May 18, 2024

Mambo ya kuzingatia unaponunua jagi la kuchemshia maji

Unatakiwa kufahamu kuwa kila chaguo lako lina matokeo tofauti ikiwemo uwezo wa kudumu na kukidhi mahitaji yako.

  • Bei ya jagi siyo lazima iendane na ubora wa jagi.
  • Angazia litakapotumika, malighafi yaliyolitengeneza na matumizi.
  • Kabla ya kununua, omba ushauri kwa wataalamu.

Dar es Salaam. Kuununua jagi au birika kwa ajili ya kuchemshia maji ni jambo moja lakini kupata kifaa hicho kinachoendana na mahitaji yako ni jambo lingine. 

Inahitaji kuwa na uelewa mpana wa kitu unachokihitaji kabla ya kukinunua kwani badala ya kununua jagi la kukurahisishia maisha, unaweza kujikuta umenunua teknolojia ya kukuongezea gharama au kukupatia hasara.

Uzingatie nini unapoingia kwenye duka lililosheheni majagi ya aina mbalimbali ya kuchemshia maji huku lengo lako ni kutaka kununua jagi moja tu? Elimika kwa dondoo hizi:

Malighafi ya jagi unalonunua

Katika duka la vifaa vya umeme, utakutana na majagi yaliyotengenezwa kwa kioo, shaba (stainless steel) na plastiki. Utachagua lipi?

Unatakiwa kufahamu kuwa kila chaguo lako lina matokeo tofauti.

Fundi wa vifaa vya umeme wa jijini Dar es Salaam ambaye anafahamika kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa jina la @fundi_dsm amesema kwa kawaida majagi yaliyotengenezwa kwa malighafi ya shaba hudumu kwa muda mrefu kuliko ya malighafi mengine.

“Stainless (shaba) zinadumu zaidi kuliko plastic na ghali pia, zinafaa sana kwa matumizi ya ofisini,” amesema @fundi_dsm.

Ni sawa na kusema, majagi ya shaba yanaweza kuhimili vishindo ikiwemo kupasuka pale linapoanguka.

Hata hivyo, majagi haya hushika uchafu wa chumvi endapo yakitumika kwa kipindi kirefu bila kuoshwa.

Majagi ya shaba yanafaa kwa matumizi ya sehemu yenye watu wengi mfano nyumbani na ofisini. Picha| Rodgers George.

Matumizi yake

Kitu ambacho kinatumiwa na watu wengi kinapaswa kuwa imara kwani kila mtu ana namna yake ya kujali mali iliyopo mbele yake.

Wakati mnunuzi anapokuwa anajali mali hiyo, yule ambaye hana uchungu nayo anaweza ona thamani ya kitu hicho sawa na bure.

Mpishi wa keki kutoka Tabata Kinyerezi, Evelyn Oscar amesema kwa eneo la nyumbani ambapo jagi linaweza kutumika na watu wengi, ni vyema kuchukua jagi imara ili lidumu muda mrefu.

“Unakuta mtoto kashika kadondosha, huyu naye kaja kachemsha kaacha kulirudisha alipotoa, inahitaji jagi ambalo litahimiri mikiki mikiki hiyo. Mimi kwa hali hiyo sishauri jagi la kioo na la plastiki siyo sana. La shaba linafaa,” amesema Oscar.

Zingatia pia mahitaji yako

Kutakuwa kuna haja gani kununua jagi dogo wakati una mahitaji makubwa? 

Mfano endapo umenunnua jagi la lita moja katika ofisi yenye watu 10, jagi hilo litachemsha maji kwa mizunguko zaidi ya mitatu kukidhi mahitaji ya chai kwa watu wa ofisi nzima kulingana na saizi ya vikombe wanavyotumia.

Badala yake, jagi la lita mbili au zaidi lingeweza kukidhi mahitaji kwa kuchemsha maji mara mbili tu.

Pia,  kumbuka kadri jagi linavyochemsha maji ndivyo linavyotumia umeme pia. Hivyo katika sehemu ya watu wengi, unashauriwa kununua jagi kubwa ili upunguze matumizi ya umeme.

“Kama una watu wengi ofisini unaweza kuchemsha maji kwa pamoja ili kuoka gharama ya umeme, ila kama ni binafsi, unaweza kutumia ndogo,” ameshauri fundi_dsm.

Majagi ya kuchemshia maji yapo ya aina nyingi ikiwepo plastiki, shaba na kioo. Picha| Don’t Waste Your Money

Gharama ya jagi

Kwa baadhi wanadhani kadri bei ya jagi inavyopaa ndiyo ubora wa jagi hilo unahakikishwa. Mara nyingi ukubwa wa bei ya jagi huendana na gharama za usafirishaji, malighafi yaliyotengeneza jagi hilo na kodi iliyotozwa wakati jagi hilo linaingia nchini.

Ni vyema kufahamu kuwa yapo majagi ambayo huuzwa kwa bei ndogo lakini ni imara kuliko hata yale ya bei kubwa. 

Oscar ameshauri kuongea na wataalamu kupata ushauri kwani unapoenda dukani, siyo wauzaji wote watakupatia maoni ya ukweli. Wengine  wanachojali ni kuuza bidhaa waingize pesa.

“Ninaamini lazima utakuwa na rafiki hata mmoja ambaye ana jagi. Uliza jagi analotumia na uimara wake. Ukishindwa, tafuta mafundi wa bidhaa za umeme watakushauri vizuri bila shida,” amesema Oscar.

Habari za teknolojia ni fahari ya Nukta Habari. Endelea kutufuatilia kwa ajili ya kupata maudhui ya kukuridhisha.