November 24, 2024

Zanzibar ilivyojipanga kukabiliana na wimbi la tatu la Corona

Imesema inaimarisha kinga na kuweka rasilimali watu katika kila hospitali kwa lengo la kujiandaa iwapo mlipuko wa ugonjwa wa Corona wimbi la tatu litakapojitokeza.

  • Inaimarisha kinga na kuweka rasilimali katika kila hospitali.
  • Pia wizara itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa
  • Hatua hiyo imekuja  baada ya kuongezeka kwa maambukizi hayo katika nchi za jirani ikiwemo Uganda, Afrika Kusini na Congo DRC.

Mwanza. Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ya Zanzibar imesema inaimarisha kinga na kuweka rasilimali watu katika kila hospitali kwa lengo la kujiandaa iwapo mlipuko wa ugonjwa wa Corona wimbi la tatu litakapojitokeza.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Tanzania Bara kuwatahadharisha wananchi wake juu ya ujio wa wimbi hilo na kuwataka kuchukua tahadhari zote zinazopendekezwa na wataalam wa afya ikiwemo kuvaa barakoa. 

Waziri wa wizara hiyo, Nassoro Ahmed Mazrui aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 22, 2021 amesema hatua hiyo imekuja  baada ya kuongezeka kwa maambukizi hayo katika nchi za jirani ikiwemo Uganda, Afrika Kusini na Congo DRC.

Amesema nchi hizo zimekiwa na mwingiliano mkubwa wa shughuli za kijamii na kiuchumi na watu Zanzibar. 

“Wizara imo katika taratibu za kuweka miundombinu na rasilimali watu katika kila hospitali kwa lengo la kujiandaa iwapo mlipuko wa ugonjwa huu utajitokeza,” amesema Mazrui. 

Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya wimbi la tatu la Corona ambalo limeanza kuingia Tanzania. Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui ameeleza hayo mbele ya waandishi wa habari leo ofisini kwake Mnazi Mmoja Zanzibar. Picha| Salma Said.

Aidha, waziri huyo ambaye ni Mbunge wa kuteuliwa kutoka chama cha ACT-Wazalendo amesema kwa sasa wanahakikisha wageni wote wanaoingia Zanzibar wanakuwa na vyeti vya uthibitisho wa kutokua na maambukizi

“Wizara inahakikisha kua wageni wote wanaoingia nchini ambao wanatoka katika nchi hatarishi zaidi wanafanyiwa kipimo cha haraka,” amesema Mazrui huku akizitaja nchi hizo  kuwa ni India, Afrika Kusini, Uganda na Congo DRC.

Nchi nyingine ni Uingereza, Marekani, Peru, Phillipines na Brazil ambazo zimegundulikana kuwa na aina mpya ya virusi vya Corona.

Pia wizara itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuvaa barakoa, na kukaa umbali wa mita moja.

 Lakini pia kuweka matayarisho katika ngazi ya hospitali zote za za visiwa vya Unguja na Pemba.

“Sehemu hizi ni kwa ajili ya kuwatibu na kuwahifadhi watu watakaosadikiwa kuwa na ugonjwa katika hospitali za serikali na binafsi pamoja na kupima watu wote wenye dalili za ugonjwa wa Corona kwa kutumia kipimo cha haraka,” amesema Waziri huyo.

Tanzania iliacha kutoa takwimu za Corona kwa umma tangu Mei mwaka jana ambapo ilikuwa imerekodi visa 509 na vifo vya watu 21 kutokana na ugonjwa huo.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi mwaka huu ameaihidi kushirikiana na wadau duniani kupambana na ugonjwa huo ikiwemo kuruhusu chanjo kuanza kutumiwa na wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini.