October 7, 2024

Kwanini umeme hukatika baada ya swichi kuu kujizima?

Swichi kuu ni kifaa cha umeme ambacho kinapokea umeme kutoka kwenye chanzo cha umeme na kisha kuusambaza kuelekea kwenye vifaa vya umeme nyumbani, ofisini na viwandani.

  • Swichi kuu ni kifaa kinachosambaza umeme ndani ya nyumba baada ya kuipokea kutoka kwenye chanzo. 
  • Kifaa hicho hujizima pale unapotokea muingiliano wa umeme katika jengo.
  • Unashauriwa kuita fundi ili kurekebisha changamoto iliyotokea na siyo kulazimisha kuiwasha swichi kuu.

Dar es Salaam. “Ni nini kimetokea?” ni kati ya maswali mengi ambayo watu hujiuliza pale swichi kuu (main switch) inapojizima na umeme kukatika nyumbani au ofisini. 

Swichi kuu ni kifaa cha umeme ambacho kinapokea umeme kutoka kwenye chanzo cha umeme na kisha kuusambaza kuelekea kwenye vifaa vya umeme nyumbani, ofisini na viwandani.

Lakini kuna wakati swichi hiyo hujizima na kuacha maswali kwa watumiaji wake, ni kwa nini hilo limetokea.

Kwanini umeme hukatika endapo swichi hiyo ikijizima?

Fundi umeme kutoka kampuni ya vifaa vya umeme ya Susuma Traders Morogoro Daniel Susuma amesema kifaa kinachofanya umeme kukatika ni “circuit breaker” ambacho kinajizima baada ya kutokea muingiliano wa umeme katika jengo ama eneo hilo.

“Mfumo wa umeme ulivyotengenezwa hautakiwi kuingiliana. Endapo sehemu yeyote aidha makutano ya waya au sehemu ambapo umeme unaenda iwe taa, soketi na hata friji ikapata muingiliano, itarudisha taarifa kwenye swichi kuu.

“Ili kuepukana madhara yatakayojitokeza na ule muingiliano ikiwemo kuungua kwa kifaa, circuit breaker(iliyopo ndani ya swichi kuu) inajizima,” ameelezea Susuma.

Zaidi, swichi hiyo itaendelea kujizima hadi pale utakapotatua muingiliano na changamoto iliyojitokeza katika eneo husika.

“Kama wewe sio mtaalamu wa umeme, unashauriwa kuita fundi umeme ili afuatilie ni wapi kuna shida. Usilazimishe kuwasha hiyo swichi bila kujua tatizo ni nini,” amesema Susuma.


Zinazohusiana


Hata hivyo, Ushauri mwingine aliotoa mtaalamu huyo ni pamoja na kuzingatia ubora wa swichi hiyo wakati wa manunuzi, ukubwa wa jengo lako na ukubwa wa matumizi yako ya umeme.

“Nashauri uangalie ubora wa kampuni zinazozalisha hicho kifaa na ukubwa wa matumizi ya jengo lako kwa sababu main switch (swichi kuu) zimegawanyika kutokana na ukubwa wa matumizi,” amesema mtaalam huyo.

Una swali gani na ungependa kufahamu? Wakati unajibu hilo kupitia barua pepe yetu ya newsroom@nukta.co.tz na mitandao ya kijamii, usicheze mbali, wiki ijayo tutaangazia matumizi ya viyoyozi.