November 28, 2024

Sababu za Raha kuangazia wafanyabiashara huduma ya data Tanzania

Kampuni inayotoa huduma ya intaneti nchini Tanzania ya Raha imezindua huduma ya ‘Azure Stack’ ilnayoongeza kiwango usalama mtandaoni.

  • Ni huduma  ya ‘Azure Stack’ inayowezesha kutunza data za biashara katika teknolojia ya “cloud”. 
  • Pia ni njia rahisi ya kusambaza data ukiwa mtandaoni.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara waliokuwa wakihaha kupata jukwaa bora la kutunza kumbukumbu na data za shughuli zao, wameendelea kupata suluhu baada ya Kampuni inayotoa huduma ya intaneti nchini Tanzania ya Raha kuzindua huduma  ya ‘Azure Stack’ ili kuongeza kiwango cha usalama mtandaoni. 

Huduma hiyo inayotolewa kupitia teknolojia ya “cloud” inawezesha biashara mbalimbali kupata jukwaa la kidijitali la kuhifadhi na kusambaza taarifa au data za shughuli zao za kila siku huku wakijihakikishia usalama na usiri wa taarifa zao.

Jukwaa hilo huenda likawafaa zaidi vijana wanaomiliki kampuni na biashara zinazochipukia kupata eneo sahihi kutunza data kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa shughuli zao na huduma wanazotoa kwenye jamii. 

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Raha Limited nchini Tanzania, Reuben Lucas amesema kuzinduliwa kwa huduma hiyo ni kukidhi ukuaji wa mahitaji ya biashara kutafuta majukwaa salama ya mtandaoni ambako wanaweza kuhifadhi data zao.

Amesema kwa sasa, kampuni nyingi zinaendesha shughuli zao mtandaoni na uanzishwaji wa mifumo thabiti ya kidijitali ni muhimu kuwahakikisha biashara hizo zinakuwa endelevu na zinachangia katika maendeleo ya Taifa. 

“Usambazaji wa huduma hii ya ‘Azure Stack’ nchini ni hatua nyingine kubwa tuliyoifanikisha huku tukiendelea kusaidia kuhamasisha maendeleo thabiti ya kiuchumi na kiteknolojia tunayoyaona kuwahi kutokea Tanzania hapo awali,” amesema Lucas katika uzinduzi wa huduma hiyo uliofanyika Mei 20 jijini Dar es Salaam.


Zinazohusiana


Ili kupata huduma hiyo ambayo kwa sasa inapatikana katika miji 60  duniani, mteja anatakiwa kuwasilisha taarifa na kulipia kulingana na mahitaji yake na kisha utaunganishwa bila kuhitaji kuweka miundombinu katika biashara yake.

Huduma hiyo haiitaji mfanyabiashara kununua vifaa vya kuhifadhia data kama kanzidata (servers) na huduma zinazohusiana jambo linalopunguza matumizi katika kampuni hasa zinazochipukia.

Pia inapunguza changamoto ya usafirishaji wa data na inawezesha shughuli za kibiashara kuendelea kufanyika kwa ufanisi kutokana na mifumo iliyowezeshwa kuendana na mabadiliko ya kimazingira.

“Sasa, wateja wetu katika ukanda wote wa Afrika ya Mashariki wana uhakika wa mazingira salama na ya kuaminika kwenye shughuli zao za Tehama muda wowote,”-  amesema Afisa Mtendaji Mkuu wa Liquid Telecom, ambayo ni kampuni mama ya Raha Limited,  Adil El Youssefi.

Raha inahudumia biashara zaidi ya 1,500 kwa kuwaunganisha na huduma ya intaneti ili kurahisisha utendaji wa shughuli zao nchini.