Tutegemee nini ujio wa simu mpya za Sony Aprili 14?
Baada ya chaji na kamera kupigwa vikumbo na wababe wa sasa akiwemo Samsung na iPhone, Sony imejizatiti upya.
- Baada ya chaji na kamera kupigwa vikumbo na wababe wa sasa akiwemo Samsung na iPhone, Sony imejizatiti upya.
- Simu hiyo ambayo bado haijapewa jina inatajwa kuwa na kasi na uwezo mkubwa.
- Simu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Aprili 14 mwaka huu.
Dar es Salaam. Kwa baadhi ya kampuni za kutengeneza simu, kila mwaka ni nafasi nyingine kwao kuingiza bidhaa mpya sokoni ili kuendelea kuwepo katika soko la ushindani.
Samsung wameshaingiza sokoni toleo la 21 la simu za Samsung Galaxy, One Plus wameingiza sokoni toleo la tisa na kwa sasa, tunategemea Experia mpya kutoka Sony.
Nini kipo sokoni kwa sasa?
Hadi sasa, toleo la Sony ni simu ya Sony Xperia 5 II ambayo iliingia sokoni Septemba mwaka jana ikiwa na kamera ya nyuma yenye MegaPixel (MP) 12 sawa na Samsung Galaxy S20 ambayo nayo iliingia sokoni mwaka huo.
Hata hivyo, kwa kamera ya mbele Sony ina uwezo wa MP 8 kitu ambacho kwa mwaka 2020 ilipigwa bao na Samsung ambayo kamera yake ya mbele ina uwezo wa MP32.
Kupigwa bao na Samsung kulienda mbali zaidi baada ya kuwa na betri lenye uwezo wa mAh 4000 huku Samsung ikiwa na mAh 4500, na hivyo kuifanya Samsung kukaa na chaji kwa muda mrefu zaidi.
Sony ya mwaka jana huenda iliwavutia watu ambao wanaopendelea uhifadhi mkubwa wa vitu. Sony hiyo ina uwezo wa GB128 za uhifadhi, sawa na Samsung. Tofauti kati ya simu hizo, Sony ina sehemu ya kuweka kadi ya kumbukumbu huku Samsung ikiwa haina.
Uzinduzi huo utafanyika kwa njia ya mtandao kupitia chaneli ya YouTube ya Sony Aprili 14 kuanzia saa 4:30 asubuhi. Picha| Sony
Tunachokijua kuhusu simu ijayo kutoka Sony
Hivi karibuni Sony imetangaza kuingiza simu mpya sokoni ifikapo Aprili 14 na tayari fununu za muonekano, jina na hata sifa za simu zijazo zimeshaingia katika masikio ya wadau wa teknolojia.
Wadau ikiwemo taasisi ya The Verge, Tech Radar na wengineo wanasema, endapo Sony itaingiza simu hiyo sokoni, itashindana na wababe katika soko la simu janja akiwemo OnePlus na Samsung Galaxy S 21 ambao kamera zao ni moto wa kuotea mbali.
Tech Radar imeandika, “Sony inaingiza simu iitwayo Sony Experia 1iii ambayo kamera yake inatumia teknolojia ya “periscope zoom” ambayo sifa yake kuu ni kupiga picha zilizo na ubora mara tano au zaidi ikilinganishwa na kamera zilizopo kwenye simu janja kwa sasa.
Xperia 1iii inakuja na kamera ya nyuma yenye uwezo wa MP64 zaidi ya mara tano ya uwezo wa iPhone 12 Pro Max ambayo kamera yake ina uwezo wa MP12 sawa na toleo la awali la Sony Experia 1ii.
Hata hivyo, Sony kufua dafu kwa Samsung ni kibarua kikubwa kwani Samsung iliyopo sokoni ina kamera yenye uwezo wa MP108.
Soma zaidi:
- Nyeusi, nyeupe: Yanayofahamika kuhusu OnePlus 9, OnePlus 9 Pro
- OnePlus: Simu yenye mapinduzi ya kamera kuwekwa hadharani leo
- Kijana anayetikisa mitandao ya kijamii kwa utamaduni wa Kimasai
Uwezo wake wa betri siyo mchezo
Kama tetesi hizi ni za kweli, huenda Sony imefanyia kazi changamoto ya simu zake kutumika kwa muda mfupi baada ya toleo lililopita kuwa na betri la mAh4000.
Experia 1iii inatarajiwa kuwa na betri lenye uwezo wa mAh 5000 ambalo linakadiliwa kuwa na uwezo kutumika hadi siku mbili ikiwa simu imechajiwa vizuri.
Tovuti ya Droid Life imesema, simu mpya ya Sony inaweza kuwa na uhifadhi wa ndani (RAM) wa GB12 huku uhifadhi wa kawaida ukiwa ni GB256. Hilo linaashiria kasi kubwa ya kufanya vitu katika simu hiyo hata kucheza michezo ya kidijitali.
Yapo mengi yanayosemekana kuja na simu ya Sony Experia 1iii. Kufahamu zaidi na hata kutazama tukio hilo mubashara, usisite kutembelea Nukta Habari ifikapo Aprili 14, siku ya uzinduzi.