November 24, 2024

Jinsi ya kununua chaja bora ya simu yako

Ni pamoja na kufahamu uwezo wa chaja hiyo kupokea na kuchaji simu yako.

  • Ni pamoja na uwezo wa chaja hiyo kupokea na kuchaji simu yako.
  • Fahamu pia aina ya chanja unayonunua kama inaweza kufanya kazi kwenye simu yako ili usiishie kununua pambo.
  • Endapo utainunua mtandaoni, hakikisha muuzaji huyo amethibitishwa na atakuuzia chaja halisi.

Dar es Salaam. Huenda katika kila pochi ya mwanadada na begi la mtu yoyote haikosekani chaja ya simu kwani kifaa hicho ni sehemu ya uhai wa mawasiliano ya wengi.

Kizungumkuti huanza baada ya chaja kupotea au kuharibika na kukulazimu kununua nyingine ili kuendelea kuwa hewani. 

Hapo ndipo changamoto mbalimbali huibuka ikiwemo chaja mpya kukosa ufanisi unaohitajika, kutumia muda mrefu kuichaji simu na wakati mwingine kuharibika mapema kuliko ilivyokusudiwa.

Zipo chaja zifaazo kuchajia simu kwenye gari, za kuchaji simu haraka na zile zisizo na waya. Picha| Rodgers George.

Uzingatie nini ili usiingie mkenge unaponunua chaja kwa ajili ya simu yako?

Kagua uwezo wa kupokea umeme 

Kwa kimombo inaitwa “Input Voltage Rating” na hii hutofautiana kutoka nchi moja kwenda nyingine. Mfano kwa nchi ya Marekani, umeme wake ni wa voti 120 hivyo huenda ukipata chaja iliyo na uwezo chini ya hapo isiwe ya manufaa kwako.

Zipo chaja zinazopokea umeme kuanzia voti 100 hadi 240 na zingine zinazopokea voti 240 pekee.

Licha ya kuwa chaja nyingi zilizopo sokoni (Tanzania) zina uwezo wa kupokea umeme wa voti  240, huenda ukahitaji kuthibitisha hilo hasa kama unaagizia chaja kwa njia  ya mtandao kutoka nchi nyingine.

Hiyo inamaanisha kuwa pale uwezo wa umeme utakapopungua chini ya voti 240, chaja hiyo huenda isipokee umeme au ikachaji simu yako taratibu.

Ili kuwa na uhakika wa kuchaji simu yako katika mazingira yoyote ya umeme, unashauriwa kununua chaja inayoweza kupokea umeme kuanzia voti 100 hadi 240 na itakuwa rahisi kuitumia utakaposafiri kwenda nchi yeyote ikiwemo India na Marekani.

Unaweza kutumia App ya Google lens kuskani chaja kabla ya kuinunua, itakusaidia kung’amua kama chaja hiyo ni halisi kwa kutambua baadhi ya sifa za chaja hiyo kama zinaendana chaja halisi pamoja na kutafsiri lugha iliyotumika katika chaja hiyo endapo hauielewi.


Uwezo wa chaja kuchaji simu

Kila simu inakuja na uwezo tofauti wa betri na hivyo kuhitaji chaja ambayo inafaa kuchaji betri hilo. Mfano, endapo utachagua chaja ambayo uwezo wake wa kuchaji betri ni mdogo, simu yako itachukua muda mrefu kujaa.

Inashauriwa uchague chaja inayoendana na uwezo wa simu yako ili kutokuumiza betri la simu yako.

Mathalan, ukichagua chaja iliyo na uwezo wa voti 5 (5V-”Amps”2A), una uhakika wa simu yako kuchaji na kujaa ndani ya muda mfupi kutokana na uwezo mkubwa wa chaja hiyo tofauti na utakapochagua chaja yenye uwezo wa A 5V-1A ambao ni uwezo mdogo.

Fahamu kuwa, Amps ni kiasi cha umeme kinachoingia kwenye simu wakati inachajiwa.

Ili kuepuka kuuziwa chaja feki kwa bei ya chaja orijino, hakikisha unatembelea duka linalouza vitu bora. Picha| Rodgers George.

Usiagize mtandaoni endapo hauna uhakika na muuzaji

Kama unatumia simu ya Samsung, unaweza kuagiza moja kwa moja kutoka duka la Samsung, vivyo hivyo kwa Iphone na simu zingine.  Lakini kwa wauzaji wengine wa mtandaoni huenda ikakuwia vigumu kuwa na uhakika wa ubora na uthabiti wa chaja hiyo.

Pia, itakuwa ni ngumu kwako kuirudisha, kubadilisha na hata kuwa na uhakika kupata chaja halisi kwa ajili ya simu yako.

Mbali na hilo, huenda ikachukua muda mrefu kukufikia au zaidi ukadhulumiwa na pesa yako ikaenda bure.

Hata hivyo, mbali na chaja zilizotengenezwa na kampuni za kutengeneza simu, zipo chaja ambazo zimetengenezwa na wadau wengine ambazo pia zipo vizuri. Inashauriwa kuuliza wataalamu na kufanya utafiti kubaini chaja ipi inafaa.


Fahamu aina ya chaja unayonunua

Kwa sasa kuna chaja ambayo inafaa kutumia katika kila eneo. Zipo chaja zifaazo kuchajia simu kwenye gari, za kuchaji simu haraka na zile zisizo na waya.

Kabla ya kununua chaja hizo, hakikisha unafahamu kuwa simu yako ina uwezo wa kuchajiwa na chaja hiyo. Mfano, siyo simu zote zinaweza kuchajiwa kwa chaja za kujaza simu haraka almaarufu kama “fast chargers” ambazo huenda zikaharibu betri la simu  yako.

Pia, unaweza kuvutiwa na kununua chaja isiyo na waya (wireless) wakati simu yako haikubaliani na aina hiyo ya chaja.


Soma zaidi:


Hakikisha thamani ya chaja na bei

Siku hizi kuna kitu kinaitwa “kuingizwa mjini” au “kupigwa” sio kila duka linauza vitu halisi. Hivyo huenda ukaishia kuwa mhanga kwa kuuziwa kiti cha bei ya juu lakini kikakosa ubora.

Ili kuepuka kuuziwa chaja feki kwa bei ya chaja orijino, hakikisha unatembelea duka linalouza vitu bora. 

Usitumie kichwa cha chaja ya simu ya Techno katika simu ya Samsung au iPhone bila kufahamu uwezo wa kichwa hicho cha chaja.

Kupitia makala hii, huenda umejifunza kitu. Endapo utakuwa na maoni yoyote, usisite kutuandikia kupitia mitandao ya kijamii kupitia @NuktaTanzania.

Makala hii imefanyiwa uthibitishaji na Wahandisi wa masuala ya mawasiliano, Erick Maleza na Gadson Mang’ana.