November 24, 2024

Startups sita zilizochangia kupunguza Corona Tanzania

Wabunifu hao wamejikita katika kubuni teknolojia na mifumo ya kidijitali inayorahisisha tiba ya ugonjwa huo lakini wengine wametengeneza programu tumishi (Apps) kuwasaidia wanafunzi kusoma wakati huu ambao wako nyumbani.

  • Startups hizo ni Jenga Hub, Zaidi Recyclers, Tai Tanzania, Mtabe App, Bits and Bytes na Visual Aided Stories.
  • Zimekuwa mstari wa mbele kutoa suluhisho za teknolojia kupambana na Corona. 
  • Wadau wajipanga kuziongezea nguvu kuwafikia watu wengi zaidi.

Dar es Salaam. Licha ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) kuathiri shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi duniani, umekuwa ni fursa kwa wabunifu wa teknolojia kuibuka na suluhu mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huo.

Wabunifu hao wamejikita katika kubuni teknolojia na mifumo ya kidijitali inayorahisisha tiba ya ugonjwa huo lakini wengine wametengeneza programu tumishi (Apps) kuwasaidia wanafunzi kusoma wakati huu ambao wako nyumbani. 

Kutokana na umuhimu wa wabunifu hao, Mfuko wa Ubunifu na Maendeleo ya Watu (HDIF) umezichagua kampuni sita za teknolojia zinazochipukia (startups) Tanzania ambazo zimekuwa mstari wa mbele kukabiliana na COVID-19 ili kuzijengea uwezo zaidi. 

Startups hizo za Tanzania ni Jenga Hub, Zaidi Recyclers, Tai Tanzania, Mtabe App, Bits and Bytes na Visual Aided Stories.

Zilipatikana katika shindano maalum la “HDIF Covid-19 Responsive Challenge” liliandaliwa na mfuko huo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID, kampuni ya Seedspace Dar es Salaam na kituo cha Ubunifu cha Ifakara.

Washindi hao watapatiwa zawadi ya pesa na wataunganishwa katika programu ya utayari wa uwekezaji (Investment ready program) pamoja na kupata nafasi ya kufanyia kazi zao katika ofisi ya Seed Space.

Hiyo itawapa fursa ya kupata mafunzo zaidi ili kuendeleza kazi zao na kuifikia jamii kwa upana zaidi. 

Kampuni ya kuchakata taka za karatasi ya Zaidi Recyclers wamebuni ngao ya uso kwaajili ya watu kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona pale wanapokuwa kwenye mikusanyiko. Picha| Zaidi Recyclers.

Kwanini zimechaguliwa?

Startups hizo zimejikita zaidi katika kutatua changamoto za afya, elimu zilizojitokeza hasa kwa wanafunzi na vijana wakati huu wa COVID-19. 

Mathalan, Mtabe App imekuwa ikiwasaidia wanafunzi kusoma masomo ya darasani wakiwa nyumbani kwa kutumia simu zao za mkononi hasa zenye mtandao wa WhatsApp na hata kuwafikia wale wasiokuwa na intaneti.

Mbali na Mtabe, Kampuni inayojihusisha na kurejeleza taka za karatasi ya Zaidi Recyclers yenyewe ilijikita kutengeneza ngao za kufunika uso ili kuwasaidia wafanyakazi kujikinga dhidi ya Corona wanapokuwa katika shughuli zao. 

Mkurugenzi Msaidizi na Meneja wa Uzalishaji wa Zaidi Recyclers, Esther Matiku amesema mara baada kuripotiwa kwa ugonjwa wa Corona nchini Tanzania, kitu cha kwanza kilikuwa ni kufikiria namna ya kuwakinga wafanyakazi. 

“Tulianza kutengeneza ngao za uso kwa malighafi za plastiki kuwauzia watu wa kawaida na wawatumishi wa sekta ya afya,” amesema Matiku.


Zinazohusiana


Mkurugenzi wa Tai Tanzania Ian Tarimo amesema waliibuka na wimbo wa miondoko ya kisingeli wa “Chapa Corona” uliolenga kuelimisha jamii kuhusu kujikinga na Corona hasa kwa watu ambao wanashindwa kufikiwa na habari kwa kukosa intaneti.

“Tuliamua kutafuta vijana kutoka kwenye jamii yao, wakaandika mashairi, tukaingia studio, tukarekodi wimbo unaondana na jamii zao,” amesema Tarimo.

Amesema ushindi huo utawapatia nafasi ya kuendelea kuihudumia zaidi jamii ya Watanzania hasa kutumia njia rahisi ya katuni kuelimisha vijana. 

Wakati Tai Tanzania wakitumia wimbo,  Visual Aided Stories wametumia sanaa kuelimisha jamii kupitia michoro ya ukutani kuelimisha umma kuchukua tahadhari ya kujikinga na COVID-19.

Ushindi wa startups hizo ni chachu kwa vijana wengine kubuni suluhisho litakalosaidia jamii kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakumbuka na siyo tu Corona.