October 6, 2024

Viashiria vya jiko lako la gesi kuhitaji matengenezo

pale unapoona changamoto yoyote katika utendaji kazi wa jiko lako lagesi, unashauriwa kuita fundi ili afanye matengenezo.

  • Ni pale linapoanza kutoa moto wa njano ambao huwachafua masufuria.
  • Dalili nyingine ni uvamizi wa viumbe waharibifu kama panya.
  • Pale jiko lisipofanyiwa marekebisho linaweza kusababisha madhara nyumbani, majeraha na kifo.

Dar es Salaam. Kwa Watanzania baadhi, ni desturi hadi kitu kiharibike kabisa ndiyo wachukue hatua ya kutafuta fundi kwa ajili ya matengenezo.

Wengi hushindwa kuona dalili mbaya wakati wakitumia vifaa vya umeme au kielektroniki ikiwemo kupunguza ufanisi kutoka katika vitu vyao ikiwemo kupunguza ufanisi na kupata matokeo madogo kuliko inavyotarajiwa.

Moja ya vifaa hivyo, ni majiko ya gesi ambayo hutumika kwa shughuli mbalimbali za kupika majumbani ambapo lisipofanyiwa matengenezo kwa wakati linaweza kupunguza uwezo wake wa utendaji. 

Utafahamu vipi kuwa jiko lako linahitaji kupelekwa kwa fundi? Endapo utaona dalili hizi, fahamu kuwa jiko lako linahitaji matengenezo kabla halijafanya: 

Fundi wa vifaa vya umeme wa jijini Dar es Salaam ambaye anafahamika kupitia ukurasa wake katika mtandao wa Instagram wa @fundi_dsm amesema amesema dalili hizo ni pamoja na jiko kupata kutu. Dalili zingine ni:


Uvamizi wa viumbe waharibifu

Huwa unafanya nini baada ya kusikia panya wanasemezana ndani ya jiko lako na kukimbizana pale unapolikaribia? Wengi huwaacha panya hao na kudhani wameondoka. 

Hata hivyo, @fundi_dsm anasema wadudu kama panya ni waharibifu katika majiko kwani wana kawaida ya kuharibu sufi/pamba za ndani ya jiko ambazo hujaza joto kwenye jiko hasa linalotumika kuoka mikate.

Uonapo dalili hii, ni vyema kuanza kukabiliana na panya hao nyumbani kwako na kisha kulifikisha jiko lako kwa fundi kwani uharibifu wa sufi zake hulifanya kutokufanya kazi kwa ufanisi na kutumia muda mrefu kupika na hivyo kuongeza matumizi ya gesi.

Moto wa gesi haupaswi kuwa na rangi yeyote zaidi ya bluu. Ukiona rangi tofauti, ita fundi. Picha| Freepik.

Harufu ya gesi kuvuja

Baadhi huichukulia hali hiyo kama jambo la kawaida na kuendelea na matumizi ya jiko. Lakini hawafahamu kuwa gesi ikivuja inaweza kuleta madhara ikiwemo kulipuka na kusababisha majeraha na kifo.

Mtaalam huyo wa vifaa vya umeme anasema ni muhimu unaposikia harufu ya gesi wakati wa kutumia jiko lako uzime jiko hilo na ukague sehemu ambayo gesi inaweza kuwa inavuja ikiwemo kuangalia kama kuna jiko lingine ambalo haulitumii, huenda limeachwa wazi.

“Unapoingia jikoni, kabla hujawasha jiko kagua knob (viwashio vya jiko) zako zote ziwe zimezimwa, kama ukikuta on, fungua madirisha na mlango wa oven gesi iondoke, washa jiko baada ya masaa mawili kwa usalama wako,” ameshauri fundi huyo.

Kuvuja kwa gesi ni changamoto ambayo inahitaji dharura kuishughulikia kwa sababu isipodhibitiwa madhara yake ni makubwa. Picha| Mtandao.

Jiko kugandiwa na mafuta

Wengi baada ya msosi kuwa tayari, wanaacha jukumu la kusafisha jiko lifanyike kesho yake ambapo mafuta yanakuwa yameganda kwenye jiko na mengine yameingia sehemu yasiyostahili.

Hata katika kufanya usafi, ni wachache huufanya usafi huo kwa umakini.

Daktari wa majiko amesema, mafuta kugandia kwenye jiko ni moja ya kisababishi cha jiko kutoa moto wa njano (ambao una masizi) na pia kuharibu sufuria.

“Usafi ni muhimu jikoni hasa kwenye majiko ya gesi, usiache mafuta yaendelee kuganda, ukimaliza kupika, lisafishe jiko lako,” amesema fundi huyo.

Dalili nyingine ni pamoja na moto kuwa hafifu, moto kulipuka lipuka na kwa majiko yaliyounganishwa na umeme, kutetemeshwa na jiko ukilishika. 

Siyo kwa majiko tu, kwa bidhaa yoyote ya umeme au gesi unayotumia nyumbani, inashauriwa kuikagua mara kwa mara ili kuhakikisha inafanya kazi vizuri na kuepusha madhara makubwa ambayo yanaweza kutokea endapo matumizi yataendelea wakati bidhaa hiyo ina changamoto.