November 24, 2024

Zijue fursa zinazoweza kuwatoa vijana kimaisha

Fursa hizo zinaweza kuwasaidia vijana hao kutotegemea ajira ni pamoja na kufanya kazi za ushauri wa kifedha na dalali msomi.

  • Licha ya Serikali kutangaza upatikanaji wa mikopo kwa vijana bado vijana wanalalamika kukosa ajira na mitaji.
  • Kuna baadhi ya fursa za kibiashara ambazo mtu anaweza kuzianzisha kwa kiasi kidogo cha fedha.
  • Moses Samora ameshauri vijana kuamsha walichojifunza shuleni ama kufanya kitu wanachopenda.

Dar es Salaam. Hivi karibuni, Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilitoa takwimu kuwa vijana milioni 59 duniani hawana ajira huku milioni 136 kati ya vijana wote duniani wakiishi katika umaskini. Hata nyumbani hali si shwari sana. 

LIcha ya takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kubainisha kuwa ukosefu wa ajira umeendelea kushuka kutoka asilimia 10.3 mwaka 2014 hadi asilimia 9.7 mwaka 2018, bado kuna vijana wengi hasa wahitimu wa vyuo na vyuo vikuu wanahaha kupata vibarua vya kuwaingizia kipato jambo linalowaacha na mfadhaiko.

Wimbi la vijana hao hujikuta wakifanya kazi ambazo hawajasomea, wengine hukata tamaa na kuwa tegemezi kwa familia zao huku kisingizio kikiwa ni mitaji na kukosa watu wa kuwadhamini ili kuajiriwa kwa haraka.

Kati ya vijana waliofanikiwa kuepukana na changamoto ya ajira ni Bryson ambaye ni mhitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Kodi aliyesomea shahada ya usimamizi wa kodi na ushuru wa forodha na kuamua kuanza ujasiriamali kwa mtaji wa chini ya Sh10,000.

“Ni mwaka mmoja tangu nimemaliza elimu yangu ya chuo kikuu na kwa sasa ninajishughulisha na ujasiriamali wa chakula hasa vya uokaji,” amesema Bryson .

Kuachilia mbali na ujasiriamali kama afanyao Bryson, zipo baadhi ya fursa ambazo kijana yeyote anaweza kuzifanya zinazohitaji mtaji mdogo ambao kijana anawez akuumudu ama kwa kuchangiwa na ndugu na jamaa.  Nukta (www.nukta.co.tz) imeziangalia kiundani fursa hizo na kuzileta mbele yako. 

Vijana wengi hutazamia kazi za ofisini na zenye kuwalipa haraka. Picha |Mtandao.

Msaidizi binafsi

Kufanya kazi hii unahitaji kompyuta au simu janja ambapo vitu vyote vinapatikana kwa kiasi cha walau Sh400,000 tu. Kutokana na watu kuwa na mambo mengi wanayoyafanya, unaweza kuwasaidia kazi zao kwa kuwa msaidizi binafsi ambaye unaweza wakumbusha ratiba, mikutano na mambo ambayo wanaweza kuyafanya.

Kazi hii haihitaji ofisi bali ni kuwa na kifurushi kwenye kifaa cha mawasiliano hususan simu janja unayoweza kuweka kifurushi ya cha muda wa maongezi na intaneti cha Sh2,000 kwa siku tatu na kukusaidia kufanya kazi vyema. Kazi hii itakusaidia kupata ujira utakaosaidia kukuza mtaji wako na kupanua huduma hiyo. 

Mshauri wa mambo ya kifedha

Kazi hii inafaa zaidi watu ambao wamesomea masuala ya uchumi na fedha kwa kuwa wanauelewa zaidi. Kuna kampuni na watu binafsi wengi ambao wanahitaji huduma hii ambayo haihitaji mtaji mdogo hususan wa kufanikisha mawasiliano na nauli za kukutana na wateja. 

Moses Samora, moja kati ya watu ambao hukutana na vijana wengi katika kazi zake, anasema kuna namna mbili ambazo mhitimu yoyote anaweza kutizamia ili kuondokana na ukosefu wa ajira.

Amesema kijana yeyote anahitaji kufanyia kazi kile alichojifunza chuoni ama kufanya kitu ambacho anakipenda zaidi.

“Amsha ulichosemea shuleni na kukifanya huduma. Kama umesomea uchumi anza kufundisha watu juu ya masuala ya uchumi ama gundua kile ukipendacho na ukifanye,” amesema Samora ambaye ni mkufunzi na mtoa huduma zinazohusu usimamizi wa rasilimali watu. 


