October 6, 2024

Ziara ya Magufuli Mtwara yaondoka na kigogo wa Takukuru

Ni Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mtwara ang’olewa na Rais baada ya kushindwa kuhudhuria mkutano ili kujibu malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Chigugu katika wilaya ya Masasi.

  • Ni Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mtwara ang’olewa na Rais baada ya kushindwa kuhudhuria mkutano.
  • Amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo kuteua kamanda mwingine leo.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemfukuza kazi Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mtwara, baada ya kushindwa kuhudhuria mkutano wa kiongozi huyo wa juu nchini uliofanyika leo katika wilaya ya Masasi. 

Rais Magufuli amefanya uamuzi huo leo (Oktoba 16, 2019)  baada ya kumuita kamanda huyo kwenye mkutano katika kijiji cha Chigugu, Wilayani Masasi na kuelezwa kuwa hayupo.

Kutokuwepo kwa kamanda huyo kwenye msafara wa Rais, kulisababisha kukosekana mtu wa kujibu hoja za wananchi kuhusu madai yao ya fedha wanazowadai viongozi wa chama cha msingi cha Amcos ambao wanadaiwa wametoweka na fedha hizo. 

“Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mtwara yuko wapi? Hatuna Kamanda Takukuru Mtwara? Kama hayupo aondoke moja kwa moja nilete mtu mwingine hapa,” ameuliza Rais huku akishangiliwa na wananchi aliokuwa anawahutubia na kuongeza kuwa,

“Kuanzia leo siyo kamanda wa Takukuru mkoa huu. Mwambie mtu wa Takukuru alete mtu mwingine hapa, akatufutiwe kazi nyingine. Hatuwezi tukakaa tunabembelezana, ushenzi wa namna hii watu wanapata shida,” amesisitiza Rais.

Amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo kuteua kamanda mwingine leo na anatakiwa alipoti kesho, huku akisema anaweza kuwa hafai kuwa Rais  au mwanasiasa na katika kipindi chake hataruhusu kubembelezana katika majukumu ya kuwatumikia wananchi.


Zinazohusiana:   


Rais Magufuli yuko mkoani Mtwara katika ziara ya kukagua shughuli za maendeleo akitokea mkoani Lindi huku akiendelea kuwabana vigogo katika utekelezaji wa maendeleo katika maeneo yao. 

Akiwa Nachingwea mkoani Lindi leo amewabana mkuu wa wilaya hiyo, Rukia Muwango na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bakari Bakari baada ya wananchi kulalamikia ucheleweshwaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo soko na miundombinu ya maji. 

“Nawashukuru ndugu zangu wa Nachingwea kwa kuwa wakweli, ukweli humweka mtu huru, Sh71 milioni zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa soko lakini mambo yanasuasua. Hayo mengine niachieni mimi nitafanya maamuzi.

“Tunahitaji watendaji wakali, huyu mkurugenzi wenu ameniuzi sana, anasema alikua anafanya kazi Marekani, sijui alikua anaokota makopo?” amehoji Rais.