Facebook yaibuka na app nyingine kuwaunganisha watu mtandaoni
Ni app ya Catchup inayowezesha upigaji wa simu miongoni mwa marafiki walio tayari kuchati kwenye makundi ya mtandao huo.
- App hiyo ya Catchup inasaidia kujua nani yuko mtandaoni kwa ajili ya kuchati.
- Inarahisisha mazungumzo ya sauti kwa marafiki na makundi ya mtandao huo.
- Kwa sasa inafanyiwa majaribio nchini Marekani.
Katika kukidhi mahitaji ya mawasiliano ya watumiaji wake, Facebook imezindua programu tumishi (App) mpya inayowezesha upigaji wa simu miongoni mwa marafiki walio tayari kuchati kwenye makundi ya mtandao huo.
App hiyo ya CatchUp inawawezesha watumiaji wa makundi hayo kufahamu nani yuko mtandaoni ili kumpigia simu na kujiunga na mazungumzo yanayoendelea kwenye kundi husika.
“Kukutana imekuwa siyo rahisi. Sasa unaweza kujua nani yuko mtandaoni na ukachati naye au kuingia katika mazungumzo ya kundi. Huna haja ya kuweka miadi, muda wowote unaweza kuzungumza,” inaeleza Facebook katika maelekezo ya app hiyo.
Pia ndani ya app hiyo watumiaji wanaweza kutengeneza ujumbe wa “status” kuwafahamisha wengine kuwa wako tayari kuchati na kutengeneza makundi ya kuendeleza mazungumzo mbalimbali.
Ni njia nyingine ya kujumuika na watu licha ya kuwa watu wanatumia app ya Messenger yenye chaguo la kutumia simu za video.
Zinazohusiana:
- Zawadi ya Mark Zukerberg: Facebook kuwakutanisha makapela mtandaoni
- Facebook yafanya maboresho utafutaji wa bidhaa mtandaoni
Uzuri wa app hiyo ambayo unatakiwa kuipakua kwenye simu yako inawezesha kuwaona watu waliopo kwenye kundi ambao wako tayari kwa ajili ya mazungumzo ya sauti.
Programu hiyo itawasaidia watu katika maeneo yenye changamoto ya mtandao na ambako mawasiliano ya simu ni njia muhimu ya kuunganisha watu.
Kwa sasa, app hiyo inafanyiwa majaribio nchini Marekani kwa simu zote zinazotumia mfumo endeshi wa iOS (iPhone) and Android.