October 6, 2024

Zifahamu tozo zinazotozwa kwenye hifadhi za Tanzania 2019-2020

Kutembelea vivutio vilivyopo katika hifadhi hizo ni njia mojawapo ya kuendeleza sekta ya utalii ili kuongeza pato la Taifa na utolewaji wa huduma za kijamii.

  • Ni tozo za viingilio zilizoanza kutumia Julai 1, 2019 na zitamaliza muda wake ifikapo Juni 30, 2020.
  • Watalii wa kigeni kulipa takribani mara mbili ya watalii wenyeji na wakazi wa Afrika Mashariki.
  • Watoto chini ya miaka mitano hawalipii chochote kuona vivutio vya hifadhi hizo.  

Dar es Salaam. Kutembelea hifadhi za Taifa zilizopo nchini Tanzania, inaweza kuwa sehemu sahihi kwa ajili ya mapumziko yako ya mwisho wa mwaka 2019. 

Kutembelea vivutio vilivyopo katika hifadhi hizo ni njia mojawapo ya kuendeleza sekta ya utalii ili kuongeza pato la Taifa na utolewaji wa huduma za kijamii. 

Wakati ukipanga bajeti yako utakayotumia katika hifadhi hizo, una kila sababu ya kufahamu tozo mbalimbali za viingilio katika hifadhi ili ujipange vizuri namna utakavyofanikisha safari yako. 

Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imetangaza tozo mbalimbali zinazotozwa kwenye hifadhi inazosimamia nchini kwa wageni wa ndani na nje ya nchi. 

Tozo hizo ni za kipindi cha mwaka mmoja na tayari zimeanza kufanya kazi tangu Julai 1,  2019 na mwisho wake utakuwa Juni 30, 2020.

Uchambuzi uliofanywa na www.nukta.co.tz wa tozo hizo umebaini kuwa zinawabeba zaidi wazwa kuliko wageni, jambo linawapa fursa zaidi ya kufaidika na rasilimali zao.

Tozo hizo ambazo zinamanisha tozo za wageni na wakazi, nyingi zinaonekana kuwa na utofauti wa takribani asilimia 50 kati ya ile ya mgeni na mkazi ambapo tozo ya mgeni ni mara mbili ya ile ya mkazi/ mtanzania.

Licha ya kuwa tozo hizo zinatofautiana kulingana na hifadhi husika, bado tozo kwa wageni ziko juu kidogo ya zile wanazopazwa kulipa wazawa. 

Leo tunakuletea tozo zinazotozwa katika baadhi ya Hifadhi za Taifa ambazo unaweza kuzitembelea kabla ya mwaka 2019 kuisha. 

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Hifadhi hiyo iliyopakana hifadhi ya Ngorongoro ina ukuwa wa kilometa za mraba 30,000,  ni kati ya vivutio vikuu nchini Tanzania.

Wanyama kama digidigi, swala na pundamilia, huipamba hifadhi hiyo kwa misimu tofauti tofauti ya mwaka huku baadhi yao wakikimbilia Ngorongoro kutafuta majani mwezi Januari.

Hata hivyo, uzuri huu ni bure kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano lakini kama una miaka zaidi ya hapo, inabidi pesa ikutoke.​

Kwa mgeni aliye juu ya miaka 15 itabidi agharamie Sh138,198  huku yule aliye na miaka chini ya 15 akitakiwa kugharamia Sh46,066 tu. 

Kwa Watanzania, wakazi wa nchi za Afrika Mashariki na wataalamu, pochi zao nabidi zitoe Sh69,099 kwa wote wenye miaka zaidi ya 15 na kwa wale wenye miaka mitano hadi 15 watatakiwa kulipa Sh23,033 kwa kila mtu.

Hifadhi ya Serengeti iliyopakana hifadhi ya Ngorongoro ina ukubwa wa kilometa za mraba 30,000,  ni kati ya vivutio vikuu nchini Tanzania. picha| Mtandao.

Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro

Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa hekari 75,575 inavutia watalii siyo tu kwa wanyama bali kwa mlima mrefu zaidi barani Afrika.

Ili upate kuingia kwenye hifadhi hiyo yenye Mlima Kilimanjaro wenye urefu wa mita 5,895, kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni bure huku wageni wenye miaka mitano hadi 15 wakilipia Sh46,066 na waliozidi miaka 15 wakitakiwa kulipa Sh161,231.

Kwa Watanzania, wakazi wa nchi za Afrika Mashariki na wataalamu, wanatakiwa Sh80,615 na kwa mtalii mzawa mwenye miaka mitano hadi 15 atagharamia Sh23,033.

Hifadhi za Taifa za  Arusha, Tarangire na Ziwa Manyara

Hifadhi hizi zinatozo gharama zinazofanana. Wakati Manyara ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 330, Tarangire imechukua kilometa za mraba 2,600 kwenye ardhi ya Tanzania  na hifadhi ya Taifa ya Arusha ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 137

Hifadhi hizi zinakupatia muda wa kustaajabu wanyama kama tembo, tumbili, sokwe na twiga.

Ikiwa ni bure kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano, Sh103,648 itamtoka mgeni mwenye umri zaidi ya miaka 15 huku yule mwenye umri wa miaka mitano hadi 15 akitozwa Sh34,549.

Kwa wazawa na wakazi wa Afrika Mashariki, Sh51,824 itahitajika kutoka kwa mtalii mwenye miaka 16 na zaidi huku Sh17,274 ikimtoka kijana mwenye miaka mitano hadi 15.


Zinazohusiana


Kitulo inayofahamika kwa maua yake adimu na hifadhi zingine zote tajwa zina upekee wa aina yake. KUanzia sokwe wa Saadani hadi mto na mibuyu ya Ruaha ni sehemu tu ya uzuri wa Tanzania.

Kutembelea hifadhi hizi ni rahisi kwani ndizo zenye gharama nafuu ikilinganishwa na zingine. Kwa watalii wa kigeni mwenye umri zaidi ya miaka 15, Sh69,099 itamtoka huku kwa kijana mwenye miaka mitano hadi 15 atatakiwa kulipia Sh23,033. 

Kwa Watanzania, wataalamu na wakazi wa Afrika Mashariki gharama ya kutalii kwenye mbuga hizo ni Sh34,549 kwa watu wote walio juu ya miaka 15, huku kwa watu wenye miaka mitano hadi 15 wakitakiwa kulipa Sh11,516.

Kwa watoto wote chini ya miaka mitano hawahitaji kulipia senti yoyote kuuona uzuri wa Tanzania katika umri mdogo.

Hifadhi ya Taifa ya Gombe

Hifadhi hii ndiyo hifadhi yenye viwango vya juu zaidi vya tozo kati ya hifadhi zote nchini, kwa sababu mtalii wa kigeni kutembelea anahitaji kuwa na Sh320,330 huku kijana wa kigeni mwenye miaka 5 hadi 15 akilipia Sh46,066.

Mtanzania na mkazi wa Afrika Mashariki pia anagharamia Sh115,165 ikiwa ni pungufu mara mbili ya mtu mzima mgeni na kijana aliye chini ya miaka 15 akigharamia Sh23,033. 

Chaguo lako ni lipi kati ya hifadhi hizo kufanikisha mapumziko yako?