November 24, 2024

Zingatia haya kabla ya kuthibitisha habari ya uzushi kuhusu Corona

Ni muhimu kuyafahamu kabla ya kuthibitisha habari yoyote ya uzushi kuhusu Corona.

  • Uwe na taarifa za kutosha juu ya habari unayotaka kuthibitisha
  • Vijue vyanzo na zana za kidijitali utakazotumia kuthibitisha. 

Dar es Salaam. Kutokana na kasi ya kusambaa kwa habari za uzushi mtandaoni hasa kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga Corona, huenda ukawa miongoni mwa watu wanaotamani kuthibitisha habari fulani inayosambaa ili kuzuia isilete madhara zaidi kwa jamii yako.

Kabla ya kuthibitisha habari yoyote ya uzushi au uliyo na mashaka nayo, kuna baadhi ya mambo unayotakiwa kuyafahamu au kuzingatia ili kuondoa utata wa habari unayotaka kujua ukweli wake. 

Hakikisha una taarifa za kutosha

Jambo la kwanza ni kuwa na taarifa za kutosha juu ya habari unayoitafutia ukweli. Hii itakusaidia kujua kwa undani wa kitu unachokitafutia ukweli na kukupa ujasiri unapokipeleka kwa jamii.

Fahamu habari hiyo imetoka wapi, nani kaitoa na madhumuni yake. Hii itakupa picha ya kuifanyia kazi. 

Baada ya kuwa na taarifa za kutosha juu ya habari unayoithibitisha, ni muhimu kujua vyanzo vya uhakika zikiwemo mamlaka zilizoidhinishwa kutoa taarifa kuhusu COVID-19. 

Tafuta zana za kidijitali kubaini ukweli zaidi

Angalia kama habari husika imetoka katika vyanzo sahihi na kama siyo unaweza kuendelea na hatua zinazofuata za kutafuta zana za mtandaoni zitakazokusaidia wakati unaanza kuthibitisha ukweli wa habari husika.


Zinazohusiana:


Zana za uthibitishaji wa habari hutegemea aina ya habari iliyopotoshwa. Mfano habari ambayo iko kwenye mfumo wa picha ina zana za kuithibitisha ikiwemo TinyEye na Google Image. 

Jifunze namna ya kuzitumia zana hizo ili kukurahisishia kila unapopata famba mtandaoni kuhusu COVID-19.

Vilevile, hakikisha unajua namna sahihi ya kuandika habari unayotaka kuithibitisha ili wasomaji au wasikilizaji waweze kuelewa kwa urahisi ujumbe unaowapelekea. 

Ufahamu huo utakusaidia siyo tu kuthibitisha habari bali kutambua kwa haraka kila habari ya uzushi inayokufikia katika viganja vya mikono yako kupitia mtandaoni.