Google yafuta apps zaidi ya 20 zilizokuwa zikidukua taarifa Facebook
App hizo zilikuwa zimepakuliwa na watumiaji zaidi ya 250,000 na zilikuwa zikifanya kazi yake kama kawaida licha ya kuwa na ajenda ya siri wakati zikifanya kazi.
- App hizo idadi yake ni 25 na zimejizolea maelfu ya watumiaji.
- Kwa mujibu wa wataalamu, zimekuwa sokoni kwa zaidi ya miaka miwili.
- Unashauri kama unatumia ni vema ukazifuta ili kujiweka salama.
Dar es Salaam. Duka la programu tumishi la Google Play Store limeondoa programu tumishi 25 kwenye mfumo wake baada ya programu hizo kubainika kuiba taarifa za watumiaji wa mtandao wa Facebook waliokuwa wamepakua app hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tovuti ya Znet, app hizo zilikuwa zinatumiwa na wadukuzi kuiba taarifa za Facebook kutoka kwa watumaiji wake zikiwemo maneno ya siri.
Vuguvugu hilo limetokea baada ya kampuni ya nchini Ufaransa inayoshughulika na usalama wa kimtandao ya Evina kubaini sintofahamu ya app hizo.
Evina imesema, app hizo zilikuwa zimepakuliwa na watumiaji zaidi ya 250,000 na zilikuwa zikifanya kazi yake kama kawaida licha ya kuwa na ajenda ya siri wakati zikifanya kazi.
Kampuni hiyo ya usalama wa mtandaoni pia imesema, hatari ni kwamba, baadhi ya app hizo zikiwemo File Manager na Health Step Counter zimekuwa kweye Google Play Store kwa zaidi ya miaka miwili kabla ya kuondolewa na hivyo kuwia vigumu kufahamu kiwango cha maafa kilichofanyika.
Endapo umepakua app yoyote kati ya hizo, unashauriwa kuzifuta na kubadili neno siri la mtandao wa FaceBook. Picha| Rodgers George.
Hata wakati app hizo zikitolewa kutoka duka la Play Store, bado utahitaji kuzifuta kutoka kwenye simu yako wewe mwenyewe.
Mtaalamu wa masuala ya teknolojiaya mawasiliano Jensen Seth ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa mara nyingi virusi programu (malware) ndiyo hutumika na wadukuzi kufanya kazi hizo.
Seth amesema kirusi programu maarufu kwa jina la Trojan ndiyo hutumika zaidi huku kikiambatanishwa na apps au tovuti ambazo hukuomba ruhusa ya kuhusiana na vitu mbalimbali vikiwemo mahali (location) na mawasiliano (contacts).
“Ukikubali tu unakuwa umewafungulia mlango kuhusiana na taarifa zako,” amesema Seth.
Zinazohusiana
- Apps 10 za kilimo zinazoweza kuwanufaisha wakulima Tanzania
- ‘Apps’ za elimu zinavyoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule
- Zijue App 42 zinazohatarisha betri la simu yako
Zaidi, mtaalamu huyo ameshauri kwa mtu ambaye tayari anajihisi amepakua kati ya app hizo, ni muhimu kuhamisha (backup) taarifa zake na kufuta kila kitu.
“Kuzuia mara nyingi kama ni kompyuta tumia “antivirus” (kudhibiti virusi) kujua kama ipo na kama inaweza kutolewa kwa antivirus kama antivirus ikishindwa backup data zako na futa kila kitu,” ameshauri mtaalamu huyo.