October 7, 2024

Startups nane za Tanzania kuchuana kuingia shindano la dunia la Seedstars

Shindano hilo ni mahususi kwa startups zinazotatua changamoto za jamii kwa kutumia teknolojia rahisi.

  • Shindano hilo ni mahususi kwa startups zinazotatua changamoto za jamii kwa kutumia teknolojia rahisi.
  • Startup itakayochaguliwa itaiwakilisha Tanzania katika shindano la Afrika na dunia. 
  • Mshindi wa dunia atakayepatikana atapata mtaji wa Sh1.2 bilioni.

Dar es Salaam. Ni mpambano mwingine wa kampuni nane za teknolojia zinazochipukia (Startups) ikiwemo ya ElimuTube zinazoingia uwanjani ili kupata kampuni moja itakayoiwakilisha Tanzania katika shindano la dunia la Seedstars litakalotoa fursa ya kupambania mtaji wa Dola za Marekani 500,000. 

Licha ya kuwa mshindi wa jumla atapewa kiasi hicho ambacho ni sawa na Sh1.2 bilioni, pia atanufaika na fursa zingine za mafunzo ya uendeshaji kampuni za teknolojia na kukutanishwa na wawekezaji. 

Shindano hilo linalofanyika kila mwaka linaloendeshwa na kampuni ya Seedstars yenye matawi mbalimbali duniani ni mahususi kwa startups zinazotatua changamoto za jamii kwa kutumia teknolojia rahisi katika kutoa huduma na bidhaa.

Mpambano huo utafanyika Novemba 14, 2020 jijini Dar es Salaam kabla ya mshindi mmoja kuchaguliwa na majaji baada ya kupitia suluhu zinazotolewa na startups hizo.


Soma Zaidi


Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo Novemba 12, 2020 imezitaja starups ambazo zitashiriki mpambano huo kuwa ni AfyaTest MedTech Company, Code Developers Tanzania, Denistle na Dundiza Technologies.

Zingine ni ElimuTube, Flamingo Foods, Fundi App na Locofin.

“Tuna matarajio ya kumuona mshindi wa Seedstars Dar es Salaam 2020 baada ya kupokea zaidi ya maombi 30 kutoka kwa startups mbalimbali,” amesema Meneja wa Hafla na Jamii wa Seedstars kanda ya Afrika, Lorraine Davis.

Ili startup itakayochaguliwa kesho ipate fursa ya kushiriki shindano hilo la dunia, itakuwa na kibarua kingine cha kuchuana na startups zingine za Afrika ambazo zinapigania kuwa miongoni mwa kampuni tano zitakazoliwakilisha bara hilo katika shindano la dunia. 

Tofauti na miaka iliyopita, shindano la mwaka huu litafanyika kwa njia ya mtandao ikiwa ni hatua ya kukabiliana na athari za janga la Corona ambalo limeleta changamoto ya watu kutokukusanyika pamoja. 

Nani katoboa?

Tazama video hii kuziona startups hizo nane na kazi zinazofanya

Mwaka uliopita wa 2019, Tanzania iliwakilishwa na app ya Sheria Kiganjani ambayo inatoa msaada wa kisheria kwa njia ya mtandao.

Pambano hilo litakalofanyika kesho limeandaliwa na Seedstars Dar es Salaam kwa kushirikiana  na Kituo cha Kimataifa cha Biashara (ITC) pamoja na Mpango wa Ufuatiliaji wa Teknolojia na Biashara (Fast Track Tech innitiative).

Mashindano haya yanafanyika kwa mara ya sita huku mwaka jana (2019) Tanzania ilizikutanisha startups 10 zikiwemo nne kutoka Zanzimbar na kinyang’antiro hicho kunyakuliwa na taasisi ya Sheria Kiganjani inayotoa suluhu ya masuala ya kisheria kidijitali.

Je, ni nani atatoboa mwaka huu? Usikae mbali na Nukta Habari.