November 27, 2024

Zana za ushindi za kukuvusha mwaka 2021

Ni pamoja na kujijengea tabia ya uthubutu wa kufanya kitu bila kuogopa macho na maneno ya watu.

  • Ni pamoja na kujijengea tabia ya uthubutu wa kufanya kitu bila kuogopa macho na maneno ya watu.
  • Pia, kwa kufanya unachokipenda, itakupatia urahisi wa kufanya kazi zako.
  • Kwa waajiri, wanashauriwa kuwa karibu na wafanyakazi wao ili malengo ya kampuni yafikiwe.

Dar es Salaam. Katika pita pita zangu za mtandaoni, Nimekutana na nukuu ikisema “Siku 365 ni sawa na fursa 365”. Nilihitaji glasi ya maji ili kuelewa undani wa nukuu hii na baada ya halmashauri ya akili yangu kushauriana na akili za baadhi ya rafiki zangu maana yake ilipatikana.

Kwa ambaye bado upo njia panda, siku 365 ni sawa na mwaka mzima. Kwa miaka mirefu ukiwemo mwaka 2020, idadi ya siku huongezeka na kuwa 366. 

Hivyo nukuu hiyo maana yake ni sawa na kusema mwaka 2021 unakuja na fursa 365 ukiwa na fursa mpya kila siku.

Ikiwa zimebaki siku nne tu kuumaliza mwaka 2020, unahitaji nini ili kufanya mabadiliko yako katika nyanja za kijamii, kuichumi, kiafya na nyinginezo? Jaribu dondoo hizi: 

Jenga tabia ya uthubutu

Baadhi ya watu huingiwa na uoga pale wanapotaka kuanzisha jambo fulani. Baadhi huogopa kupata hasara ya uwekezaji na wengine huogopa maneno ya watu yakiwemo “nitaonekanaje na majirani zangu kuwa nauza mihogo?” 

Kukutia moyo, wakati unaogopa majirani, rafiki na ndugu watakuonaje kwa kuanzisha biashaa ndogo, majirani zako wana vipato vyao na huenda usiku wanapata usingizi wakiwa wana amani kiuchumi wakati wewe unakosa usingizi kwa mawazo ya kukosa fedha.

Niliwahi kuambiwa na mtu wangu wa karibu kuwa, utajiri mwingi umejaa makaburini kwani ni sehemu ambapo watu waliokuwa na mawazo makubwa ya kubadili ulimwengu wamezikwa. 

Kwa mwaka 2021, jitahidi kuwa na malengo madhubuti ambayo yanaweza kufanyika. Picha| freepik.com.

Fanya kitu unachokipenda

Mbunifu na mtaalam wa grafiki, Karim Salkim amesema kupitia kufanya kitu unachokipenda, mtu unaweza kuwa na furaha na kazi yako na hata pale unapoyumba, inaweza kuwa rahisi kuinuka.

Mkazi huyo wa Dar es Salaam ameiambia Nukta kuwa, kwa mwaka 2021, ni vyema watu wakajitahidi kufanya vitu ambavyo wana hamasa navyo na watafute namna ya kutengeneza fedha kupitia njia hiyo.

“Jitahidi kuwa na furaha wakati unafanya hivyo,” amesema Salkim.

Jenga mahusiano chanya kazini

Mkurugenzi wa kampuni ya kuzalisha unga wa mahindi na chakula cha mifugo cha Lina Mills, Christian Phillip amesema kwa waajiri ni muda wa kujenga mahusiano mazuri na waajiriwa wao. 

Ushauri wa Phillip ni kuwa, wafanyakazi wako wakiwa na furaha hata kazi zako zitafanyika vizuri na watafanya kazi bila kinyongo.

“Waongezee mshahara kama unaweza, wapatie vijibonasi na posho za hapa na pale. Wakiwa hawana mawazo, kazi zako zitaenda vizuri,” amesema Phillip ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam.


Soma zaidi:


Weka mipango yako, fanya kazi kwa bidii

Mjasiriamali wa manukato, nguo na pochi za wanawake mwenye ofisi yake maeneo ya Makumbusho jijini Dar es Salaam, Loyce Msolwa amesema kuanza mwaka bila mipango ni sawa na kutembea gizani.

Wakati mwaka unaanza, ni vyema kuweka mipango inayowezekana kufanyika na kuweka muda utakaoweza kutimiza mipango yako.

Kwa Msolwa, jambo lingine ni kumtanguliza Mungu na kutokukata tamaa.

Jitathmini uwezo wako 

Mkurugenzi wa Rospa Media Steven Genya amesema kwa mwaka ujao ni vyema mtu kutathmini uwezo wake na kipaji chake na kuvihusisha na fursa zilizopo.

Kwa Genya imani kwa Mungu pia ni muhimu sana kwani “bila yeye hakuna linalowezekana”. hivyo ni kusema, kwa kufahamu uwezo wako pamoja na madhaifu yako, itakuwa rahisi kujijenga na kuwa bora zaidi kuliko mwaka uliopita.

Je, umejipangaje kufikia malengo yako ya mwaka 2021?