Mambo yanayochochea matumizi makubwa ya petroli kwenye gari
Wakati baadhi ya wamiliki wa magari wakidhani gari imeharibika au vituo vya kuweka mafuta vinawaibia, saa zingine ni tabia zao ndio sababu ya matumizi ya mafuta kuwa makubwa.
- Ni pamoja na kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu.
- Pia kulazimisha gari kuwa na mwendo kasi ghafla.
- Matumizi ya kiyoyozi na kushindwa kufanyia gari marekebisho.
Dar es Salaam. Kwa baadhi ya wamiliki wa magari, jambo linalokera ni pale matumizi ya mafuta yanapoongezeka huku kipato chao kikiwa bado ni kilekile.
Baadhi yao hufikirii gari limechoka kiasi cha kutaka kutafuta lingine na wengine hushutumu vituo vya kuuza mafuta kutokuweka kiwango stahiki cha mafuta wanaponunua.
Hata hivyo, watu hao wanatakiwa kufahamu kuwa zipo tabia na mazingira yanayosababisha matumizi ya mafuta kuongezeka ikiwemo matumizi ya gia yasiyo sahihi wakati wa kuendesha gari.
Mfanyabiashara wa Kariakoo, Peter Mashauri ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa wakati wa kuendesha gari mtu anatakiwa kutumia gia sahihi katika eneo sahihi.
Peter ambaye anamiliki gari amesema pale unapoweka gia ambayo siyo sahihi katika eneo fulani, inalilazimu gari kutumia nguvu nyingi na hivyo kutumia mafuta mengi pia.
“Unaposhindwa kuweka gia sahihi kwa wakati, gari lako lazima uone matumizi ya mafuta ni makubwa. Mfano upo kwenye mlima na ukaenda na gia namba moja, gari inakuwa inatumia nguvu ya ziada. Ndio maana unaona magari ya mkoa yakifika kwenye mteremko yanatumia gia huru (neutral gear),” amesema Mashauri.
Matumizi ya gia sahihi katika wakati sahihi yataokoa mafut yako. Picha| Google Images.
Sababu nyingine za kuongezeka kwa matumizi ya “wese” ni hizi hapa:
Matumizi ya kiyoyozi
Kiyoyozi husaidia kujikinga na joto la nje ya gari lakini pia huhitajika kutumika kwa ajili ya kuzungusha hewa ndani ya gari pale vioo vinapokuwa vimefungwa ili kuepusha vumbi la nje kuingia kwenye gari.
Kwa mujibu wa mashauri, hali hiyo pia ni sababu ya gari kutumia mafuta mengi.
“Unapokuwa kwenye lami, kama hamna ulazima wa kufunga vioo, shusha madirisha upate hewa safi ya nje, unazima kiyoyozi unakuwa unasevu mafuta,” amesema Mashauri.
Foleni na msongamano wa magari barabarani
Hii hutokea katika muda ambao watu wanakuwa katika haraka ya kuwahi makazini na majumbani kwao hasa siku za wiki ambapo magari mengi yanatumia barabara na hivyo kusababisha foleni.
Hali hiyo huwafanya madereva wengi kuziacha gari zao zikiunguruma bila kuzizima wakijiandaa na kusogea pale gari zao zitakapoitwa na trafikia au taa za barabarani.
Wakati hali hiyo ikiwa ni kawaida katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, pale gari linapoendelea kufanya kazi wakati hausogei, haimaanishi kuwa mafuta hayatumiki.
Mkazi wa Morogoro, Martha Wiliam amesema hali hiyo husababisha magari kuishiwa mafuta wakiwa barabarani na kulazimika kutoa pesa ambayo ipo nje ya bajeti kuongeza mafuta.
“Unakuta umekaa kwenye foleni nusu saa nzima unasubiri msafara au ajali imetokea. Mafuta yanakuishia unalazimika kusukuma gari au kuingia gharama za kutuma bodaboda akufuatie mafuta,” amesema William.
Gari linapoendelea kufanya kazi wakati hausogei, haimaanishi kuwa mafuta hayatumiki. Picha| Google Images.
Gari inaposhindwa kufanyiwa “service”
Baadhi wamiliki wa magari husahau kupeleka gari zao kufanyiwa huduma, almaarufu kama “service” ambayo huhusisha kubadilisha mafuta ya gari, kusafisha machujio ya gari na huduma zingine ikiwemo kuweka uwiano wa matairi.
William amesema, pale gari inapokosa huduma hizo, inakuwa inachangia pia matumizi makubwa ya mafuta.
“Ukipita muda wa matumizi ya oili (oili ya injini na oili zingine za gari) ama filters (machuujio) kuwa chafu na mabomba ya gari kuvuja husababisha kuongezeka kwa matumizi ya mafuta,” amesema William.
Kukanyaga kitufe cha mafuta ghafla
Hali hii inaweza kutokea pale unapohitaji kupita mbele ya gari lingine kwa haraka. Baadhi hukanyaga pedo ya mafuta kuilazimisha gari iende kwa kasi zaidi.
Mdau wa usafiri huo, Ivan Phares ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, hali hiyo inafanya mzunguko wa injini ya gari kuwa juu hivyo ulaji wa mafuta huongezeka.
“Kulazimisha gari kwenda ghafla kwenye mwendo mkubwa kitaalamu wanasema “forced acceleration” inafanya gari kuongeza ulaji wa mafuta. Unashauriwa unapokanyaga pedo ya mafuta, mshale wa kuonyesha mzunguko wa injini usipende kuzidi RPM 2,” amesema Phares.
Kuna nini unachohitaji kujifunza kuhusiana na magari? Wasiliana nasi tukupatie mawazo ya wataalam na wadau wa usafiri huo. Unaweza kutufikia kupitia mitandao ya kijamii (Instagram, Facebook, Twitter na Telegram) kupitia @NuktaTanzania.