Vodacom yaibuka na mfumo mpya wa kidigitali
Ni mfumo unarahisisha utoaji huduma za kampuni hiyo ya simu ikiwemo M-Pesa.
- Ni mfumo unarahisisha utoaji huduma za kampuni hiyo ya simu ikiwemo M-Pesa.
- Unaweza kuunganishwa na programu mbalimbali kuwasaidia wananchi kufanya biashara kwa urahisi.
- Wabunifu watakiwa kutoa mazao yatakayoboresha zaidi mfumo huo.
Dar Es Salaam. Wateja wa kampuni ya Vodacom Tanzania, sasa wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kampuni hiyo kuzindua mfumo wa kidijitali unaorahisisha utoaji wa huduma zake ikiwemo ya M-Pesa.
Mfumo huo mpya wa kiteknolojia (Application Programing Interface) unajumuisha programu za simu (Apps) za M-Pesa na “My Vodacom App” ambazo zinawawezesha watumiaji wa simu janja kupata huduma kwa urahisi na haraka.
Mfumo huo (Application Programing Interface-API) pia unawezesha uunganishaji wa mifumo ya malipo katika mfumo wa huduma za kifedha wa M-Pesa uwe rahisi, wa haraka na wenye ufanisi zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Hisham Hendi aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo Oktoba 1, 2020 jijini Dar es Salaam amesema lengo ni kuunga mkono ubunifu wa mifumo ya kidigitali inayorahisisha utoaji huduma na kuwaletea maendeleo wananchi na Taifa.
“Tunaunga mkono ubunifu wa mifumo ya kidigitali itakayo badilisha maisha ya watu, na ndiyo maana sasa tumefungulia API za M-Pesa ili kurahisisha biashara zenu na watengenezaji wa programu kuunganisha mifumo mingine na mfumo wa M-Pesa,” amesema Hendi.
Mfumo huo unaweza kuunganisha huduma zaidi ya moja, jambo linatoa fursa kwa wabunifu kubuni apps zitakazorahisisha utoaji wa huduma hasa za malipo kwa njia ya simu.
Zinazohusiana:
- Vodacom kuingiza sokoni mashine za kidigitali za kuuzia vinywaji, vitafunio
- Vodacom yazindua teknolojia kudhibiti upotevu data za wateja
Mkurugenzi wa Vodacom M-pesa, Epimack Mbeteni amesema API mpya iliyozinduliwa leo inaongeza ufanisi na kurahisisha uunganishaji wa mifumo ya malipo katika mfumo wa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi wa M-pesa.
Mbeteni amewataka wabunifu wa programu za simu na kompyuta kubuni programu zitakazofanya kazi pamoja na mfumo wa Vodacom ili kutoa huduma zilizo bora kwa wateja wao.
“Tunatumaini kwamba tutaona mawazo mengi mapya, programu na biashara mbalimbali zikiunganishwa na mfumo wetu mkubwa kwa ajili ya kutoa huduma zilizoboreshwa zaidi kwa wateja.” amesema Mbeteni.