May 18, 2024

Mambo ya kuangazia wakati unafanya manunuzi ya gari

Ni muhimu kuhakikisha unanunua gari zima ambalo halitokusumbua na kukuingizia gharama ambazo haujajiandaa nazo.

  • Urahisi wa upatikanaji wa vipuri gari likiharibika.
  • Uwezo wake wa kuhimili barabara za vumbi.
  • Uwezo wa injini na ufanisi wa sehemu muhimu ndani ya gari. 

Dar es Salaam. Mbali na kuwa matumizi ya gari ni kumsafirisha mtu kutoka sehemu moja hadi nyingine, wakati wa kununua chombo hicho cha usafiri unahitaji kufahamu baadhi ya mambo ili usijikute umenunua usafiri ambao utakutesa badala ya kukurahisishia maisha.

Mambo hayo ya kuzingatia ni pamoja na kuwa na uhakika wa vifaa muhimu vya gari kama vinafanya kazi ikiwemo taa, vifuta vioo, magurumu, betri la gari na vinginevyo.

Mdau wa magari wa jijini Dar es Salaam, Santus Salvatory ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa manunuzi ya gari yanaenda mbali zaidi ya fedha uliyonayo kwani ni muhimu kuhakikisha unanunua gari zima ambalo halitokusumbua na kukuingizia gharama ambazo haujajiandaa nazo.

“Yapo mambo mengi ya kuzingatia. Mengine ni makubwa na mengine ni madogo, mfano kukagua kama taa zote zinafanya kazi ili kuepuka gharama za kubadilisha taa baada ya kununua, kuangalia kama vipangusa vioo vipo sawa, betri na kama uskani wa gari unafanya kazi ipasavyo,” ameshauri Salvatory.

Kagua injini na betri la gari hiyo kabla ya kutoa fedha zako

Ile furaha ya kuachana na tabu za kugombania daladala inaweza kuwa sababu ya baadhi ya wanunua magari kukimbilia kutoa fedha bila kukagua kama gari hizo zipo sawa na kweli zitarahisisha maisha badala ya kuongeza gharama.

Salvatory amesema, kuangalia vitu vya muhimu ikiwemo injini na betri ambalo linafanya kazi ya kusambaza nishati ya umeme kwenye gari ni muhimu wakati wa manunuzi ili kuepuka kununua betri lingine.

“Endapo utaingizwa mjini na kuuziwa gari ambalo injini yake ni mbovu, safari zako kuelekea gereji zitakuwa ni nyingi kuliko hata safari za kwenda kwenye mishemishe zako,” amesema mdau huyo.

Hakikisha sehemu muhimu za gari zinafanya kazi vizri ikiwemo injini ya gari. Picha| Best Cars.

Sehemu ya uskani wa gari 

Kwa Tanzania, imezoeleka dereva huwa katika upande wa kulia wa gari lakini kwa nchi zingine, uskani wa dereva huwa katika upande wa kushoto.

Mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Peter Mathias amesema endapo utanunua gari ambalo uskani wa dereva upo kushoto, itakupatia tabu kuzoea kuendesha gari lako katika barabara za Tanzania.

“Wapo ambao gari zao mfumo wake wa uskani upo kushoto lakini wanapata shida ya kuzoea uendeshaji wa gari zao katika nchi kama Tanzania ambazo magari mengi uskani wa dereva upo kulia ukiwa ndani ya gari,” amesema Mathias ambaye ni mmiliki wa gari binafsi.

Wakati wa kuagiza, usisahau hilo ili usivuruge furaha yako ya kupata gari la ndoto yako.

Eneo ambalo gari yako itatumika

Huenda baadhi ya watu wanasahau kuangalia jambo hili wanapokuwa wanafanya manunuzi ya gari zao lakini ni kitu muhimu kuzingatia kwa ajili ya usalama wa gari yako. Mazingira unayoishi au sehemu gari  litapotumika ni muhimu kuzingatia.

Mkazi wa Dar es Salaam, Ivan Phares amesema endapo utanunua gari ya chini wakati unaishi au gari inafanya kazi kwenye sehemu ambazo hamna barababra nzuri, utakuwa unaitesa gari hiyo.

“Mfano mtu wa kijijini anahitaji gari ngumu na za juu kama “Pickup” hasa kama barabara haziko vizuri,” amesema Phares.

Ili gari lako lidumu muda mrefu, pia inategemea linatembea katika barabara gani. Picha| Revv.

Upatikanaji wa vipuri vya gari (spare parts)

Kuna wakati gari yako itaharibika utahitaji kununua vipuri. Lakini itakuwaje endapo utazunguka maduka yote ya kuuza vipuri vya magari na usipate? Ni lazima uingie gharama ya kuagiza nje ya nchi ambapo itakugharimu pesa zaidi.

Phares amesema pale unaponunua gari kwa njia yoyote, ni vyema kuhakikisha kuwa “spea” za gari lako zinapatikana kwa wingi ili pale sehemu ya gari yako inapoharibika, uwe na uwezo wa kurekebisha haraka na kuendelea na matumizi.

“Unaweza nunua ferari lakini spare (vipuri vya gari) hapa nchini hamna,” amesema Phares.

Andiko hili ni muendelezo wa makala zingine nyingi zinazohusu magari kutoka Nukta Habari ikiwemo orodha ya magari yanayonunuliwa zaidi na Watanzania, namna ya kupunguza joto kwenye gari yako na tabia zinazochochea matumizi makubwa ya petroli. 

Endelea kusoma habari za Nukta kwa yanayokuhusu ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu magari na matumizi yake.