May 19, 2024

Namna ya kutokomeza matukio ya ubakaji Tanzania

Ubakaji ni matukio ambayo hayawezi kuzuiwa na doria za polisi mitaani pekee kwa kuwa sehemu kubwa ya hufanyika katika mazingira ya kificho kama majumbani, mashambani na hata mashuleni.

  • Matukio ya ubakaji hayawezi kuzuiwa na doria za polisi mitaani pekee kwa kuwa sehemu kubwa ya hufanyika katika mazingira ya kificho.
  • Madhara ya ubakaji hayaishii siku ambayo mtu atabakwa kwa sababu huzalisha matatizo mengi zaidi baada ya tukio kutokea.
  • Wadau washauri jamii iwekeze katika elimu na kuongea na watoto ili kuwaelewesha kuwa ubakaji upo na wanapaswa pia kujilinda. 

Dar es Salaam. Katika sehemu ya kwanza ya makala haya tuliangazia ongezeko la makosa ya ubakaji nchini na namna baadhi ya waliofanyiwa ukatili kwa kubakwa wanavyokosa haki kwa kesi zao kumalizwa ndani ya familia.

Ripoti ya Takwimu Muhimu za Tanzania mwaka 2019 (Tanzania in Figures 2019) ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) imeeleza kuwa makosa ya ubakaji yameongezeka kwa asilimia 2.8 kufikia makosa 7,837 mwaka jana kutoka 7,617 mwaka 2018.

Leo tunaangazia kwa undani athari anazoweza kupata muathirika na jinsi wadau wanavyopambana kutokomeza vitendo hivyo kwenye jamii.

Athari za kubakwa ni zaidi ya maumivu ya mwili

Daktari kutoka kituo cha afya cha AAR cha jijini Dar es Salaam, Dk Julieth Seba amesema madhara ya ubakaji hayaishii siku ambayo mtu atabakwa kwa sababu huzalisha matatizo mengi zaidi baada ya tukio kutokea.

“Wengi wanaobakwa ni watoto  wadogo. Baada ya ubakaji, wapo watakaokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito. Wengine wanaishia kupata magonjwa yanayoambukiza kwa kujamiana,” anasema Dk Seba.

                           

Mambo yatakayosaidia kupunguza ubakaji 

Mwanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia Ritha Tarimo anasema ili kupunguza vitendo vya ubakaji Tanzania, jamii yapaswa kuwekeza katika elimu na kuongea na watoto ili kuwaelewesha kuwa ubakaji upo na wanapaswa pia kujilinda. 

“Kama nchi, tuinuke pamoja, tusaidiane, turudi katika mafundisho ya upendo na hali ya umoja na ya kumuona mtoto wa mwenzako kama wako. Tuwekeze katika elimu hasa elimu ya kujilinda na kufundisha uhalisi wa kuwa ubakaji upo una unatokea,” amesema Tarimo.

Amesema ushirikiano wa wadau mbalimbali utasaidia pia kumaliza tatizo hilo la ubakaji na kuongeza uwajibikaji kwenye jamii. 


Viongozi wa dini kuokoa jahazi

Mratibu wa Shirika la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa amesema viongozi wa dini wanapaswa kushirikishwa kikamilifu kwa kutoa mafundisho kwa watu ili waache kushiriki katika vitendo hivyo.

Mbali na mafundisho ya kidini, mwanaharakati huyo mashuhuri anashauri kuwa sheria na mifumo ya kisheria dhidi ya ubakaji ieendelee kuboreshwa ili kuwadhibiti wa vitendo hivyo nchini. 

Ubakaji hauisumbui jamii na Tanzania pekee. Mamlaka nazo zinahaha kutokomeza uhalifu huo ambao huacha athari lukuki kwa waathirika ikiwemo matatizo ya kisaikolojia, mimba zisizotarajiwa, magonjwa hatari kama Ukimwi na wakati mwingine majeraha yaletayo vilema vya kudumu. 


Zinazohusiana


Polisi kuwashughulikia wabakaji

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania David Misime ameiambia Nukta kuwa tatizo la ubakaji duniani lina historia ndefu na linaendelea kuongezeka kadri siku zinavyokwenda.

Misime amesema ubakaji ni matukio ambayo hayawezi kuzuiwa na doria za polisi mitaani pekee kwa kuwa sehemu kubwa ya hufanyika katika mazingira ya kificho kama majumbani, mashambani na hata mashuleni.


Kinachofanywa na serikali

Misime amesema polisi na taasisi nyingine za Serikali wanaendeela na utoaji wa elimu kwa umma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kusimamia kesi za ubakaji kuanzia ngazi ya chini hadi mahakama.

“Tunaamini jamii ikiwa na uelewa wa pamoja juu ya ubaya na madhara ya  ubakaji mafanikio ya kuzuia yatakuwa makubwa,” ameeleza Misime.

Misime amesema jeshi hilo limefanikiwa kujenga ofisi za madawati ya jinsia na watoto zaidi ya 400 nchini yanayoshughulikia kesi za unyanyasaji wa kijinsia ikiwepo ubakaji.

“Tushirikiane kwa pamoja katika kuelimishana kuanzia ngazi ya familia ili kubaini na kuzuia matukio haya. Jamii isifiche matukio haya,” amesema Misime akisisitiza kuwa utoaji wa taarifa utachochea vita ya kutokomeza kabisa vitendo hivyo.