Mambo ya kuzingatia unapotumia mashine ya kutolea maji nyumbani
Inashauriwa kuikagua mashine yako mara mbili kwa mwaka na kuiacha ikiwa safi wakati wote.
- Inashauriwa kuikagua mashine yako mara mbili kwa mwaka.
- Kuisafisha mashine yako kutakuepusha na matatizo ya kiafya.
- Pia kutasaidia kuepuka gharama za kununua mashine mpaya kila mara.
Dar es Salaam. Kutokana na mazowea au imani yetu juu ya teknolojia za nyumbani, baadhi husahau kuwa mashine zinazotumika myumbani ikiwemo blenda, mshaine ya kutolea maji na nyinginezo zinahitaji kuhudumiwa ili ziendelee kufanya kazi kwa ufanisi.
Kwa mashine ya kutolea maji ya kunywa almaarufu kama “water dispenser”, baadhi hudhani kuwa kuharibika kwake ndiyo sababu pekee ya kufanya mashine hiyo ikutane na fundi.
Hata hivyo, mashine hiyo inahitaji kutunzwa, kusafishwa mara kwa mara kwa kuondoa vumbi na uchafu mwingine ili ifanye kazi kama inavyotakiwa.
Umuhimu wa kuisafisha mashine ya maji
Mbali na kuisafisha mashine ya maji kwa nje, mashine hiyo inahitaji kufanyiwa usafi wa kina kwa ajili ya kuondoa uchafu ambao haufikiki kwa kitambaa.
Fundi wa vifaa vya umeme wa jijini Dar es Salaam ambaye hakupenda jina lake litajwe anasema mashine ya maji inatakiwa kukaguliwa walau mara mbili kwa mwaka kulingana na maelezo ya watengenezaji.
Fundi huyo ambaye anatumia akaunti ya Instagram ya @fundi_dsm amesema kuna umuhimu wa kuisafisha na kuikagua mashine yako ili kuepuka madhara ya kiafya ambayo unayoweza kupata ikiwa mashine itakuwa chafu.
Amesema unaweza kugundua kama mashine ya maji inahitaji ukaguzi endapo utaanza kusikia harufu isiyo ya kawaida unapokunywa maji yaliyotoka katika mashine hiyo huku muda mwingine yakiwa na uchafu.
Soma zaidi:
- Usifanye makosa haya wakati wa kununua “blender”
- Unataka kusafiri nje ya nchi? Jiweke tayari kwa mambo haya
- Teknolojia inavyosaidia kupunguza athari za mafuta mwilini
Mbali na kupata maji machafu kutokana na ukungu unaoweza kuwepo ndani ya mashine, kutokuisaifisha mashine yako ya maji inaweza kuwa sababu ya kutunza wadudu wasiohitajika hasa katika mashine ya maji.
“Changamoto tuliona mara nyingi ni wadudu kama sisimizi, nyuki, mjusi, buibui na kadhalika. Pia panya huwa wanakula mabomba kama dispenser inaachwa kwa kipindi bila kutumika,” amesema fundi huyo.
Amesema hiyo inaweza kuifanya mashine kuharibika mapema au kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Pia inaweza kukuongezea gharama za kununua mashine mpya mara kwa mara, jambo ambalo linaweza kukuharibia bajeti yako.
Mtaalam huyo wa vifaa vya umeme, amesema kabla ya kuisafisha mashine ni muhimu kupata ushauri kwa wataalam wa mashine hizo ili wakushauri njia na vifaa maalum vinavyotumika kuisafisha.