Zingatia haya kabla hujanunua bidhaa mtandaoni
Kabla ya kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali mtandaoni, kuna baadhi ya vitu unavyotakiwa kuzingatia ili kupata bidhaa halisi uliyonunua na yenye kukidhi matakwa yako.
- Jiridhishe na aina ya kampuni inyotoa huduma ya manunuzi mtandaoni kama ina uhalali.
- Pitia sera za fidia na kurudisha bidhaa kama zina tija kwako.
- Hakiki anuani ya mahali unapoishi ili kuepuka mzigo kupotea.
Manunuzi ya bidhaa na huduma mtandaoni yanaongezeka kwa kasi duniani kutokana na ukuaji wa teknolojia na uhitaji wa watu kupata vitu kutoka sehemu tofauti duniani.
Kabla ya kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali mtandaoni, kuna baadhi ya vitu unavyotakiwa kuzingatia ili kupata bidhaa halisi uliyonunua na yenye kukidhi matakwa yako.
Izingatiwe kuwa bidhaa za mtandaoni huwezi kuzishika badala yake unaziona kwa picha na taarifa zake. Sasa zingatia haya wakati ukifanya manunuzi yako mtandaoni.
Jambo la kwanza kabla hujafanya manunuzi mtandaoni, jiridhishe na tovuti, programu tumishi au mahali unapofanyia manunuzi yako kama ni mfumo unaojulikana na unaweza kukupa bidhaa na huduma unayotaka.
Hii itakusaidia kuepuka matapeli ambao wanatumia mtandao kujipatia fedha kwa njia isiyo halali.
Baada ya kuhakikisha kama tovuti au programu tumishi ni sahihi kuna haja ya kuangalia kama programu tumishi hiyo inatoa huduma halisi. Mfano kama programu inawezesha kuuza nguo, iwe kweli inahusika na biashara hiyo.
Utambulisho wa programu tumishi ni muhimu kwa mteja kama anafanya malipo, kupata nakala ya risiti kuonyesha kwamba amefanya malipo ya kitu fulani kwa muda muafaka.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa
Mahali mzigo wako unatakiwa kufika ni jambo lingine la kuzingatia kwa sababu, wakati mwingine bidhaa inaweza kwenda kwa mtu asiye sahihi na kusababisha upotevu wa mzigo.
Hakiki anuani ya mahali unapoishi ili mzigo ukufikie kwa wakati na kuepuka usumbufu usio wa lazima.
Kama mteja unatakiwa kujua sera ya fidia na kurudisha (Return & Refund policy) ya kampuni husika mtandaoni ili kukuweka katika nafasi nzuri ya kukwepa hasara ikiwa mzigo utapata changamoto. Fahamu vizuri taratibu za kurudisha mzigo kama haukidhi mahitakji yako.
Kitu cha mwisho cha kuzingatia ni kuangalia maoni ya watu waliyowahi kutumia huduma husika ya manunuzi mtandaoni. Maoni ya watu yatakupa picha kamili ya ufanisi na ubora wa mfumo unaotaka kutumia kwa manunuzi mtandaoni.
Hata hivyo, manunuzi ya bidhaa kwa njia ya mtandao ni njia rahisi ya kujipatia bidhaa popote ulipo kwa kutumia simu yako ya mkononi, jambo linalookoa muda na gharama za kwenda dukani moja kwa moja.