November 24, 2024

Sababu za akaunti ya Trump kufungwa rasmi

Twitter yasema amekiuka sera na sheria za mtandao huo kwa kuchochea vurugu.

  • Anadaiwa kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani.
  • Twitter yasema amekiuka sera na sheria za mtandao huo.

Dar es Salaam. Akaunti ya Twitter ya Rais wa Marekani anayeondoka madarakani Donald Trump amefungiwa rasmi baada ya mtandao huo kusema kuna hatari ya rais huyo kuendelea kuchochea vurugu zaidi. 

Hatua hiyo inafuatiwa Trump kufungiwa akaunti yake ya Twitter (@realDonaldTrump) kwa saa 12 Jumatano Januari 6 mwaka huu baada ya kutoa wito kwa wafuasi wake kuvamia  bunge la nchi hiyo lijulikanalo kama Capitol Hill jijini Washington,D.C. 

Twitter katika taarifa yake iliyotolewa Januari 8 imesema imefikia uamuzi huo baada ya kufuatilia mwenendo usioridhisha wa matamko ya Trump katika mtandao huo na ikiachiwa ataendelea kuleta madhara zaidi.

“Tumefunga kabisa akaunti yake kwa sababu inaweza kutumika kuchochea vurugu zaidi,” imesema Twitter katika taarifa yake.

Mtandao huo umesema baadhi ya jumbe ambazo amekuwa akiweka Trump zinakiuka sera na sheria za Twitter kwa sababu zinahamasisha vurugu na uvunjifu wa amani duniani. 

Moja ya ujumbe alioandika rais huyo Twitter unasema “Kwa wote ambao wameuliza, sitahudhuria hafla ya kuapishwa Januari 20.” akimaanisha kuwa hatahudhuria sherehe za kumuapisha Rais mteule Joe Biden. 

Hata hivyo, Twitter umesema kuwa ujumbe huo “umechukuliwa na wafuasi wake kuwa uchaguzi uliompa ushundi Biden kama uthibitisho kuwa haukuwa halali.”


Soma zaidi: 


Mapema Alhamis 7 Januari 2021, bunge la uwakilishi la Marekani lilimthibitisha Biden na Harris kuwa rais na makamu wa rais ajaye baada ya kuridhia kura za wajumbe 306, wengi zaidi ya 270 wanaohitajika. 

Viongozi hao wanatarajia kutwaa madaraka Januari 20, 2020.

Mbali na Twitter, kampuni ya Facebook nayo imezuia Trump kuchapisha chochote katika mitandao yake ya Facebook na Instagram.