October 6, 2024

Majaliwa amsimamisha kazi kigogo mabasi yaendayo haraka Dar

Ni Mkurugenzi wa Fedha wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Suzana Chaula baada ya kutoridhishwa na utendaji wake ikiwemo kutokutumia mashine za kielektroniki kukata tiketi.

  • Ni Mkurugenzi wa Fedha, Suzana Chaula.
  • Ni baada ya kutoridhishwa na utendaji wake ikiwemo kutokutumia mashine za kielektroniki kukata tiketi. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Suzana Chaula baada ya kutoridhishwa na utendaji wake ikiwemo kutokutumia mashine za kielektroniki kukusanya mapato ya tiketi za mabasi. 

 Majaliwa amechukua hatua hiyo leo Aprili 19, 2021 alipotembelea kituo cha kikuu cha DART-Gerezani ambapo alionyesha kutoridhishwa na utendaji wa mradi huo hasa katika eneo la ukusanyaji wa mapato. 

 “Haiwezekani watu wanafanya ujanja ujanja tu wanakuja na tiketi zao za mfukoni halafu wakimaliza anauza za POS (Mashine ya Kielektroniki ya Kukusanyia Mapato) na wasimamizi wapo tu Mkurugenzi wa Fedha yupo tu ameshindwa kusimamia hili na lipo mikononi mwake,” amesema Majaliwa. 

 Majaliwa amesema wafanyakazi wa DART wanauza tiketi kwa vifurushi na hawatumii mashine, jambo linalotoa mwanya kwa baadhi ya watu kuuza tiketi zao.

 “Kwa nini ukatishaji wa tiketi haufanyiki kwa njia ya kielektroniki kwa asilimia 100? Tiketi zinauzwa kwa vifurushi,” amesema Majaliwa. 

 Kutokana na dosari hiyo, mtendaji mkuu huyo wa Serikali amemsimamisha kazi Chaula kwa kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato wa mradi huo.

 Mabasi ya DART yamekuwa msaada kwa watu wengi wanaoingia na kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam kwa sababu yanasaidia kupunguza foleni na kuokoa muda ambao watu wanatumia barabarani.


Zinazohusiana


Uchakavu wa magari

 Pia Majaliwa ameshangazwa na kupungua kwa mabasi ya mradi huo kutoka 140 hadi 85 na hakuna jitihada zozote za kuongeza mabasi mengine ili kuwapunguzia wananchi adha ya usafiri.

 “Tangu Mtendaji Mkuu ameingia DART (Mhandisi Ronald Rwakatare) ana miaka mitano hakuna hata basi moja alilonunua, na anasema hana fedha kwani abiria hawasafiri si kila siku wanapigania kule Kimara na wote wanalipa unasemaje hakuna fedha ya kununulia magari?” amehoji Majaliwa. 

Amesema wakala huo ulianzishwa na Serikali kwa ajili ya kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi lakini viongozi hao wameshindwa kusimamia vizuri na hivyo kusababisha mradi huo kutoendelea vizuri.

 Aidha, Waziri Mkuu ametembelea karakana ya UDART ya Kurasini na ameshuhudia baadhi ya mabasi ya wakala huo yakiwa mabovu huku mengine yakiwa yameondolewa vipuri.