November 24, 2024

Zifahamu mbuga za wanyama kubwa zaidi Afrika Mashariki

Kwa taarifa yako kati ya hifadhi hizo tano, nne zinatoka Tanzania zikiongozwa na hifadhi mpya ya Nyerere.

  • Kati ya mbuga hizo, nne zinapatikana Tanzania.
  • Nyerere iliyogawanywa kukoka Selous inashikilika bendera.
  • Tsavo ya nchini Kenya kuwakilisha nchi zingine Afrika Mashariki.

Dar es Salaam. Sekta ya utalii ni kati ya sekta muhimu zinazotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kwa mujibu wa Kitabu cha hali ya uchumi wa taifa mwaka 2018, sekta hiyo iliipatia Tanzania mapato ya Sh2.15 trilioni mwaka jana.  

Kwa sehemu kubwa, mapato ya utalii yanachangiwa na watalii wanaokuja kutembelea vivutio ikiwemo wanyama na mimea iliyopo katika hifadhi za Taifa. Lakini unazifahamu hifadhi tano kubwa zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwa taarifa yako kati ya hifadhi hizo tano, nne zinatoka Tanzania. Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni inayotoa huduma za utalii ya Safaris Africana, hifadhi hizi ndiyo kubwa zaidi katika jumuiya hiyo yenye nchi sita za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Sudan Kusini na Rwanda: 

5. Ngorongoro

Hifadhi hii iliyopo Kaskazini mwa Tanzania ina ukubwa wa kilometa za mraba 8,280 ikiitwa Edeni ya Afrika kutokana na mandhari nzuri ya wanyama na mimea. Ngorongoro inashika nafasi ya nane katika orodha ya maajabu asilia duniani huku kwa mwaka 2018 pekee ilitembelewa na watalii 679,454. 

Ngorongoro itakupatia fursa ya kutazama makumi ya pundamilia wakichunga majani huku simba walioshiba wakihesabu saa na kusubiri jua lizame. Ngorongoro itakusogeza karibu na fursa ya kutembelea makumbusho ya Olduvai Gorge ambapo utaona fuvu la anayedhaniwa kuwa ni binadamu wa kwanza.

4. Serengeti

Ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 zinaipa hifadhi hii nafasi ya nne Afrika Mashariki huku jina la paradiso ya Afrika likibaki kuifanya hifadhi hii kuwa kati ya maajabu saba ya asili ya Afrika na dunia .

Ikiwa Kaskazini mwa Tanzania, Serengeti imesheheni vivutio lukuki vikiwemo simbana fisi mwenye madoa bila kusahau ndgee na wanyama wengine wengi.

Upekee huo umeifanya hifahdi hiyo itembelewe na watalii 446,030 ikia ni kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018.  

Serengeti ni jina linalotokana na neno la kimasai “Siringiti” lenye maana ya uwazi usio na mwisho na utaifadi upekee wake endapo utatembelea mbuga hii kuanzia Mei hadi Oktoba kila mwaka kwa sababu miezi mingine inatawaliwa na msimu wa mvua.

Serengeti ni jina linalotokana na neno la kimasai “Siringiti” lenye maana ya uwazi usio na mwisho. Picha| Serengeti.

3. Ruaha

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), hifadhi hii ndiyo hifadhi ya kwanza kwa ukubwa nchini Tanzania ambapo ina ukubwa wa kilometa za mraba 20,226 huku kwa mwaka 2018 pekee ilijinyakulia watalii wapatao 27,600..

Ruaha itakupa nafasi ya kuwaona tembo wakiwa kazini wakichimba mashimo kutafuta maji wakati wa kiangazi. 

Kipindi kizuri wa kutembelea mbuga hii ni wakati wa kiangazi. Ni pepo ya duniani kwani ndipo utakaposhuhudia wanyama wengi zaidi kwa mkupuo kwani wengi hutafuta maji kwenye mto Ruaha na vyanzo vingine vya maji.

Hifadhi ya Ruaha baada ya kipindi cha mvua itakupatia muonekano mzuri wa majani na maua yasiyo kifani hasa maua aina ya daisy, cleome, swathes na ipomoeas.


Zinazohusiana


2. Tsavo

Kutoka kwenye ardhi yenye utajiri wa kiafrika, Tsavo imechukua asilimia 2.36 ya ardhi ya Kenya ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba  22,000.  

Hifadhi hii ni kubwa kuliko zote nchini Kenya ikipambwa na mto Galana na maporomoko ya Lugard. Ukitembelea Tsavo, utaona wanyama wengi wakiwemo vifaru weusi, tembo na simba wa kimasai.

Tsavo imegawanywa mara mbili na kutengeneza Tsavo ya Mashariki na Tsavo Magharibi huku ikiwa na  mageti nane ya kuingilia.

1. Nyerere

Ni hifadhi ya Taifa iliyotambulishwa nchini Tanzania hivi karibuni, baada ya kumegwa kutoka sehemu ya Pori la Akiba la Selous. Nyerere ina ukubwa wa kilometa mraba zaidi ya 30,000 na ukubwa huo unaifanya hifadhi hiyo kuwa kubwa kuliko zote Afrika Mashariki na barani Afrika.

Nyerere inayobaki kuwa na vivutio vya wanyamapori na uoto wa asilia usio na kifani, inapambwa zaidi na viboko wanaokaa katika maji ya mto Rufiji na faru. ​Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ina ukubwa wa kilometa mraba zaidi ya 30,000 na ukubwa huo unaifanya hifadhi hiyo kuwa kubwa kuliko zote Afrika Mashariki na barani Afrika. Picha| Tanapa.

Mbuga hii itakuacha ukifurahia mahusiano kati ya wanyama wanaowinda na wanaowindwa huku muonekano wake ukikupa kila sababu yakutafuta kamera yako ili upige picha za kumbukumbu.

Kutokana na kuwepo kwa mto Rufiji karibu na hifadhi hiyo, Serikali inatekeleza mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 maarufu kama Stieglers Gorge, licha ya kuwa baadhi ya wanaharakati wa mazingira kutofautiana na hatua hiyo ya Serikali wakidai utachangiua kuharibu mazingira ya eneo hilo. 

Habari hii imeboreshwa takwimu za mapato yaliyopatikana kutoka katika sekta ya utalii mwaka 2018.