November 28, 2024

Rais Samia atoa onyo kali kwa wanaofanya uchonganishi mtandaoni

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya uchanganishi na kutoa taarifa zisizo za kweli na kuwa Serikali haitawafumbia macho.

  • Awataka waache kutoa taarifa zisizo za kweli.
  • Asema Serikali haitafumbia macho na itawafuta.
  • Ni pamoja na waliozusha kuhusu Hayati Rais Magufuli kupewa sumu. 

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya uchanganishi na kutoa taarifa zisizo za kweli na kuwa Serikali haitawafumbia macho.

Rais Samia amelieleza Bunge leo Aprili 22, 2021 jijini Dodoma kuwa amekuwa akiona taarifa mbalimbali mtandaoni ukiwemo uzushi juu ya kifo cha Hayati Rais John Magufuli kuwa alilishwa sumu, jambo ambalo siyo la kweli.

“Nimekuwa nikiona kwenye mitandao taarifa za uchonganishi, taarifa tuliyopewa na madaktari wetu ya kifo cha mpendwa wetu (Hayati Magufuli) ni kutokana tatizo la udhaifu wa moyo ambalo ameishi nalo kwa takriban miaka 10,” amesema Rais Samia. 

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema kama kuna mtu ana taarifa sahihi juu ya kifo cha Magufuli aende Serikali itamsikiliza na kufanya upepelezi wa kina kuhusu kifo hicho. 

“Kama wana taarifa za maana waje tuwasikilize, vyombo vya upepelezi vipo. ‘Short of that’ (kinyume na hapo) wasisimame kuleta uchonganishi ndani ya nchi. Taarifa wanazozitoa ni za kugonganisha, koo na koo, makabila na makabila, hivyo waache kuleta uchonganishi ndani ya nchi,” amesisitiza. 


Soma zaidi:


Amesema licha ya kuziona taarifa hizo, Serikali inawatafuta watu hao ambao wanaeneza uchonganishi hata kama bado haina uwezo wa kuwapata kutokana na matumizi ya mifumo ya kisasa ya teknolojia wanayotumia. 

Aidha, amewataka wanaozusha mtandaoni juu ya masuala mbalimbali wajiulize kama wanayofanya yana uhalali au yana maana mbele za Mungu.

Tangu kufariki dunia kwa Rais Magufuli Machi 17, 2021 mwaka huu, kumekuwepo na taarifa mbalimbali zikitoa sababu mbalimbali za kifo chake, jambo ambalo limekuwa likizua mijadala na taharuki kwenye jamii.