November 24, 2024

Zanzibar yafikisha wagonjwa 24 wa Corona

Idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) Zanzibar imezidi kuongezeka na kufikia 24 baada ya Wizara ya Afya visiwani humo kutangaza wagonjwa wapya sita.

  • Serikali imetangaza wagonjwa wapya sita leo na kufikisha idadi ya wagonjwa 24 visiwani humo. 
  • Wagonjwa hao wapya, watano ni wanaume na mmoja ni mwanamke.

Dar es Salaam. Idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) Zanzibar  imezidi kuongezeka na kufikia 24 baada ya Wizara ya Afya visiwani humo kutangaza wagonjwa wapya sita.

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed katika taarifa yake iliyotolewa leo (Aprili 16, 2020) amesema wagonjwa wote ni Watanzania na hawana historia ya kusafiri nje ya nchi siku za hivi karibuni. 

“Wagonjwa wote wamelazwa katika vituo maalum kwa ajili ya kuendelea na matibabu,” amesema Mohammed. 

Idadi ya wagonjwa hao wapya inafanya Zanzibar kushika nafasi ya pili kwa wagonjwa wengi wa COVID-19 baada ya Dar es Salaam ambayo hadi kufikia jana (Aprili 15,2020) ilikuwa na wagonjwa 62 katika ya 88 walioripotiwa.

Akizungumzia wagonjwa hao wapya, Mohammed amesema wagonjwa watano ni wanaume na mmoja ni mwanamke ambao wote ni wakazi wa Zanzibar.

Mgonjwa wa kwanza ni mwanaume mwenye miaka 30 mkazi wa Kibweni, wa pili mwanaume (27) mkazi wa Magogoni huku watatu pia ni mwanaume mwenye miaka 28 anaishi Kwarara. 


Zinazohusiana:


Wengine ni mwanamke (58) anayeishi Kilamahewa Juu, wa tano ni mwanaume (23) mkazi wa Amani na mwisho ana miaka 55 ambaye ni mwanaume anayeishi Kidoti visiwani humo. 

Aidha, waziri huyo amewataka wananchi wanaofiwa na ndugu zao kuchukua tahadhari za afya hasa wanapowazika maiti na ikiwezekana washirikiane na wataalam wa afya. 

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa pua, mdomo au macho, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya.

Pia wanakumbushwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima hasa katika masoko na vituo vya daladala na watu wenye dalili za ugonjwa huo wametakiwa kufika katika vituo vya afya ili wafanyiwe uchunguzi.