Zingatia haya wakati ukiwasiliana na mteja wako
Mambo hayo ni pamoja na kuwa msikivu, ongea unachokijua kwa ufasaha na tumia lugha ya mwili ikiwemo tabasamu.
- Mambo hayo ni pamoja na kuwa msikivu, ongea unachokijua kwa ufasaha na tumia lugha ya mwili ikiwemo tabasamu.
- Epuka kuwajibu wateja wako majibu ya mkato na wape nafasi kutoa maoni kwa bidhaa na huduma yako.
- Ile uwe mzungumzaji mzuri basi tenga muda wa kujifunza vitu mbalimbali kuhusu biashara yako.
Dar es Salaam. Changamoto kubwa inayowakumba watu wengi wakiwemo wafanyabiashara ni kushindwa kuwasiliana na baadhi ya watu wakihofia muonekano na jinsi watu walivyojiweka.
Wengi husahau kuwa ni rahisi kujenga mtazamo binafsi juu ya mtu kwa muonekano wake lakini haimaanishi kuwa mtazamo wako ni ukweli kwani muonekano hauelezi kila kitu ikiwemo tabia ya mtu.
Kwa vyovyote vile, mawasiliano ni nguzo muhimu katika biashara kwani inajenga na kuimarisha mawasiliano na wateja, wabia na washirika wa biashara.
Haya ndiyo mambo ambayo mfanyabiashara anapaswa kuzingatia wakati akiwasiliana na mteja wake:
1. Jifunze kusikiliza
Wapo wafanyabiashara ambao hawana tabia ya kusikiliza wateja wao. Wengi hutazamia mauzo ya mara moja yaani auze bidhaa au huduma yake na aendelee na shughuli zake.
Wafanyabiashara hao husahau kuwa kumsikiliza mteja, inampa uwezekano wa kumfikiria yeye mara zote anapohitaji bidhaa au huduma fulani kwa sababu ya kupewa kipaumbele.
Pia kumsikiliza mteja kunamjengea hisia kuwa anathaminiwa na ni sehemu ya biashara yako kwa sababu anaweza kutoa maoni na ushauri ukapokelewa.
Pale mteja anaposikilizwa, inamjengea uhusiano mzuri na mfanyabiashara. Picha| Mtandao
2. Tumia vifungua mazungumzo, zuia majibu ya mkato
Kuna muda mteja anauliza maswali mengi pasipo kununua kitu chochote mwishoni. Wengi wanafadhaika na hali hiyo na hivyo kutoa majibu ya mkato kwa wateja.
Mkufunzi wa wajasirimali katika masuala ya masoko, Charles Nduku maarufu kama Mr Brand anasema vifungua mazungumzo ni pamoja na tabasamu, salamu na umakini kwa mteja wako.
Kama mfanyabiashara, unatakiwa kujua kuwa majibu yako ni sehemu ya huduma kwa wateja. Wateja wengine huuliza maswali ili kujua bei na kulinganisha bei ili kufanya maamuzi ya manunuzi ya jumla baadaye.
Ni vizuri endapo utakuwa mchangamfu kwa wateja wako na kufanya nao mazungumzo kwa upole na usikivu. Inampa mteja hali ya kukuzoea na kukufikiria wewe kila anapohitaji bidhaa na huduma.
3. Jifunze kutumia Lugha ya mwili
Fikiria pale mtu anapokuongelesha huku ameweka mikono mifukoni au unapoongea naye anaangalia saa mara kwa mara. Hivyo ni baadhi ya vitu vidogo vidogo ambavyo huathiri mazungumzo na mawasiliano.
Nduku maarufu kama Mr Brand anasema wakati wa kuongea, basi na viungo vya mwili wako vithibitishe kile kinachotoka mdomoni mwako.
Kama mfanyabiashara, unahitaji kuyapa mazungumzo yako maisha ili mtu unayezungumza naye apate mshawasha wa kuendelea kukusikiliza.
Unaweza kufanya hayo kwa kung’arisha sura yako kwa tabasamu na kuongea kwa mifano inayoendana na mazingira.
Zinazohusiana
- Namna huduma kwa wateja inavyoweza kukuza brand ya biashara
- Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara
4. Epuka aibu, waangalie watu machoni
Tangu tukiwa shule, walimu walifundisha kuangalia watu machoni pale unapofanya wasilisho darasani. Hiyo ni kwa sababu kuna siri iliyojificha nyuma ya lugha hiyo.
Mr Brand anasema kwa kufanya hivyo, inamfanya mtu kuona namna gani una uhakika na jambo unalozungumza na hata umakini wako juu ya kitu unachoongelea.
Vuta taswira hii, unafanyiwa wasilisho la bidhaa na mtu halafu mtu huyo hawezi kukutazama hata usoni. Hawezi hata kunyanyua sura yake kukuelezea kitu anachofanya.
Ni dhahiri kuwa utapoteza hamu ya kumsikiliza na utakuwa na mashaka na kitu anachokifanya. Ni muhimu kwa mfanyabiashara yeyote kuishinda aibu na kufanya mawasilisho yake kwa kujiamini.
Nduku maarufu kama Mr Brand anasema wakati wa kuongea, basi na viungo vya mwili wako vithibitishe kile kinachotoka mdomoni mwako. Picha| Mtandao.
5. Fahamu yanayoendelea kwenye jamii yako na jifunze mambo mbalimbali.
Siyo vibaya ukijua jinsi mashine ya kutolea vivuli “photocopy machine” inayofanya kazi au hata kufahamu jinsi ya kutumia kompyuta na kamera ama jinsi ya kuunganisha projekta.
Ninalojaribu kuzungumzia hapa ni hali ya wafanya biashara kujihusisha na jambo moja tu. Siyo vibaya lakini pia katika ulimwengu sasa, ni vizuri ukiwa na taarifa mbalimbali zinazoendelea au hata kuchukua kozi ya masoko pale unapoweza.
Kujua mambo mengi kutaongeza ujuzi na uwezo wako wa kuwasiliana na watu wengine kwa sababu utakuwa na taarifa za kutosha kwa kile unachozungumza.
Biashara ni mawasiliano, yakikosekana, bidhaa na huduma yako havitapata wateja wa kununua. Imarisha mawasiliano na wateja wako.