October 7, 2024

Facebook yaingiza programu mpya ya muziki sokoni

Hatua hiyo imekuja siku chache tangu mtandao huo uzindue app ya Catchup inayowezesha simu za sauti kwenye makundi.

  • Ni app ya Collab ya kutengeneza na kuangalia muziki wa video.
  • Itachuana vikali na TikTok inayotamba kwa video fupi.
  • Kwa sasa iko kwenye majaribio.

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa muziki unaendelea kuingia katika kila sekta na kuwa sehemu muhimu ya kuwaburudisha na kuwafurahisha watu rika tofauti duniani.

Hatimaye Facebook imeingia katika tasnia ya muziki kwa kuanzisha program tumishi ya simu  (App) itakayowawezesha watumiaji kutengeneza muziki na kuusambaza kwa watu mbalimbali.

Hatua hiyo imekuja siku chache tangu mtandao huo uzindue app ya Catchup inayowezesha simu za sauti kwenye makundi.

Kwa mujibu wa tovuti ya Social Media Today, timu ya majaribio ya bidhaa (NPE) ya  Facebook imeanza  kuipitia bidhaa hiyo mpya ili kwenda sambamba na mahitaji ya watu kwa sasa.

App hiyo ya Collab (music collaboration app) inawawezesha watumiaji kutazama, kurekodi na kuchanganya pamoja vipande vya muziki wa video ili kupata vionjo tofauti tofauti.


Zinazohusiana


Vipande hivyo wanaweza kuvipakia kutoka kwenye simu zao na kutengeneza muziki uliokamilika wa sekunde 15.

“Muziki ni njia yenye nguvu kufikisha ujumbe. Collab inatumia teknolojia kuwasaidia watu kuvumbua ubunifu wao kwa muziki halisi wa video,” imeeleza Facebook.

Facebook imeeleza kuwa hiyo inaweza kuwa njia muhimu kuimarisha mahusiano na mawasiliano ya watumiaji wake.

Collab inaingia katika ushindani na app ya TikTok ambayo imekuwa ikitumiwa zaidi na  watu wanaopenda kutengeneza video fupi mtandaoni.

Hata hivyo, watumiaji wa Collab wanatakiwa wawe wabunifu kutengeneza muziki wa video wenye ujumbe unaotosheleza sekunde 15.

Kwa sasa app hiyo iko kwenye majaribio katika nchi za Canada na Marekani.