November 24, 2024

Ni maumivu watumiaji wa simu Tanzania

Serikali yapendekeza kila laini kulipiwa Sh10 hadi Sh200 kila siku kulingana na uwezo wa mtumiaji kuongeza salio.

  • Serikali kutoza Sh10 hadi Sh10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa.
  • Serikali inapendekeza kutoza kiasi cha Sh10 hadi Sh200 kwa siku kwa kila laini ya simu kutokana na uwezo.
  • Dk Nchemba amesema mabadiliko hayo yataongeza mapato ya serikali.

Dar es Salaam. Hapana shaka kuwa bajeti ya kwanza ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itapeleleka maumivu kwa watumiaji wa simu Tanzania baada ya kupendekeza tozo katika miamala ya kifedha ya simu na katika matumizi ya kawaida ya vifaa hivyo vya mawasiliano. 

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba ameliambia Bunge Juni 10, 2021 kuwa Serikali imependekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki ikiwemo kutoza tozo ya Sh10 hadi Sh10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa. 

Kwa mujibu wa waziri huyo, kiasi cha tozo kitatofautiana kulingana na thamani ya muamala wa fedha unaotumwa au kutolewa. 

Dk Nchemba amesema pendekezo hilo litaongeza mapato ya Serikali kiasi cha Sh1.254 trilioni.

Maumivu mengine katika mapendekezo hayo ya Dk Nchemba ni kuanza kutoza tozo kwa siku katika laini za simu.  

Katika mapendekezo hayo, Serikali inapendekeza kutoza kiasi cha Sh10 hadi Sh200 kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji. 

“Pendekezo hili litapelekea kuongeza mapato ya Serikali kiasi cha Sh396.3 bilioni,” amesema Dk Nchemba.