TikTok kinara wa kupakuliwa mtandaoni
Kwa mwezi Agosti, mtandao huo umepakuliwa na watu zaidi ya milioni 60 na hivyo kuongoza miongoni mwa programu za simu zisizo za michezo.
- Kwa mwezi Agosti, mtandao huo umepakuliwa na watu zaidi ya milioni 60 na hivyo kuongoza miongoni mwa programu za simu zisizo za michezo.
- Mtandao huo umechauna vikali na Zoom ambayo ilikuwa kimbilio la mawasiliano wakati wa janga la Corona.
- Licha ya umaarufu wa FaceBook, WhatsApp na Instagram, hazijafua dafu kwa TikTok.
Dar es Salaam. Licha ya misukosuko iliyopata ikiwemo kufungiwa nchini Marekani, programu tumishi (App) ya mtandao wa kijamii wa TikTok imeendelea kuvunja rekodi ya kupakuliwa na kutumiwa na watu wengi duniani.
App hiyo ya kupakia video za burudani inayomilikiwa na kampuni ya ByteDance ya nchini China inaongoza kupakuliwa miongoni mwa programu za simu zisizo za michezo (non-gaming) duniani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na taasisi ya maendeleo ya programu za simu ya Sensor Tower, TikTok imeshika nafasi ya kwanza katika upakuaji wa programu tangu mwezi Mei, 2020 ikitokea nafasi ya pili iliyoshika mwezi Aprili.
App hiyo inayopatikana katika mifumo endeshi ya simu za iPhone na Android imevunja rekodi hiyo baada ya kujizolea watu zaidi ya milioni 63.3 kufikia mwezi Agosti huku ikiiacha kwa mbali mitandao mingine maarufu ikiwemo Facebook, Instagram na WhatsApp.
Sensor Tower imeeleza kuwa kuwa TikTok ambayo ilianza kutumiwa mwaka 2016 imepakuliwa zaidi kwenye maduka ya mtandaoni ya Play Store na App Store.
Zoom imeshika nafasi ya pili baada ya kupakuliwa na watu milioni 52.2, ikifuatiwa na Facebook ambayo imeshuka kutoka namba mbili mwezi Julai.
Huenda mafanikio ya muda mfupi ya Zoom yametokana na athari za ugonjwa wa Corona (COVID-19) ambao uliwafanya watu wengi kuwasiliana kwa njia ya mtandao ili kuepuka mikusanyiko.
Nafasi ya nne imeshikiliwa na mtandao wa Instagram huku tano bora ya orodha hiyo imefungwa na WhatsApp.
Soma zaidi
- Ushindani nguo za mtumba, dukani unavyowafaidisha wanunuzi Tanzania
- Ujasiriamali: Abuni jukwaa la mtandaoni kurahisisha manunuzi Tanzania
- Tanzania yaweka tozo mpya kwa watalii 2020-21
App zingine zinazokamilisha kumi bora ni pamoja na App ya simu za video ya Google Meet katika nafasi ya sita ikifuatiwa na app ya video za burudani ya Snack Video na namba nane imeshikiliwa na Facebook Messenger.
Orodha hiyo imeiweka app ya Snapchat kama namba tisa huku 10 bora ikifungwa na mtandao wa kijamii wa Telegram.
Huenda mitikisiko inayoikumba TikTok sasa hasa kutakiwa kuondoka Marekani kwa sababu za kiusalama, ndiyo imeipatia umaarufu kwa watu wengi kuipakua ili kujua nini kinaendelea ndani ya mtandao huo.