Zingatia haya wakati ukifanya manunuzi msimu wa sikukuu
Jipange na tengeneza bajeti kabla ya kununua bidhaa na fanya manunuzi mtandaoni, epuka gharama kubwa zisizo na msingi ili kuwafurahisha watu.
- Jipange na tengeneza bajeti kabla ya kununua bidhaa.
- Fanya manunuzi mtandaoni, epuka gharama kubwa zisizo na msingi ili kuwafurahisha watu.
Msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na mwaka mpya umefana. Katika kipindi hiki wengi wapo katika mapumziko na familia zao ili kujitathmini na kuweka mambo sawa kwa ajili ya kuanza mwaka mpya wa 2019.
Pamoja na hayo, kipindi hiki huusisha manunuzi makubwa ya bidhaa na huongeza matumizi ya pesa katika ngazi ya familia. Lakini kwa wafanyabashara ni kicheko kwasababu mauzo na faida zinaongezeka maradufu.
Sikukuu inaweza kuwa furaha lakini pia ikawa ni maumivu kwa baadhi ya watu. Ili kujiepusha na maumivu baada ya sikukuu hizi za mwisho wa mwaka, jaribu mambo haya ili kuhakikisha manunuzi yako yanaendana na hali yako ya kifedha.
Jipange kabla ya kufanya manunuzi
Ni vema kutengeneza bajeti ya vitu utakavyonunua kabla ya kwenda dukani ili kujiweka katika nafasi ya kutokutumia kiasi kikubwa cha fedha bila kutarajia.
Hiyo inatokana na ukweli kuwa maduka mengi yana bidhaa nyingi za kuvutia ambapo usipokuwa makini utajikuta unataka kununua kila kitu ili kutimiza furaha yako. Jipange kabla ya kufanya manunuzi na dhibiti tamaa ya kudisha manunuzi (Shopping spree).
Fanya manunuzi mtandaoni
Manunuzi ya bidhaa mtandaoni yatakusaidia kupunguza kidogo gharama za usafiri na muda utakaotumia kutembelea maduka mbalimbali katika eneo lako. Pia itakuepusha na msongamano wa watu na magari yanayokwenda katika maduka makubwa.
Njia hii ni nzuri kwa sababu mnunuzi anakuwa na uchaguzi mpana wa bei za bidhaa zinaonekana mtandaoni na akikamilisha oda yake, bidhaa inamfikia alipo.
Pia unaweza kutumia programu ya kufuatilia na kulinganisha bei za maduka mbalimbali (CamelCamelCamel au The Tracktor) ili kufanya maamuzi sahihi na kupata punguzo la bei.
Njia hii ni nzuri kwa sababu mnunuzi anakuwa na uchaguzi mpana wa bei za bidhaa zinaonekana mtandaoni na akikamilisha oda yake, bidhaa inamfikia alipo. Picha| marketingland.com
Nunua bidhaa inayodumu muda mrefu
Unaweza kununua bidhaa ambayo itatumika hata baada ya msimu wa sikukuu kuisha ili kupunguza gharama za kununua bidhaa ya aina moja mara kwa mara.
Sambamba na hilo nunua bidhaa ambayo inapendwa na familia yako ili kujenga kumbukumbu inayoweza kusaidia kuimarisha upendo na uhusiano wenu.
Hata hivyo usiogope kununua bidhaa nyingi za aina moja hasa kama ni zawadi ambazo unataka kuwapa watu wengi, kwa sababu maduka yanatoa ofa mbalimbali kama “Nunua 1 upate mbili”.
Fanya manunuzi kwenye maduka makubwa (Shopping Malls)
Iwapo umeshindwa kufanya manunuzi mtandaoni, unaweza kwenda katika maduka makubwa ambayo hutoa huduma mbalimbali kama migawaha, burudani, kumbi za starehe na maegesho ya magari yasitoza fedha nyingi.
Hii itakurahisishia kama mmetoka familia yote kwenda katika manunuzi na kukusaidia kupunguza gharama za kutembelea maeneo tofauti tofauti.
Kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam maduka hayo ni kama Mlimani City, City Mall, Quality Centre na Shoppers ambayo yanakupa wigo mpana wa kupata huduma nyingi kwa wakati mmoja.
Hii itakurahisishia kama mmetoka familia yote kwenda katika manunuzi na kukusaidia kupunguza gharama za kutembelea maeneo tofauti tofauti. Picha|gawker.com
Usifanye manunuzi wikiendi
Siku za mwisho wa wiki, maduka mengi huwa na msongamano mkubwa wa watu, kama hupendi kashikashi basi kamilisha manunuzi yako siku za kawaida hasa nyakati za jioni.
Nenda dukani peke yako licha kuwa haifurahishi ukilinganisha kama uko na marafiki au familia. Hii itakusaidia kuokoa muda na kukuepusha na ushawishi wa kutumia pesa nyingi kwa mambo yasiyo ya lazima.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa
Fahamu muda muafaka wa kufanya miamala
Kila mtu ana akaunti yake ya benki au simu inayoitumia kutunza pesa. Kama bado hautumii mtandao kufanya malipo, ni muhimu kufanya miamala mapema kuliko kusubiri mpaka siku ya manunuzi ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.
Hii itakusaidia pia kujua kiasi cha pesa ulichonacho na kama bajeti haitoshi utatafuta namna ya kuweka sawa.
Hata hivyo, mapumziko ya mwisho wa mwaka ni kipindi cha kushusha pumzi, kujumuika na marafiki, familia na ndugu ili kuepuka shughuli zinazoweza kukuletea msongo wa mawazo.
Panga mambo yako vizuri, fanya manunuzi kulingana na uwezo wako. Kumbuka kuna maisha baada ya sikukuu!