October 7, 2024

Sababu ndege za Kenya kuruhusiwa kutua Tanzania

Ni baada ya Kenya kuondoa sharti la raia wa Tanzania kukaa karantini kwa siku 14 wanapoingia nchini humo.

  • Ni baada ya Kenya kuondoa sharti la raia wa Tanzania kukaa karantini kwa siku 14 wanapoingia nchini humo.
  • Sasa wasafiri wa nchi hizo mbili wako huru kutumia ndege za Kenya. 

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni kicheko kwa wasafiri wanaotumia mashirika ya ndege ya nchini Kenya likiwemo la Kenya Airways, baada ya Serikali ya Tanzania kuruhusu ndege za nchini hiyo kutua nchini. 

Hatua hiyo imekuja baada ya Kenya kuondoa sharti la raia wa Tanzania kukaa karantini kwa siku 14 wanapoingia nchini humo ambalo lilikuwa limekwa awali ili kujikinga na Corona.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Johari Hamza katika taarifa yake iliyotolewa leo (Septemba 16, 2020) amesema kutokana na kulegezwa kwa masharti hayo, ndege za Kenya zinaruhusiwa kutua tena nchini.

Johari amesema ndege zote za mashirika ya Kenya za Kenya Airways, Fly 540 Limited, SafariLink Aviation na AirKenya Express Limited zinaweza kutua katika viwanja vya ndege vya Tanzania kwa muda wote.

Amesema tayari wameitaarifu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya kuhusu kuruhusiwa kwa ndege hizo.


Soma zaidi:


Julai 31 mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilibatilisha kibali cha ndege za Shirika la ndege la Kenya (Kenya Airways) kutua nchini ikiwa ni majibu dhidi ya uamuzi wa Serikali ya Kenya kutoiweka Tanzania katika orodha ya nchi ambazo raia wake wangeruhusiwa kuingia Kenya kuanzia Agusti mos bila kukaa karantini. 

Hata hivyo, jana Septemba 15, Kenya imeondoa sharti la Watanzania kukaa karantini siku 14 kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini humo. 

Muda mfupi baada ya anga la Tanzania kufunguliwa kwa ndege za Kenya, shirika la ndege la Kenya Airways limesema litaanza safari zake za kwenda jijini Dar es Salaam kuanzia Jumatatu Septemba 21. 

“Ndege yetu ya kwanza kwenda Dar es Salaam itakuwa Jumatatu Septemba 21, ambapo tutakuwa na safari ya asubuhi na safari  ya pili itakuwa Septemba 23. Safari za kwenda Zanzibar zitarejea Septemba 26 kwa safari tatu kwa wiki; Jumatatu, Jumatano na Jumamosi,” imeeleza Kenya Airways katika taarifa yake iliyotolewa leo.

Hiyo siyo mara ya kwa nchi hizo mbili kuingia katika mivutano ya kibiashara, licha ya kuwa zimekuwa zikitegemeana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. 

Kenya inawakilisha asilimia 4.3 ya mauzo yote ya nje ya Tanzania na asilimia 4.1 ya manunuzi yote ya Tanzania kutoka nje ya nchi. 

Inaelezwa kuwa zaidi ya kampuni 529 za Kenya zinaendesha biashara zake nchini Tanzania na zimewekeza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 1.7 (takriban Sh39.5 trilioni) na kutengeneza ajira kwa Watanzania zaidi ya 56,260.