Zinazohusiana: 


Mpishi binafsi

Kuzingatia ukweli wa kwamba mabachela wengi hawafahamu kupika na wengineo hukosa muda wa kufanya hayo, hii inaweza kuwa fursa kwa kijana anayejua kupika. Anachohitaji mtu yeyote kufanya kazi hii ni nauli ya kumfikisha na kumrudisha kutoka “ofisini” kwake.

Kwa mujibu wa maelezo ya Samora, baadhi ya kazi zinahitaji mtu kuaminika kwani mtu kukukabidhi funguo ya nyumba yake inahitaji uaminifu sana.

Hata hivyo, sio rahisi kwa mtu kumaliza miaka mitatu na zaidi ya elimu bila kupata watu kadhaa anao wafahamu kwani watu hao hao ndio mtu anaweza kuanza nao.

Mwasilishaji wa bidhaa

Kazi hii inahusisha kufahamiana na watu ambao wametingwa na majukumu mengi kiasi cha kwamba kuwapa wazo la wewe kufanya kazi hiyo inaweza kuwapa ahueni.

Kijana anaweza kuwa anachukua oda za familia kadha wa kadha na kisha kununua mahitaji yao na kuyapeleka kwenye maeneo yanayohitajika. Kazi hii ni fursa kubwa kwani kuna familia nyingi ambazo zipo mbali na masoko hivyo kuifanya huduma hii kuwa kati ya fursa muhimu kwenye usawa huu wa kidijitali.

Dalali msomi

Sia Mrema ni moja kati ya madalali wasomi. Yeye ni mhitimu wa chuo kikuu lakini kwa sasa anauza nguo za kiume na vifaa vingine kama baiskeli, viatu na chochote anachoona kina uhitaji.

Siku moja Sia alitembelea maduka ya nguo Kariakoo jijini Dar es Salaam na kupiga picha baadhi ya bidhaa kwenye maduka kadhaa na kisha kuzipost kwenye WhatsApp status yake ambapo ndani ya siku moja aliuza mashati matano akitengeneza faida zaidi ya Sh10,000. Watu wengi waliomba kupelekewa bidhaa hiyo. Hadi sasa mtaji wa Sia umekua na ananunua na kuuza mwenyewe. Hapigi tena picha kufanya udalali kwa mwanzo.

“Ninatumia vyema mawasiliano niliyonayo na watu. Ndani ya mwaka mmoja, nina watu zaidi ya 10 ambao hawaendi madukani kununua nguo kwasababu wote hunifuata niwatafutie na kuwapelekea,” amesema Sia.

Kijana yoyete anaweza kugeuza elimu aliyonayo kuwa biashara. Hata mtu mwenye ufahamu wa ufundi seremala anaweza kuufanya ujuzi huo kuwa biashara yake bila kusubiri ajira | Picha na Mtandao.

Japokuwa fursa hizi hudharaulika kutokana na vijana wengi kutizamia kazi za ofisini na zenye kuwalipa haraka, bado zimeweza kuwanufaisha watu wengi ambao waliziona kama sehemu ya kujikwamulia.

“Mtazamo wa vijana wengi ni kuajiriwa ofisini hivyo kuona kazi zingine kama kazi zisizofaa hasa pale zinapohitaji nguvu kazi,” amesema Sia.

Samora ameenda mbali zaidi na kuainisha kuwa mtu yeyote anaweza kugeuza elimu yoyote aliyonayo kuwa biashara. Hata mtu mwenye ufahamu wa ufundi seremala anaweza kufanya ufahamu huo kuwa biashara yake.

Maelezo yake yameeleza kuwa mtu anaweza kujihusisha na ubunifu wa nyumba, kupanga nyumba na hata kupangilia bustani na ikampa faida endapo ndicho kitu anachopenda.

Tekla Buyamba (27) ni mjasiriamali anayelima mbogamboga mkoani Morogoro na yeye amesema kijana mwenye nguvu ni uzembe kukosa kazi.

Amesema Serikali imetoa nafasi kwa vijana kupewa mkopo ikiwa watakua katika vikundi na mikopo inashuhudiwa ikitolewa kwa vijana wanao kidhi vigezo lakini bado vijana wanalalamika.

“Kama wanaweza kujiunga kwenda kwenye sehemu kwa ajili ya “get together” wanashindwa nini kujipanga kwenda kuchukua mikopo?”

Tekla amesema ni wakati wa vijana sasa kuamka na kuchangamkia fursa zilizopo mbele yao kwani “Mchagua jembe sio mkulima”