WhatsApp kuzima mawasiliano kwa wasiokubaliana na sera mpya
Ni sera mpya ya faragha ambayo kwa sehemu itashirikisha taarifa zao binafsi na mtandao wa Facebook.
- Ni sera mpya ya faragha ambayo imepokewa kwa hisia tofauti.
- Zoezi hilo litafanyika ifikapo Mei 15 mwaka huu.
Watumiaji wa WhatsApp ambao hawatakubali kanuni na masharti mapya ya mtandao huo ifikapo Mei 15 mwaka huu hawataweza kupokea wala kutuma ujumbe katika mtandao huo mpaka wakubaliane utaratibu huo.
Kwa ambao hawatakubaliana na matakwa hayo, akaunti zao zitawekwa katika orodha maalum ya akaunti zisizofanya kazi (inactive) na akaunti hizo zisipohuishwa zinaweza kufutwa baada ya siku 120.
Mapema January mwaka huu, jukwaa hilo la mawasiliano ya ujumbe mfupi liliwatangazia watumiaji wake kuwa linaanda sera mpya ya faragha ambayo kwa sehemu itashirikisha taarifa zao binafsi na mtandao wa Facebook na makundi mengine inayoyasimamia.
Tangazo hilo liliibua mjadala mpana duniani huku baadhi ya watumiaji wakiamia Telegram na Signal ili kulinda taarifa zao.
Soma zaidi:
- Uunganishwaji wa WhatsApp, Facebok bado sana
- WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania
- Wadau mtandaoni watoa neno WhatsApp kudhibiti habari za uongo
Kutokana na suala hilo, WhatsApp ilisogeza mbele uzinduzi wa sera hiyo hadi Mei badala ya tarehe ya awali ya Februari ili kutoa fursa ya kuwaelimisha watumiaji wake juu ya mabadiliko hayo mapya.
Duru za kimataifa zinaeleza kuwa WhatsApp itaendelea na mpango wake licha ya maoni tofauti kutoka kwa watumiaji wake.
Uongozi wa mtandao huo umeeleza mara kadhaa kuwa sera hiyo mpya ina nia njema wala haikusudii kuweka wazi taarifa watumiaji wake.