Zawadi unazoweza kuwanunulia wazazi msimu wa sikukuu
Wanunulie vitu vitavyowasaidia kupunguza changamoto za maisha.
- Wapatie wazazi wako muda wa kukaa na kuongea mambo mawili matatu na wewe.
- Wanunulie vitu vitavyowasaidia kupunguza changamoto za maisha.
Dar es Salaam. Kwako mtafutaji. Huenda shughuli za kutafuta uhuru wa kiuchumi zimekupeleka mbali na wazazi wako kiasi cha kutokuwaona kwa muda mrefu.
Katika msimu huu wa sikukuu, huenda umepanga kuwafurahisha kwa zawadi zinazoweza kujenga tabasamu kubwa usoni mwao, basi una mengi ya kufanya.
Endapo haujalifikiria hilo, huenda ukaanza kujichanga ili walau umpatie zawadi mzazi na hata mlezi wako kwa ajili ya msimu huu wa sikukuu. Wapatie zawadi hizi:
Mpatie simu mpya
Fikiria hili, unampa mzazi wako boksi limefungwa vizuri kwa ustadi kabisa na anapofungua, anakutana na simu nzuri ambayo huenda umewahi kumsikia akiiongelea. Tabasamu atakalokuwa nalo, linatosha kabisa kuyayusha matatizo moyo wako.
Unaweza kupata muda wa kumdadisi ni simu gani angependa kuwa nayo na kisha ukamnunulia mzazi wako simu hiyo.
Simu hiyo itamrahisishia mawasiliano na hata kuendana na teknolojia mpya. Picha| freepik.com
Watembelee na tumia muda mwingi nao
Siyo lazima uwe vizuri kiuchumi ili uwatembelee wazazi wako. Unachohitaji ni nauli ya kwenda nyumbani na kurudi. Ni kweli mkono mtupu haulambwi lakini muda wako na kuwakumbuka wazazi wako ni jambo ambalo litawapatia faraja kuliko kitu chochote.
Wapo watu ambao kwa mwaka mzima wamekuwa wakiwaona wazazi wao katika picha tu, katika msimu huu wa sikukuu, ndiyo nafasi wanayoweza kuwa nayo ya kukutana na wazazi wao.
Soma zaidi:
- Hii ndiyo zawadi unayoweza kumpatia mama yako
- Zawadi za kielektroniki unazoweza kumpatia umpendae msimu wa sikukuu
- Zawadi zinazowafaa wanawake sikukuu ya wapendanao
Wapangie safari ya pamoja
Endapo hali yako ya kiuchumi ni nzuri, unaweza kuwapangia wazazi wako safari ya kutembelea sehemu mbalimbali zikiwemo fukwe na mbuga za wanyama na kisha kuwapangia chumba cha hoteli walau kwa siku moja au mbili watakapopumzika.
Mpango huu upo kichwani mwa Evans William mkazi wa jiji la Dar es Salaam ambaye amesema hawezi kuwanunulia vitu kwani ana uhakika kuwa wanaweza kuvinunua wenyewe.
Mpango wake ni kuwatoa ‘out’ na kuwapeleka sehemu nzuri ambayo itawafanya wajione wako tofauti na ulimwengu wanaoishi.
Katika kukusanya maoni ya habari hii, nilikutana na baadhi ya watu ambao wameondokewa na wazazi wao. Iliniumiza moyo kuwauliza swali hili kwani nilijihisi kuwatonesha vidonda.
Kati yao ni mkazi wa jijini Dar es Salaam, David Macha ambaye amewapoteza wazazi wake wote wawili miaka mine iliyopita.
Macha amesema, zawadi ambayo hadi leo anawapatia wazazi wake waliotagulia mbele ya haki ni kuwapenda wadogo zake na kuwatunza kama ambavyo wao wangewatunza.
“Sipendi kuwaona wadogo zangu katika huzuni, wakikosa kitu ndiyo maana napigana ili wapate mahitaji yote muhimu kama ambavyo wazazi wangu wangefanya. Ni zawadi pekee inayoweza kuwapatia tabasamu kokote waliko,” ameeleza Macha.
Wazazi wakiwa hai ni furaha kwa familia na watoto pia. Wafurahishe wazazi wako kwa zawadi. Picha| iStock.
Wanunulie vitu vya kudumu
Kama uchumi wako uko vizuri ni wakati sahihi kuwanunulia wazazi wako zawadi za kudumu ambazo zintawasaidia kutatua changamoto za maisha. Kama makazi yao ni duni, basi wajengee nyumba nzuri ili waishi sehemu nzuri.
Pia unaweza kuwafungulia miradi ya kiuchumi itakayowasaidia kuwaingizia kipato cha kujikimu ili kupunguza mzigo wa utegemezi kwako. Vitu hivi na vingine, vitaonyesha jinsi unavyowajali na kuwathamini wazazi wako.