mbalimbali ya jamii.

Mchakato huo utawasaidia kuwa na mawazo ya habari yatakayosaidia uzalishaji wa habari zenye ubora wa hali ya juu. 


Soma zaidi:


Hata hivyo, Musokwa amesema juhudi za kuongeza ubunifu zinawaweza kuwa endelevu ikiwa zitaanza vyuoni kwa wanafunzi wanaosomea uandishi wa habari kujengewa uwezo wa kuwa wabunifu.

“Ni kuanza na wanafunzi wanaosomea na taaluma ya habari wakiwa vyuoni, kuwajengea mtazamo wa kuwa wabunifu ili wakiingia katika tasnia ya habari waweze kutekeleza majukumu yao kwa viwango vya juu,” amesema.

Mdahalo huo ni sehemu ya Wiki ya Ubunifu (#IW2020) ambayo imeandaliwa na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ikiwemo Tume Ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Seedspace Dar es Salaam na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID).

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forums, Maxence Mello amesema wanahabari wanapaswa kutengeneza maudhui yanayokidhi mahitaji ya walaji na siyo wanayofikiri wao kuwa yanawafaa Watanzania. 

Amesema ubunifu unaweza kuongezeka kama vyombo vya habari vitatoa fursa kwa Wanahabari kubobea katika kuandika habari za sekta ili kuwa na uwanja mpana wa kutoa habari zenye maslahi mapana kwa wananchi.