July 8, 2024

Yatakayosaidia watahiniwa kutoboa mtihani kidato cha sita 2020

Wadau wa elimu wamependekeza baadhi ya mikakati itakayosaidia watahiniwa kidato cha sita mwaka 2020 kufanya vizuri ikiwemo kuwaandaa kisaikolojia na kuwahimiza kusoma kwa bidii.

  • Shule, walimu watakiwa kuwasaidia watahiwa kusoma kwa bidii kabla mitihani haijaanza Juni 29.
  • Baadhi ya wakuu wa shule wamesema wamekamilisha maandalizi ya mtihani huo. 
  • Necta yawataka wanafunzi kuzingatia ratiba iliyotolewa. 

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Serikali kutangaza tarehe ya kuanza kwa mitihani ya kidato cha sita 2020, wadau wa elimu wamependekeza baadhi ya mikakati itakayosaidia wanafunzi kufanya vizuri ikiwemo kuwaandaa kisaikolojia na kuwahimiza kusoma kwa bidii. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako Mei 22 alitangaza kuwa mitihani ya kidato cha sita itaanza rasmi tarehe 29 Juni 2020 na itafanyika hadi 16 Julai 2020.

Hiyo ina maana kuwa wanafunzi hao watakuwa na siku 28 tu za kujiandaa na mitihani hiyo baada ya Rais Magufuli kuwaruhusu wanafunzi wa kidato cha sita kurejea shuleni Juni mosi ili wajiandae na mitihani. 

Dk Magufuli lifikia uamuzi huo sambamba na kuwaruhusu vyuo vyote nchini vifunguliwe kutokana na maendeleo mazuri ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) ambao alisema umepungua kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.

Hata hivyo, wadau wa elimu wamesema kipindi cha kujiandaa kwa ajili ya mtihani hiyo ni kifupi lakini bado wanafunzi hao wana nafasi nzuri ya kufanya vizuri. 

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE) Dk Luka Mkonongwa ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kwa sasa shule zinatakiwa ziweke mikakati ya kuhakikisha wanawasaidia wanafunzi waliokaa nyumba kwa miezi miwili kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao. 

“Moja ya njia ni kuwatengenezea programu ya kusoma mpaka usiku…ule muda ambao wanafunzi wanaoutumia kusoma binafsi walimu wanaweza kuutumia kufundisha. Hili ni suala tu la kufidia ule muda wa miezi miwili uliopotea,” amesema Dk Mkonongwa. 

Dk Mkonongwa ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya elimu amesema walimu wanapaswa kuwafanyia maandalizi ya kisaikolojia wanafunzi watakaporudi shuleni Juni mosi ili watambue kuwa wana wajibu wa kujisomea zaidi kuliko kuwategemea walimu.


Zinazohusiana: 


Amesema wanafunzi watambue kuwa Corona ilikuwa dharura na sasa wana kibarua cha kukamilisha ndoto zao za kwenda chuo kikuu kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita.   

“Wakiweza kuandaliwa hivyo kisaikolojia wanaweza wakafanya vizuri tu bila shida,” amesema mhadhiri huyo. 

Pia amebainisha kuwa anaamini Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) katika utungaji wa mtihani wa kidato cha sita limezingatia dharura iliyojitokeza ya Corona na maswali mengi yatakuwa yale ambayo wanafunzi wamekamilisha mada za darasani. 

Mtihani wa kidato cha sita ndiyo ngazi ya mwisho kwa wanafunzi wa sekondari kujiandaa na elimu ya juu ili kwenda kubobea katika taaluma zao zinazohitajika kuhudumia jamii baada ya masomo. 

Walimu, wanafunzi walivyojipanga

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisimiri ya mkoani Arusha, Valentine Tarimo ameiambia Nukta kuwa walianza kujianda mapema kwa ajili ya mtihani huo na hawaoni kuwa siku zilizobaki kabla wanafunzi kufanya mtihani zitaathiri ratiba ya masomo.

“Wakati walipofunga hiyo miezi miwili tuliwapa kazi za kufanya chini ya programu maalum ya mtandaoni na matumaini yangu kwamba wataendelea na masomo kama kawaida na Corona haijaathiri masomo yao,” amesema Tarimo. 

Uboreshaji wa miundombinu katika shule ya sekondari Kisimiri wachangia kuongezeka kwa ufaulu.Picha| Valentine Tarimo.

Amesema shule yake ambayo tangu mwaka 2012 haijawahi kutoka 10 bora kitaifa kidato cha sita imejiandaa vema kuwapokea wanafunzi ili kumalizia masomo yaliyobaki wakiwa salama. 

“Tunaendelea kutekeleza maelekezo tuliyopewa na Wizara ya afya ikiwemo kuhakikisha wanafunzi wanavaa barakoa na vifaa vyote vya kunawia maji vinakuwepo shuleni ili kujizuia na maambukizi ya Corona,” amesema Tarimo.

Amesema ana imani kuwa mwaka huu wataendelea kutoa mchuano mkali kwa shule kongwe na binafsi na kuhakikisha hawatoki katika orodha ya dhahabu. 

Kisimiri iliyoshikilia nafasi ya kwanza kitaifa mwaka jana, itaendeleza umwamba wake mwaka huu? Hili tutaliangazia baada ya matokeo kutoka.

Mmoja wa waanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu kutoka Shule ya Sekondari Mbeya ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema alifikiri watakaa nyumbani muda mrefu lakini hana jinsi kukubaliana na uamuzi wa Serikali wa kurudi shule na kuhitimu. 

“Nimeanza kusoma sana maana muda uliobaki ni mchache na mambo bado ni mengi,” amesema mwanafunzi huyo huku akisema anaamini atatoboa katika mtihani huo. 

Tayari Necta imetoa ratiba ya mitihani ya kidato cha sita itakayoanza Juni 29, 2020 na kueleza kuwa watahiniwa wanatakiwa kujiandaa na kuzingatia ratiba kama inavyoelekezwa.

“Mitihani itaendelea kama ilivyopangwa hata kama itangukia siku ya sikukuu (Public Holiday),” imeeleza sehemu ya ratiba hiyo.