Zola kuwekeza zaidi Sh69 bilioni katika sekta ya umemejua Tanzania
Uwekezaji huo utawezesha kuziunganisha nyumba mpya 145,500 kwa umemejua na kutengeneza ajira zaidi ya 2,100 hasa za vijijini ambako umeme wa gridi ya Taifa haujafika.
Watu bilioni 2.2 duniani hawajafikiwa na umeme. Nishati jadidifu ni mkombozi kwa watu waliopo nje ya mfumo wa umeme wa gridi ya Taifa. Picha| Energy Storage News
- Fedha hizo zimetolewa na benki ya Maendeleo ya Ujasiriamali (FMO) ya nchini Uholanzi na kampuni ya Symbiotics ambayo inahusika kufadhili mitaji ya uwekezaji kwa miradi endelevu inayolenga kutatua changamoto za maendeleo katika jamii.
- Uwekezaji huo utawezesha kuziunganisha nyumba mpya 145,500 kwa umemejua na kutengeneza ajira zaidi ya 2,100 hasa za vijijini.
Dar es Salaam. Huenda idadi ya Watanzania wanaonufaika na umemejua ikaongezeka katika kipindi cha miaka mitano ijayo kutokana na kampuni ya Zola Electric kupata ufadhili wa Dola za Marekani milioni 32.5 (zaidi ya Sh69 bilioni) kwaajili ya usimamizi na uendeshaji wa shughuli zake hapa nchini.
Jarida la Renewable Now limeeleza katika taarifa yake kuwa ikiwa fedha hizo zitatumika vizuri zitawezesha kuziunganisha nyumba mpya 145,500 kwa umemejua hasa za vijijini ambako umeme wa gridi ya Taifa haujafika.
Fedha hizo zimetolewa na benki ya Maendeleo ya Ujasiriamali (FMO) ya nchini Uholanzi ambayo imetoa Dola za Marekani milioni 5 kama mkopo kutoka katika mfuko wake wa nishati (Access to Energ Fund) na Dola milioni 12.5 kama fedha ya Uwekezaji.
Kiasi kingine kilichobaki cha Dola milioni 15 kimetolewa na kampuni ya Symbiotics ambayo inahusika kufadhili mitaji ya uwekezaji kwa miradi endelevu inayolenga kutatua changamoto za maendeleo katika jamii.
Zinazohusiana:
- Lucy, katuni aliyejizatiti kupunguza mimba za utotoni Morogoro
- Umemejua kimbilio kwa waliopitwa na gridi ya taifa
Uwekezaji huo unatarajia kutengeneza takribani ajira 2,100 katika maeneo yasiyofikiwa na umeme wa gridi ya Taifa nchini.
“Tuna furaha kutangaza uwekezaji huu mpya kutoka FMO na Symbiotics.Utatuwezesha sisi kuwaunganisha watu wengi Tanzania, kuisaidia jamii katika maeneo tunayofanya kazi na kuendeleza shughuli zetu za kufunga mifumo ya umeme,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Zola Electric, Bill Lenihan wakati wa kutangaza uwekezaji huo Jijini Amsterdam, Uholanzi Desemba 10 mwaka huu.
Kampuni hiyo ambayo inashirikiana na taasisi zingine ikiwemo za Tesla na GE Ventures inawahudumia zaidi ya wateja 1,000,000 katika nchi tano za Afrika ikiwemo Tanzania ambapo mpaka sasa imeajiri zaidi ya watu 1,000.
Licha ya kujitanua na kukua kwa kampuni ya Zola Electric, bado kuna rasimamali muhimu hazijafikiwa na kutumika katika sekta ya nishati jadidifu, ikizingatiwa kuwa hadi sasa watu bilioni 2.2 duniani hawajafikiwa na umeme.