October 6, 2024

Zingatia haya kabla kuanzisha biashara binafsi

Zingatia sheria na kodi zinazosimamia aina hiyo ya biashara ili kuhakikisha haingii katika migogoro ya kisheria.

  • Zifahamu sheria na wajibu wako katika biashara ya aina hiyo.
  • Faida na hasara za kumiliki biashara peke yako.

Biashara iliyofanikiwa ni ile inayotengeneza faida huku ikiimarika na kuongeza wigo wake wa masoko ili kuwafikia watu wengi. 

Lakini biashara nyingi zimekwama na kufa kabisa kutokana na kukosekana kwa ushauri sahihi wa sheria za biashara na mambo ya uchumi au elimu ya fedha.

Kila biashara ina taratibu zake za kuifanya kulingana. Swali la kujiuliza ufanye biashara kwa kutumia njia gani? Siyo kila mtu anaweza kulijibu vyema swali hili. 

Elimu ya sheria inahitajika ili kufumbua swali hili. Biashara zinaweza kufanywa kwa njia mbalimbali ambazo zinatambulika kisheria kutoka zile zinazomilikiwa na mtu binafs (sole trader), ushirika (Partnership), kampuni(Company) na hata Joint Venture.

Leo tunaangazia njia ya kwanza ya ufanyaji wa biashara ambayo inatumiwa na matajiri au wafanyabisahara wengi pasipo kuielewa vzuri. Njia hii ni biashara zinazoendeshwa na mtu mmoja. 

Kwa lugha rahisi  ni mtu mmoja anayefanya shughuli zake za kibiashara binafsi. Huyu ameanzisha biashara yake mwenyewe tangu chini kabisa.

Biashara ya aina hii inamilimikiwa na mtu mmoja tu. Yeye ndiye muamuzi wa mwisho wa kila kitu katika biashara yake na hakuna wa kupinga. Njia hii inategemea kila kitu kuanzia utendaji, usimamizi na uendeshaji mpaka maamuzi ya mwisho kutoka kwa muanzishaji au mmiliki wa biashara husika.

Mfano wa njia hii ni yale maduka ya mtaani kwa mfano maduka ya jumla au rejareja maarufu kwa Mangi au kwa Mkinga. Mtu anayefanya biashara hii hutumia jina lake au jina biashara kwa Mfano Hamza Lule Trading Company. 

Aina hii ya biashara inaweza kufanywa na mtu yeyote endapo atatimiza matakwa ya kisheria. Picha|Mtandao.

Sheria zinazosimamia aina hii ya biashara

Kama una mpango au tayari unafanya biashara kwa njia hii, hauna budi pia kufahamu sheria zinazosimamia ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata faida na kuepuka matatizo ya kisheria ikiwemo kesi za uhujumu uchumi na ukwepaji wa kodi. 

Baadhi ya sheria zinazosimamia biashara ya aina hii ni pamoja na Sheria ya Jina la biashara (Business name Registration Act CAP 213). 

Sheria hii inamtaka mtu anayefanya biashara kwa jina fulani kusajil jina lake liweze kutambulika na kulindwa rasmi kisheria. Shughuli ya usajili wa majina ya biashara iko mikononi mwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela)

“Sole Trader” anawajibika kwa Sheria ya Leseni za Biashara ya mwaka 1972 (Business Licensing Act of 1972) ambapo inataka kila mfanyabiashara awe ana leseni halali. 

Hivyo basi mtu binafsi analazimika kuwa na leseni kabla hajafungua biashara yake. Leseni zimegawanyika katika makundi  mawili; zinatolewa na halmashauri na Serikali kuu kupitia wizara mbalimbali. 

Kufanya biashara bila leseni ni kosa kisheria hivyo basi mfanyabiashara binafsi anapaswa kuwa na leseni ya biashara.

Pia anatakiwa kusajiliwa kama mlipa kodi kwa mujibu wa sheria za kodi ikiwemo Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani. Elimu ya kodi ni pana kiasi, somo hili tutalipa siku yake maalumu.

Sheria za kazi zinagusa biashara hiii. Kuwa sole trader haimanishi  hawezi kuajiri wafanyakazi la hasha! Anaajiri kulingana na mahitaji yake.

Hivyo basi maisha ya wafanyakazi hawa yanapaswa kufuata utaratibu wa kisheria uliowekwa ikiwemo malipo ya mishahara, likizo na uwepo wa mikataba hai yenye kukidhi vigezo vya kisheria.


Zinazohusiana: 


Wajibu wa mmiliki wa aina hii ya biashara

Sole trader atakua na wajibu wa kisheria kwa biashara zake zote anazofanya ikiwemo kushitaki na kushtakiwa kwa kutumia jina lake mbele ya mahakama. 

Ikiwa atashindwa mahakamani basi mali zake binafsi ndiyo zitataifishwa kuweza kulipa deni husika na ikiwa atashinda basi atalipwa kama yeye binafsi.

Maisha na uhai wa biashara ya sole trader utategemea maamuzi binafsi ya muhusika, kifo cha mmiliki. 

Hasara za biashara hii ni kuwa uhai wake unategemea zaidi maisha ya mmiliki. Picha|Mtandao.

Faida na hasara za kuwa Sole trader

Ni rahisi kuanzisha kwa lugha nyepesi haina mlolongo wala mambo mengi wa kuianzisha hivyo kwa sababu haihitaji mambo mengi kwa mfano hahitaji kuandaa andiko la biashara wala kufanya usajili mkubwa BRELA. Kinachohitajika ni mtaji tu.

Hakuna uhitaji wa vikao katika kuamua mustakabali wa maisha na uendeshaji wake na faida haigawanywi, kinachpatikana kinaenda moja kwa moja kwenye mikono ya mmilikii.

Hasara za biashara hii ni kuwa uhai wake unategemea zaidi maisha ya mmiliki. Kifo cha mmiliki au kufilisika kwa mmiliki ndiyo vinaamua uwepo wa biashara kwa sababu biashara iko chini ya mwamvuli wa mtu mmoja.

Hakuna utengano kati ya mmiliki na wakati mwingine huleta ugumu kupata mikopo na kujitanua zaidi kwa sababu ya aina ya uendeshaji na umiliki wake. Huwezi kusajili katika soko la hisa kwa sababu sheria na kanuni zinasimamia soko la hisa la Dar es salaam (DSE) haziruhusu mtu binafsi kujisajili kwenye soko hilo.

Biashara hii haina ukomo wa wajibu kisheria, Ikiwa mmiliki anadaiwa kisheria yuko hatarini kufilisiwa mpaka mali zake binafsi ambazo hazipo kwenye biashara na wala hazihusiani na baishara zake.

Makala ijayo tutaangazia aina nyingine za ufanyaji biashara kama ilivyoanishwa kwenye utangulizi hapo juu.

Makala hii imeandaliwa na Hamza Lule, Wakili wa Mahakama Kuu na Mahakama za chini Tanzania. Kwa msaada wa kisheria wasiliana naye kupitia 0717521700 au Twitter: @Hamzaalbhanj